NA FARIDA MANGUBE, MOROGORO
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Kighoma Malima amewataka vijana katika kijiji cha Lubungo kuchangamkia fursa za uwekezaji katika sekta ya kilimo, kuzalisha mazao ya biashara kupitia mradi wa kilimo cha mazao ya bustani kibiashara chini ya Programu ya Beyond Farming Collective (BFC) unatekelezwa na Ushirika wa Wahitimu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUGECO).
Mhe, Malima ameyasema hayo katika kijiji cha Lubungo wakati akizundua mradi wa BFC ambapo ameipongeze SUGECO kwa kutekeleza mradi huo kwa vitendo huku akiwataka wadau wote kuendelea kutekeleza mradi huo ili kuyafikia malengo ya kukifanya Kijiji cha Lubungo kuwa cha mfano katika uzalishaji wa kisasa wa mazao ya bustani.
Aidha ameitaka SUGECO kutenga heka 100 kwajili ya malisho ya wafugaji na 200 kwa wajili ya wakulima ili kuondoa mwingiliano kati wakulima na wafugaji wakati wa kutekeleza mradi huo na kumaliza kabisa migogoro ya wakulima na wafugaji kijiji hapo.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa SUGECO Mr. Revocatus Kimario amesema mradi huo unagharimu zaidi ya shilishi Bilioni 1.13 ambapo unaenda kuwanufaisha vijana zaidi ya 1,820 ambao watajikita katika kuzalisha mazao ya biashara kama matikiti maji, vitunguu na matango na mazao mengine.
Kimario amesema mradi huo utakuwa na miundombinu yote ya uzalishaji wa kisasa hivyo ni wajibu wa vijana na wakazi wa kijiji cha Lubungo waliopata fursa kutumia mradi huo kuzalisha mazao ya bustan huku akiwahakikishia kuwepo kwa masoko ya uhakika wa mazao yatakayozalishwa.
Naye Katibu Tawala Msaidizi sehemu ya Uchumi na Uzalishaji Mali Dkt. Rozalia Rwegasira amewataka wananchi wa Kijiji cha Lubungo kuupokea mradi huo kwa mikono miwili ambapo amesema utawasaidia kulima kilimo chenye tija, pia ameitaka taasisi ya SUGECO kuendelea kutoa elimu kwa wananchi wanaozunguka eneo la mradi kulima mazao yatakayowapa kipato.