Kabla hujaanza kutumia Majira, jiulize kama ni njia sahihi kwako

Dar es Salaam. Tunaambiwa na wataalamu wa uzazi wa mpango kwamba, zipo njia nyingi zinazoweza kutumika, lakini wanawake wengi huamua kutumia njia ya vidonge vya uzazi wa mpango, maarufu kama ‘vidonge vya majira.’

Hata hivyo, wengi wanatumia vidonge hivi bila ushauri wa kitabibu na bila kufanyiwa vipimo, hivyo kukosa elimu na mwongozo mzuri kuhusu afya ya uzazi na matumizi salama ya njia hiyo.

Ingawa kuna njia nyingine kama kitanzi, vijiti na kalenda, baadhi ya wanawake huona vidonge kama njia rahisi na inayopatikana kwa urahisi, bila kutambua kuwa matumizi ya kiholela yanaweza kuhatarisha mfumo wa uzazi. Matumizi haya yasiyo ya kitaalamu yanawaweka wanawake wengi katika hatari ya matatizo ya kiafya kama vile unene uliopitiliza, uvimbe kwenye kizazi, matatizo ya mfumo wa hedhi na kuongeza hatari ya magonjwa, yakiwamo ya kisukari, shinikizo la damu na kipandauso.

Kwa mujibu wa mtaalamu wa magonjwa ya wanawake na uzazi, Dk Isaya Mhando kabla ya kuanza matumizi ya vidonge vya uzazi wa mpango mwanamke anapaswa kuchukua tahadhari.

Anasema anapaswa kutotumia sigara, asizidi miaka 35 lakini pia asiwe na shinikizo la damu, shambulio la moyo, saratani ya matiti au historia ya ndugu wa karibu aliyewahi kupata saratani ya matiti.

Tahadhari nyingine anayoitoa kabla ya matumizi ya vidonge hivyo ni kwa wenye magonjwa yasiyoambukiza ya moyo, ini, historia ya kuwa na upasuaji mkubwa ambao ulikulazimu kutotembea kwa muda mrefu, upasuaji wa kutengeneza tumbo, kisukari, matumizi ya dawa za kifua kikuu aina ya Rifampin na magonjwa ya kifafa.

“Na kwa mama aliyejifungua, anapaswa kusubiri angalau wiki tatu zipite tangu kujifungua ndipo aanze matumizi ya vidonge hivyo vya uzazi wa mpango,” anasema daktari huyo.

Aidha, kupitia tafiti mbalimbali, ikiwemo ile ya National Institutes of Health ya mwaka 2016, imethibitisha vidonge hivyo siyo chaguo sahihi kwa wenye magonjwa yasiyoambukiza kama kisukari, shinikizo la damu, saratani ya matiti na mengine mengi.

Maria Raphael (28), mkazi wa Ubungo Maziwa jijini Dar es Salaam anasimulia mkasa wake wa matumizi holela ya njia za uzazi wa mpango uliomsababishia kupata athari.

Anasema baada ya kupata mimba akiwa na umri wa miaka 23, bila kuwa na uhakika wa baba halisi wa mtoto wake, maisha yake yalibadilika ghafla.

Akawa mtu mwenye mawazo mazito, akiwa na mchanganyiko wa fikra hasi na chanya kuhusu ujauzito huo usio na baba.

“Nilikuwa na mawazo mengi sana kwa sababu ya ujauzito nilioupata bila kutarajia. Familia nzima ilinilaumu na nikawa mtu wa kulia muda wote. Niliapa kutorudia kosa hilo,” anasimulia.

Anasema siku zilisogea na miezi ikaenda na hatimaye ukafika muda wa kujifungua. “Namshukuru Mungu niliweza kuhimili yote na nikajifungua mtoto wa kike salama.”

Anasema baada ya kujifungua hakutaka kubeba ujauzito tena, kwa wakati ule.

“Kutokana na viapo vyangu vya kutorudia kosa, nilishirikisha marafiki zangu ili wanishauri ni njia gani ya uzazi wa mpango niitumie kwa kipindi chote cha kumlea mwanangu, kila rafiki alinishauri njia yake, lakini niliona njia ya vidonge ni rahisi kuliko nyingine kutokana na upatikanaji wake na matumizi yake hayakuwa na ulazima wa kwenda hospitali,” anasema Maria.

Anasema baada ya ushauri huo kutoka kwa marafiki zake, alienda duka la dawa na kununua vidonge vya majira, “Sikuulizwa maswali, kitu ambacho niliona ni rahisi sana na sahihi kwa wakati huo.”

Anasema aliuziwa dawa hizo bila kupimwa wala kuulizwa kama ana uelewa wa namna ya kutumia vidonge hivyo au kama alishawahi kuvitumia awali.

“Nilianza kuvitumia, mwezi wa kwanza ilifanya kazi japokuwa siku zangu za kupata hedhi zilikuwa hazieleweki, mara itoke nyingi, mara kidogo mara nisipate kabisa, ikawa vurugu tupu,” anasema Maria.

Anasema aliwauliza marafiki zake kuhusu hali hiyo na wakamjibu kuwa ni ya kawaida awe na amani.

Anasema aliendelea kuvitumia, lakini ilipotimia miezi mitatu, aliona mabadiliko mengi ambayo yalimpa hofu.

“Hedhi yangu ilibadilika na kuwa ya kahawia (brown) huku ikiwa katika mfumo wa mabonge makavu, ambayo ukiyapasua unakuta chenga chenga kavu mfano wa udongo,” anasimulia.

