Mwanza. “Wakati nikifanya kazi katika shirika fulani, tulitembelea shule moja jijini Mwanza na kukuta wapishi wakiwa wanapeana zamu jikoni. Mmoja anaingia na kupuliza moto, kisha anakimbia kumpisha mwenzake ili kukabiliana na moshi. Hili lilinisikitisha sana,” anasema Bernard Makachia, mbunifu wa JikoSMART.
Akizungumza na Mwananchi kwenye mahojiano maalumu kuhusu wazo la kuja na majiko hayo lilipotoka, anasema kuwa mateso ya wapishi katika shule waliyoitembelea yalimsukuma kubuni jiko la kisasa na kuni mbadala zinazotengenezwa kwa kutumia mabaki ya mimea.
“Niliumizwa sana na hali ile. Mmoja wa wale wapishi nilikutana naye baada ya muda, na aliniambia ameacha kazi kwa sababu alikuwa akisumbuliwa na kikohozi kisichopona kinachodhaniwa kusababishwa na moshi wa kuni,” anasema Makachia.
Kutokana na changamoto hizo, Makachia anasema mwaka 2019 alianza ubunifu wa kutengeneza mkaa mbadala kwa kutumia maboksi kwenye kiwanda chake kilichopo Kijiji cha Katumba Kata ya Kisesa wilayani Magu mkoani Mwanza, mkaa ambao hata hivyo haukuleta matokeo aliyotarajia kwani ufanisi wa moto wake ulikuwa hafifu huku ukichafua mazingira.
“Nililazimika kutumia malighafi nyingine zinazopatikana kama taka kavu ikiwemo mabaki ya mimea, maranda ya mbao, mabaki ya mpunga, kahawa na miwa ambazo zinapatikana kwa wingi.”
Anasema malighafi hizo ziliwawezesha kuzalisha KuniSMART ambazo zina ufanisi na upatikanaji wake ni rahisi ikilinganishwa na kuni na mkaa. “Nilipokuwa nikiziwasha moto wake unawaka haraka, mkali na usiotoa moshi unaochafua mazingira, ndipo wazo la kuziita KuniSMART lilipoanzia na niliita hivyo kwa sababu tunataka asili ya kuni zetu iendelee kuwepo,” anasema.
Safari moja huanzisha nyingine, Makachia hakuishia hapo, anasema baada ya kubuni KuniSMART, alibaini huenda zisiwe na ufanisi katika kutokomeza matumizi ya mkaa na kuni zisizo rafiki kwa mazingira kutokana na miundombinu ya majiko yanayotumiwa nchini.
Mbunifu huyo alianza utekelezaji wa wazo la utengenezaji wa jiko mbadala (banifu) litakalotumia kuni hizo na lenye uwezo wa kuhudumia idadi kubwa ya watu kwa wakati mmoja, mwaka 2022 alifanikiwa kulikamilisha.
Kwa mujibu wa Makachia, JikoSMART alilolitengeneza kwa kutumia malighafi zinazopatikana nchini baada ya kuwasha moto kwenye KuniSMART, mtumiaji anaweza kuongeza moto kwa kuunganisha feni maalumu iliyowekwa ndani ya jiko hilo, kwenye umeme ama Sola ya Jua na moto kuwaka maradufu.
“Yawezekana mtumiaji akawa anahitaji kupika chakula kiive haraka zaidi, nimesanifu na kuweka feni maalumu ndani ya jiko ambayo inawashwa kwa kutumia chaja ya simu ya batani. Unaichomeka kwenye soketi ya umeme ama sola inapuliza upepo na kuongeza moto ambao hautoi moshi kabisa,” anasema.
