Dodoma. Serikali imekamilisha awamu ya kwanza ya ujenzi wa jengo la kuwahifadhi wahisiwa wa magonjwa ya kuambukiza lililopo katika mpaka wa Mutukula Wilaya ya Missenyi Mkoa wa Kagera ambalo limegharimu Sh140 milioni.
Hayo yamesemwa leo Ijumaa Novemba 8, 2024 wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalumu (CCM) Benardetha Mushashu.
Katika swali la msingi, Mushashu amehoji ni lini Serikali itakamilisha ujenzi wa jengo la kuwatenga walioathirika na magonjwa ya mlipuko Kagera.
Akijibu swali hilo, Dk Mollel amesema Serikali imekamilisha awamu ya kwanza ya ujenzi wa jengo la kuwahifadhi wahisiwa wa magonjwa ya kuambukiza lililopo katika mpaka wa Mutukula Wilaya ya Missenyi, Mkoa wa Kagera ambalo limegharimu Sh140 milioni.
“Kwa sasa jengo hilo limekamilika na limewekewa huduma za maji, umeme, kuwekewa vitanda na tayari limeanza kutumika kuwahifadhi wanaohisiwa kuwa na magonjwa ya kuambukiza,” amesema.
Amesema katika mwaka wa fedha 2024/25, Sh80 milioni kimetengwa kwa ajili ya maboresho ya sehemu ya nje ya jengo hilo ikiwamo kuweka sehemu yenye kivuli (lounge) kwa ajili ya wasafiri, pamoja na uwekaji wa viyoyozi na samani nyingine kwa ajili ya utoaji wa huduma.
Katika maswali ya nyongeza, Mushashu amehoji Serikali ina mpango gani wa kujenga majengo hayo katika vituo vya Lusumo na Kabanga mkoani Kagera.
Pia, amesema kwa kuwa Mkoa wa Kagera umepakana na nchi jirani kadhaa na hivyo ni rahisi kupata magonjwa ya maambukizi.
“Ni lini itatimiza ahadi yake ya kujengea hospitali kubwa ya magonjwa ya kuambukiza ili wagonjwa watakaobainika katika hizo hospitali wapate matibabu kwenye hospitali hizo,” amesema.
Akijibu maswali hayo, Dk Mollel amesema fedha zinaendelea kutafutwa kwa ajili ya kujenga majengo kama hayo katika maeneo mengine ya mipakani ili kunapofika magonjwa ya mlipuko katika nchi nyingine waweze kujikinga.
Kuhusu ujenzi wa hospitali maalumu ya magonjwa ya kuambukiza, Dk Mollel amesema Mkoa wa Kagera una hospitali kubwa ya mkoa na kuwa Serikali inaendelea kupanuliwa ili hospitali hiyo iwe kubwa zaidi.
“Kikubwa sio kujenga hospitali kubwa ya magonjwa ya kuambukiza bali ni kuhakikisha magonjwa hayo hayaingii nchini. Jinsi uhitaji utakapooneka tutakwenda kuyafanya hivyo,” amesema.