“Mwezi unaofuata ikaja hedhi ya mfumo huohuo lakini nyeusi, nilishtuka ila niliona haina shida huenda ni tatizo la kawaida hasa unapotumia vidonge hivyo huku baadhi ya marafiki wakiendelea kuniaminisha ni kawaida na wachache waliona ni tatizo.”

Anasimulia kuwa siku moja alihisi kutojisikia vizuri na akaamua kwenda hospitali kufanya vipimo vya malaria na homa.

“Nilimweleza daktari ninavyo jisikia, akaniandikia vipimo, lakini kabla ya kwenda kupima nikaona si mbaya nimwelezee hiki ninachokipitia, alinisikiliza na kuniongezea kipimo cha utrasound ili kujua hali ya tumbo kwa ndani.”

Maria anasema baada ya vipimo aligundulika kuwa ana vimbe za sentimita 34 kwenye mirija ya uzazi, licha ya kutokuwa na maumivu yoyote ya tumbo.

Anasema majibu hayo yalimshtua sana, daktari akamuuliza maswali na pia akamweleza sababu zinazoweza kuwa chanzo cha tatizo lake.

Anasema miongoni mwa vyanzo inaweza kuwa matumizi holela ya vidonge hivyo vya uzazi wa mpango bila kufuata utaratibu sahihi.

“Akaniuliza kama nimewahi kutumia njia hiyo, ilinibidi niseme ukweli juu ya matumizi hayo ili nipate msaada, aliniuliza pia kama nilifanya vipimo nikamwambia hapana,” anasimulia Maria.

Anasema baada ya hapo, daktari huyo alimpatia elimu juu ya matumizi sahihi na tahadhari zinazopaswa kuchukuliwa kabla ya kuanza kutumia vidonge hivyo ili kuepuka madhara.

“Katika maelezo hayo aliniambia kuna watu hawapaswi kabisa kutumia njia za uzazi wa mpango kutokana na hali zao za kiafya na historia za familia,” anaeleza Maria na kuongeza;

“Baada ya kunipa elimu hii, nikakumbuka hata kwenye familia yetu kuna watu wanaugua magonjwa yasiyo ya kuambukiza, hivyo nikajisemea moyoni, kumbe sikupaswa kutumia njia hiyo ya uzazi wa mpango.”

Maria anasema alijutia hilo, ingawa alipata tiba ya upasuaji ili kuondoa vimbe zilizogundulika, lakini hajabahatika kupata mtoto mwingine mpaka sasa, licha ya kuwa kwenye ndoa.

Dk Mhando anasema magonjwa ya saratani ya matiti au wenye historia ya ugonjwa kwenye familia, kuna dawa hawapaswi kuzitumia, vikiwamo vidonge vya homoni (majira).

Anasema marufuku hiyo inakuja kutokana na aina za vichocheo kama estrogen, receptors ambayo ipo kwenye vidonge vya majira, hugeuka kuwa kichocheo na lishe kwenye seli za saratani, sukari na hukuza kasi ya magonjwa hayo yanayoleta madhara kwa haraka.

“Lakini pia kuna ugonjwa wa kipanda uso, mtu mwenye ugonjwa huu hapaswi kutumia vidonge vya uzazi wa mpango, vidonge hivi huwa na tabia ya kuchochea maumivu zaidi ya kichwa,” anasema mtaalamu huyo wa magonjwa ya wanawake.

Kadhalika, anasema wanawake wenye umri wa kuanzia miaka 35, hawapaswi kutumia njia hizo za uzazi wa mpango.

“Licha ya marufuku hizo, lakini pia Shirika la Afya Duniani (WHO) limetoa miongozo ya njia kuu nne za matumizi hayo ya uzazi wa mpango.

“Kundi la kwanza ni wale ambao baada ya vipimo vya hospitali wameonekana hawana kikwazo kama vile magonjwa, hivyo wanaruhusiwa kufanya matumizi ya njia hizo, watu hawa wanaruhusiwa kwa asilimia 100 kutumia njia hizo,” anasema.

Anataja kundi la pili ni la wale ambao baada ya vipimo vya hospitali kuonyesha faida za matumizi ya vidonge ni kubwa kuliko madhara yatakayo jitokeza baada ya matumizi, wanaruhusiwa kutumia njia ya uzazi wa mpango kwa asilimia 100.

Kundi la tatu ni la wale ambao baada ya vipimo wamebainika kuwa na tatizo na wakitumia njia za uzazi wa mpango, watapata madhara, lakini hana jinsi ni lazima atumie.

Watu hawa watatumia njia hizo huku hofu kubwa ikiwa ni kupata madhara muda wowote.

Kundi lingine la wanawake wanaotumia njia za uzazi wa mpango ni wale wasioruhusiwa kutumia njia hizo.

“Wasioruhusiwa ni pamoja na wanawake wenye jinsia mbili, watu hawa hawaruhusiwi kufanya matumizi hayo, huku madhara makubwa yatakayojitokeza ni magonjwa ya maambukizi katika via vya uzazi, yaani PID.

“Wengine ni wanawake wenye mishipa kwenye mapaja, hasa upande wa nyuma wa magoti, hawa hawaruhusiwi kufanya matumizi hayo, wakitumia madhara yake ni kupanuka kwa mishipa hiyo na kusababisha damu nyingi kubaki miguuni na sehemu nyingine za mwili kukosa damu ya kutosha,” anasema Dk Mhando.

Related Posts