Mbunifu huyo anasema kilo moja ya KuniSMART inayouzwa Sh500 ina uwezo wa kupika chakula cha watu 10 hadi 15, “Chakula hicho endapo kingepikwa kwa kutumia kuni ama mkaa mpishi atalazimika kutumia zaidi ya Sh3,000”. Kuhusu gharama ya JikoSMART, Makachia anasema hutofautiana kulingana na ukubwa ambapo mhitaji hutengenezewa jiko kuanzia Sh50,000, Sh70,000, Sh100,000, kwa majiko ya kutumika katika familia, huku taasisi zikitengenezwa majiko ya kuanzia Sh150,000 hadi Sh300,000.
Wanaotumia majiko wafunguka
Scholastica Joseph, ni mpishi katika Shule ya Awali ya Vision iliyopo Kata ya Nyanshishi Wilaya ya Misungwi mkoani humo, anasema matumizi ya majiko banifu hayo yanapunguza gharama na muda wakati wa kuandaa chakula.
“Tangu nimeanza kutumia majiko na kuni hizo natumia saa moja kupika chakula cha wanafunzi 60 ikilinganishwa na wastani wa saa tatu mpaka nne nilizokuwa nikitumia kupika chakula hicho kwa nishati na majiko mengine.”
“Unapowasha jiko haichukui hata dakika tano linawaka na moto wake umekolea kabisa ikilinganishwa mkaa wa kawaida ambapo nilikuwa nachukua muda mwingi kuwasha moto hadi ukolee,” anasema Scholastica.
Akizungumzia unafuu huo, Makachia anasema tangu kuanza ubunifu huo amefanikiwa kusambaza JikoSMART na kuni zake katika taasisi za elimu zaidi ya 15 mkoani Mwanza, ambapo amedai baada ya kufanya tathimini wamebaini kupunguza gharama za matumizi ya kuni kutoka wastani wa Sh1.2 milioni kila mwezi hadi Sh800,000.
Jitihada kusambaza ubunifu, ajira
Makachia anasema kupitia ubunifu wa kuni na jiko hilo alishiriki mashindano ya ubunifu wa nishati safi yaliyoratibiwa na Shirika la Kimataifa la Maendeleo (UNDP) la ‘Energy Efficiency Innovation Challenge’ na kuibuka miongoni mwa washindi 10 wa ubunifu wa nishati mbadala.
Anasema baada ya kuibuka mshindi, UNDP ilimpatia zabuni ya kutengeneza majiko 300 ifikapo mwishoni mwa Oktoba. Majiko hayo yatatolewa bila malipo kwa wafanyabiashara wadogo wakiwamo mamalishe, babalishe, wakaanga chipsi na familia zinazotumia kuni na mkaa usio rafiki kwa mazingira, ambapo wameshaanza kuyatengeneza.
Makachia anasema kwa sasa ana vijana watano aliowaajiri moja kwa moja na wengine zaidi ya 10 wanaokusanya malighafi na amejipanga kusimika mashine ya kuzalisha kuna hivyo ataongeza vijana na kufikia 20.
Mpishi huyo (Scholastica) anasema kutokana na kuvuta moshi wa kuni kwa muda mrefu hujikuta akiugua kikohozi jambo linalopunguza ufanisi katika kazi yake.
Kuhusu athari zinazoweza kusababishwa na moshi wa kuni na mkaa, Mkuu wa Idara ya Saratani Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Bugando, Dk Nestory Masalu, anasema, “mbali na kurithi na kemikali, sababu nyingine inayochangia ugonjwa wa saratani ya mapafu kwa wagonjwa wanaobainika hospitalini hapo ni kuathiriwa na moshi unaotokana na matumizi ya kuni na mkaa.”
Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO) inakadiriwa kuwa takriban watu milioni 4.3 hufariki kila mwaka kutokana na uchafuzi wa hewa itokanayo na matumizi ya nishati ya kuni na mkaa ndani ya nyumba.
Habari hii imedhaminiwa na Bill & Melinda Gates Foundation.
Kama una maoni kuhusu habari hii, tuandikie ujumbe kupitia WhatsApp: 0765864917.