Dodoma. Serikali inapendekeza kufanya marekebisho katika Sheria ya Uhamiaji, Sura ya 54 ikilenga kutatua changamoto katika utekelezaji wa masharti kuhusu hadhi maalumu kwa diaspora.
Mapendekezo ya marekebisho hayo yamo katika Muswada wa Marekebisho ya Sheria Mbalimbali namba 4 wa mwaka 2024 ambao umewasilishwa bungeni leo Novemba 8, 2024.
Naibu Spika, Mussa Zungu ameupeleka kwenye Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria kwa ajili ya uchambuzi.
Katika muswada huo, kifungu cha 3 kinapendekezwa kurekebishwa kwa kuongeza tafsiri ya misamiati ‘Kadi ya Tanzanite Diaspora’, ‘hadhi maalumu’ na ‘Tanzania non-citizen diaspora’ lengo la marekebisho likiwa ni kuyafanya masharti yanayopendekezwa kuongezwa yaeleweke kwa urahisi zaidi.
Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Hamza Johari katika kifungu cha 28 cha muswada wa sheria hiyo anapendekeza kurekebishwa ili kuongeza masharti mapya ya ruhusa ya kuingia nchini kwa kutumia Kadi ya Tanzanite Diaspora na taarifa ya idhini ya kupewa kadi hiyo.
“Lengo la marekebisho hayo ni kumwezesha mmiliki wa Kadi ya Tanzanite Diaspora na mgeni ambaye ana taarifa ya kuidhinishwa kuingia ndani ya Jamhuri ya Muungano kutumia nyaraka hiyo bila kuathiri takwa la kuwa na pasipoti halali,” inaelezwa katika madhumuni ya muswada huo.
Sheria inapendekezwa kufanyiwa marekebisho kwa kuongeza vifungu vya 36A, 36B, 36C, 36D na 36E kwa ajili ya kuweka masharti yanayohusu hadhi maalumu kwa raia wa nchi nyingine ambaye aliwahi kuwa raia wa Tanzania au mwenye asili ya Tanzania.
Masharti hayo yanakusudiwa kutumika kwa mtu ambaye alikuwa raia wa Jamhuri ya Muungano, isipokuwa kwa wale waliokuwa na uraia wa kuasili, au mtu ambaye mzazi wake mmoja, babu, bibi au mtu yeyote katika kizazi kilichomtangulia ni, au alikuwa raia wa Jamhuri ya Muungano.
Kwa mujibu wa vifungu vipya vinavyopendekezwa, pale ambapo mtu anapewa hadhi maalumu, hadhi hiyo itamwezesha kuingia katika Jamhuri ya Muungano na kushiriki katika shughuli za kiuchumi na kijamii.
Hadhi maalumu itaenda sambamba na kupata Kadi ya Tanzanite Diaspora ambayo itakuwa ni uthibitisho rasmi kwamba mmiliki wa kadi hiyo ana hadhi maalumu. Vilevile, masharti mapya yanayopendekezwa yanaainisha masuala kuhusu muda wa uhalali, wategemezi na masharti na utaratibu wa kufutwa kwa Kadi ya Tanzanite Diaspora.
Kifungu cha 45 kinapendekezwa kurekebishwa kwa kuongeza neno ‘Kadi’ marekebisho yakilenga kuainisha adhabu kwa makosa yatakayotendwa na wamiliki wa Kadi ya Tanzanite Diaspora kama ilivyo kwa wamiliki wa visa, vibali, vyeti na hati za kusafiria vinavyotolewa chini ya Sheria.
Kifungu cha 48 kinapendekezwa kurekebishwa kwa kuongeza eneo ambalo Waziri anaweza kulitengenezea kanuni ili kujumuisha utaratibu wa uombaji na utoaji wa hadhi maalumu. Lengo la marekebisho haya ni kuwezesha utekelezaji bora wa masharti ya sheria.
Muswada huo pia unapendekeza marekebisho katika Sheria ya Mawakili, Sheria ya Utekelezaji wa Haki za Msingi na Wajibu, Sheria ya Huduma za Jamii, Sheria ya Shirika la Soko la Kariakoo, Sheria ya Ardhi, Sheria ya Madini na Sheria ya Utumishi wa Umma.
Katika muswada huo Serikali inapendekeza kufanya marekebisho katika Sheria ya Ardhi, ambapo kifungu cha 19 kinapendekezwa kufanyiwa marekebisho kwa lengo la kuweka utaratibu wa matumizi ya ardhi kwa mtu aliyepewa hadhi maalumu chini ya Sheria ya Uhamiaji.
