USHINDI wa mabao 3-1 iliyopata Tabora United dhidi ya Yanga katika mechi ya Ligi Kuu Bara, imewawawezesha mastaa wa timu hiyo kuvuna kitita cha Sh 20 Milioni kutoka kwa Mkuu wa Mkoa wa Tabora Paul Chacha.
Nyuki hao wa Tabora waliifumua Yanga katika mchezo uliopigwa kwenye Uwanja wa Azam Complex, jijini Dar es Salaam kwa mabao mawili ya Offen Chikola na jingima la Nelson Munganga na kuwa ushindi wa kwanza kwa timu hiyo dhidi ya Yanga, lakini wa tatu mfululizo katika ligi hiyo msimu huu kwa sasa.
Awali RC Chacha aliahidi kama Tabora ikishinda mchezo huo angewazawadia fedha hizo na nyota wa timu hiyo wakafanya kweli kwa kuiadabisha Yanga kwa mara ya kwanza kati ya michezo minne waliowahi kukutana katika michuano tofauti ikiwamo mitatu ya Ligi Kuu na mmoja wa Kombe la Shirikisho.
Tabora ilifungwa 3-0 katika mechi ya kwanza msimu uliopita kisha kulala tena 1-0 ziliporudiana Dar es Salaam, mbali na kipigo cha 3-0 katika robo fainali ya Kombe la Suirikisho pia ya msimu uliopita.
Kipigo hicho cha pili mfululizo kwa Yanga msimu huu tena ikiwa nyumbani ni kimeipa Tabora fedha hizo ambapo mkuu huyo wa mkoa amesema timu ikiwasili fedha hizo atazikabidhi kwa wachezaji kwa ushindi walioupata ili waongeze hamasa ya kushinda michezo mingine zaidi.
RC Chacha amesema awali waliahidi timu hiyo ikishinda mchezo wowote wa Ligi Kuu ikiwa ugenini watapewa bonasi ya 10 Milioni, lakini kwa kuifunga Yanga dau limepanda na sasa watapewa 20 milioni kama zawadi ya kutikisa nchi.
Akizungumza na Mwanaspoti, Mkuu wa Mkoa wa Tabora huyo amesema mpango wa timu hiyo ni kwamba kila atakayekanyaga uwanja wa Alhasan mwinyi afungwe ili timu hiyo imalize Ligi kwenye nafasi za juu.
“Tumejipanga kwamba kila atakayekuja hapa tumfunge bao za kutosha na uwezo huo tunao kwakua tangu tunafanya usajili tulihakikisha kwamba tunasajili wachezaji bora ambao wanaweza kucheza na kutupa matokeo hivyo wapinzani wajipoange,” amesema Chacha.
Baadhi ya mashabiki wa Tabora wakiwakilishwa na Emmanuel Vedastus wamesema hawakutegemea timu yao kuishangaza Yanga kutokana na ubora ambao wapinzani wao hao wamemuwa nao tangu kuanza kwa msimu huu wa Ligi.
“Tunawapongeza wachezaji kwa kujitoa na kutupa ushindi kwa tulivyocheza mechi mbili hapa nyumbani mwanga ulionekana wa kuifunga Yanga japokua hatukua tukijua kama tuyafunga bao nyingi kiasi hiki ila tumeandika historia kama Tabora kuwa timu ya kwanza kuifunga Tabora mabao memgi msimu huu” alisema
Hata hivyo Vedastus amesema msimu jana walihujumiwa kwa mchezo wao wa nyumbani kupelekwa jijini Dodoma, lakini kama mchezo ule ungechezwa Ali Hassan Mwinyi wangefungwa nyingi.
Baada ya mchezo huo Yanga imeendelea kusalia nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu ikiwa na pointi 24 kutokana na michezo 10 sawa na Simba inayoongoza ikiwa na pointi 25, huku Singida Black Stars ikishika nafasi ya tatu na pointi 23.