Madiwani walia uchakavu Shule ya Msingi Litembe

Mtwara. Zaidi ya wanafunzi 260 wa Shule ya Msingi Litembe iliyopo katika Kata ya Madimba Halmashauri ya Wilaya ya Mtwara wako hatarini kutokana na uchakavu wa majengo wanayotumia.

Akizungumza katika kikao cha Baraza la Madiwani kilichofanyika leo Novemba 8, 2024 Diwani wa Kata ya Madimba, Idrissa Kujebweja amesema hatua za haraka zisipochukuliwa kuiboresha, shule hiyo ifungwa.

“Tuchukue hatua za haraka, twendeni kuwanusuru wale watoto hasa kipindi hiki cha mvua ambapo wanakuwa katika mazingira magumu zaidi kwa kweli.

“Hali ya miundombinu ya shule ya Litembe ni mbaya, inatupasa tuweke mpango mkakati wa haraka kuinusuru tusipofanya hivyo mwakani hawataweza kusomea katika madarasa yale,” amesema Kujebweja.

Diwani wa Kata ya Ndumbwe, Abdul Mahupa, amekubaliana na diwani huyo, akiiomba halmashauri kuchukua hatua za dharura kuboresha shule hiyo.

“Lazima tuungane ili kuhakikisha shule hiyo inaboreshwa na kuwafanya walimu na wanafunzi wanakuwa katika mazingira bora zaidi ya kusomea,” amesema Mahupa

Hata Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Mtwara Vijijini, Abeid Kafunda amekiri kuwepo kwa changamoto ya uchakavu wa shule hiyo.

Amesema tayari wameanza kufanya mawasiliano na Ofisi ya Rais, Tamisemi ili kupeleka mradi wa Boost, ingawa mradi huo umekuwa ukilenga shule zenye wanafunzi wengi.

“Tunaendelea kufanya jitihada za kuwasiliana na Tamisemi kwa ajili ya mradi wa Boost, hata hivyo mradi huu unahudumia shule zenye wanafunzi wengi, tofauti na shule zetu zenye idadi ndogo ya wanafunzi. Tunaendelea kufikiria njia mbadala.”

Aidha, Kafunda ameongeza kuwa halmashauri inafikiria kutumia fedha za ndani zitakazopatikana kwa ajili ya ukarabati wa shule kongwe ili ziweze kutumika kwa ukarabati wa Shule ya Msingi Litembe.

Related Posts