“Kwa mujibu wa marekebisho yanayopendekezwa, mtu aliyepewa hadhi maalumu atakuwa na haki ya kumiliki ardhi kupitia utaratibu wa hati miliki maalumu itakayotolewa na Kamishna wa Ardhi,” amesema Johari.
Amesema lengo la marekebisho hayo ni kumwezesha raia wa kigeni mwenye asili ya Tanzania kumiliki au kuondosha miliki ya ardhi aliyoipata kwa njia mbalimbali ikiwemo urithi au kununua.
Hati miliki maalumu itakuwa aina ya hati miliki itakayotolewa kwa vigezo na masharti maalumu.
Serikali inapendekeza kufanyia marekebisho kifungu cha 32 cha sheria hiyo ili kuainisha muda wa hati miliki maalumu itakayotolewa kwa mtu aliyepewa hadhi maalumu, kwa mujibu wa marekebisho haya hatimiliki maalumu itakayotolewa na Kamishna wa Ardhi kwa mtu aliyepewa hadhi maalumu itakuwa kwa muda usiozidi miaka 33.
Kifungu cha 20A kinapendekezwa kuongezwa na vifungu vya 48 na 49 vinapendekezwa kurekebishwa kwa lengo la kuweka utaratibu wa kutoa na kusitisha hatimiliki maalumu iliyotolewa kwa mtu aliyepewa hadhi maalumu.
Nafuu kwa wanaojifungua watoto njiti
Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Ajira na Uhusiano Kazini umesomwa kwa mara ya kwanza bungeni, miongoni mwa mambo yanayorekebishwa ni kifungu cha 33 kichohusu likizo ya uzazi.
Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Ridhiwani Kikwete katika muswada huo amesema kifungu hicho kinapendekezwa kurekebishwa ili kuongeza muda wa likizo ya uzazi kwa mwajiriwa ambaye amejifungua mtoto njiti.
Amesema marekebisho hayo yanapendekeza kujumuisha katika likizo yake ya uzazi muda uliobaki kufikia wiki thelathini na sita za ujauzito.
“Lengo la marekebisho haya ni kulinda ustawi na afya za watoto wanaozaliwa kabla ya wakati na kuhitaji muda wa kutosha wa uangalizi wa mama,” amesema.
Amesema kifungu cha 34A kinapendekezwa kuongezwa ili kumwezesha mwajiri kumpatia mwajiriwa likizo bila malipo isiyozidi siku 30.
“Lengo la marekebisho haya ni kuweka mazingira mazuri yatakayomwezesha mwajiriwa kupata likizo bila malipo kutokana na majanga au dharura zinazoweza kujitokeza,” amesema.
Akitoa hoja ya kuahirisha mkutano Bunge leo Novemba 8, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameagiza wizara zote kuandaa kwa wakati taarifa za utekelezaji wa maazimio yote kulingana na mapendekezo yaliyotolewa na Kamati za Bunge kuhusu ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa mwaka ulioishia Juni 30, 2023 na kuziwasilisha Ofisi ya Waziri Mkuu ili iweze kuwasilisha taarifa ya Serikali kwa Spika wa Bunge.
“Napenda kuwakumbusha maofisa masuuli na watendaji wote serikalini kuhakikisha kuwa wanazingatia sheria, kanuni na taratibu za fedha za umma ili kutimiza ndoto na malengo ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kuwaletea Watanzania maendeleo endelevu,” amesema.
Majaliwa ametoa rai kwa wakulima wote, kutumia mvua kulima mazao yanayoendana na upatikanaji wa mvua katika maeneo yao na kuzingatia ushauri wa wataalamu wa kilimo.
Pia amewataka kujenga tabia ya kufuatilia taarifa za utabiri wa hali ya hewa na kuzingatia maelekezo yanayotolewa na Serikali ikiwemo kuhama kwenye maeneo hatarishi na kufanya shughuli za kiuchumi na kijamii katika maeneo salama.
Ameagiza viongozi wa mikoa na wakurungezi wa halmashauri zote kusimamia kikamilifu ujenzi wa miundombinu kwa ajili ya kuwapokea wanafunzi ifikapo Januari, 2025 ili kuhakikisha wanaanza masomo kwa wakati mmoja.
Kuhusu mikopo ya elimu ya juu, ili kukabiliana na ongezeko la wahitaji, amesema Serikali inaangalia uwezekano wa kuishirikisha sekta binafsi katika ugharimiaji wa elimu ya kati na ya juu. Bunge limeahirishwa hadi Januari 28, 2025
“Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuwakumbusha maofisa masuuli na watendaji wote serikalini kuhakikisha kuwa wanazingatia sheria, kanuni na taratibu za fedha za umma ili kutimiza ndoto na malengo ya Rais Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya kuwaletea Watanzania maendeleo endelevu,” amesema Majaliwa.