Amri ya kupeleka ndege Amsterdam imetolewa kutokana na machafuko hayo yaliyojiri muda mfupi baada ya mchezo wa ligi ya Ulaya kati ya Ajax Amsterdam iliyoibuka mshindi kwa magoli matano kwa sifuri dhidi ya Maccabi Tel Aviv kwenye uwanja wa mpira wa Johan Cruyff.
Baada ya amri hiyo ya Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu, jeshi la Israel limetangaza kupeleka ndege mbili kuwaondoa mashabiki wa Israel kwa kushirikiana na serikali ya Uholanzi.
Soma zaidi: Rais wa Israel alaani mashambulizi mjini Amsterdam
Mashuhuda katika tukio hilo walichukua picha za video zikilionesha kundi la wanaume mbele ya stendi kuu ya Amsterdam wakiwakimbiza watu wengine huku sauti za ving’ora vya magari ya polisi zikisikika. Polisi mjini humo imesema ilimeshawakamata watuhumiwa 62 kuhusiana na tukio hilo. Watu watano wako hospitalini kutokana na majeraha yaliyotokana na mapambano.
Kulingana na taarifa ya polisi, awali mashabiki waliondoka uwanjani bila ya lolote kutokea lakini machafuko yaliibuka usiku katikati ya mji. Vyombo vya habari vya Israel na wanasiasa wameyataja machafuko hayo kuwa mabaya zaidi kushuhudiwa Uholanzi tangu vita vya Gaza vilipoanza zaidi ya mwaka mmoja uliopita.
Netanyahu: Ukatili uliofanyika Amsterdam hautapuuzwa
Taarifa ya ofisi ya Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu imesema picha zilizojaa ukatili kuhusu tukio hilo la Amsterdam dhidi ya raia wake halitapuuzwa.
Rais wa Israel Isaac Herzog amesema mashambulizi hayo yanaibua kumbukumbu ya mashambulizi yaliyofanywa na kundi la Hamas mwaka jana pamoja na mashambulizi ya chuki dhidi ya Wayahudi wa Ulaya katika karne zilizopita.
Naye Waziri Mkuu wa zamani wa Israel Naftali Bennet amelizungumzia tukio hilo na kusema kuwa, Wayahudi wanashambuliwa katika maeneo kadhaa kwa nguvu ya kikatili Amsterdam na kukiita kinachoendelea kuwa ni mauaji ya kikabila. Bennet ametoa wito kwa mamlaka za Uholanzi zichukue hatua haraka ili kuzuia vifo na majeruhi zaidi.
Kwa upande wake Waziri Mkuu wa Uholanzi Dick Schoof amesema tukio hilo linapaswa kulaaniwa vikali na kwamba kila liwezekanalo linapaswa kufanyika ili kuwakamata na kuwashtaki wahusika.
Naye Waziri wa mambo ya kigeni wa Israel Gideon Saar amezungumza na mwenzake wa Uholanzi Caspar Veldkamp akiiomba serikali ya Uholanzi iwasaidie raia wake kuwasili salama katika uwanja wa ndege wakati ndege za Israel zitakapofika kuwachukua.