Simba yatuma salamu kAngola, yaituliza Bravos mapema

HIZI ni habari njema kwa Simba ambayo inajiandaa kuivaa timu ya Onze Bravos katika hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika na mashabiki wa Msimbazi watapenda kuzisikia.

Simba imepanda kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu Bara baada ya kuwa na mwenendo mzuri wa matokeo na haitacheza mechi yoyote nyingine ya kimashindano hadi itakapoivaa Bravos, sasa hizi ni taarifa njema.   

Kitendo cha kuongoza msimamo wa Ligi Kuu Bara, kinaiweka Simba katika hali nzuri kisaikolojia katika maandalizi yao ya mchezo dhidi ya Onze Bravos katika hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika, lakini habari njema zaidi ni mwendo wa kusuasua wa wapinzani hao ndani ya Ligi Kuu ya Angola ‘Girabola’.

Wakati Simba ikiwa kileleni ikiwa na pointi 25 ilizovuna katika mechi 10, Bravos inashika nafasi ya nne katika msimamo wa Ligi Kuu Angola ikiwa imepata pointi 13 katika michezo minane iliyocheza hadi sasa.

Simba inaonekana kutamba kitakwimu za ligi ya ndani mbele ya Bravos jambo ambalo hapana shaka litaifanya isiingie kinyonge katika mechi ya kwanza ya hatua ya makundi dhidi ya timu hiyo ya Angola, Novemba 28 kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.

Hadi sasa, Simba imeangusha pointi tano katika mechi 10 ilizocheza za Ligi wakati huo Onze Bravos imeangusha 11 kupitia michezo minane iliyocheza hadi sasa katika Ligi Kuu Angola.

Pointi 25 ambazo Simba imekusanya katika mechi 10, imeifanya iwe na wastani wa kupata pointi 2.5 kwa mchezo wakati huo pointi 13 ambazo Bravos imezivuna katika mechi nane za  Gilabora, zinaifanya timu hiyo ya Angola kuwa na wastani wa pointi 1.6 kwa mchezo.

Idadi hiyo ya pointi 25 za Simba, imekusanywa kwa timu hiyo kupata ushindi katika mechi nane, kutoka sare moja na kupoteza moja wakati idadi ya pointi 13 za Onze Bravos katika Ligi Kuu ya Angola imepatikana baada ya kupata ushindi mara tatu, kutoka sare mara nne na kupoteza mchezo mmoja.

Katika takwimu za mabao ya kufunga, Simba imeiacha Bravos kwenye mataa kwani imefumania nyavu mara 21 katika mechi 10 ikiwa ni wastani wa mabao 2.1 kwa mechi huku wapinzani wao hao kutoka Angola, kwenye ligi ya kwao, wamefunga mabao 10 katika michezo minane ikiwa ni wastani wa bao 1.3 kwa mechi.

Safu ya ulinzi ya Simba inaonekana kufanya vizuri zaidi katika kuzuia kulinganisha na ile ya Onze Bravos kwa kuzingatia mechi ambazo kila moja imecheza kwenye ligi yake.

Simba imeruhusu nyavu zake kutikiswa mara tatu tu katika Ligi Kuu Bara ikiwa ni wastani wa bao 0.3 kwa mechi wakati huo Onze Bravos imefungwa mabao saba katika Girabola yanayofanya iwe na wastani wa kuruhusu bao 0.9 kwa mchezo.

Pamoja na kuwa na takwimu bora kwenye ligi ya ndani kulinganisha na wapinzani wao, kocha wa Simba, Fadlu Davids alisema kuwa timu yake inapaswa kuweka uzito mkubwa katika maandalizi ya kuikabili Onze Bravos, Novemba 28 kwani mechi haitokuwa rahisi.

“Akili yetu sasa itajikita huko kwenye shirikisho. Kwetu sisi makocha tutakuwa na muda wa kujua kila taarifa za wapinzani wetu juu ya ubora wao lakini huku tukiendelea na maandalizi taratibu.

“Tunatakiwa kuanza vizuri, ikiwezekana kwa ushindi mkubwa na bila kuruhusu bao. Kitu muhimu hapa ni sisi kutumia nafasi tutakazotengeneza, kwa sababu hizi ni mechi ambazo hazina nafasi nyingi,” alisema Fadlu.

Simba ina kibarua cha kuhakikisha inatinga hatua ya nusu fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika baada ya kuishia katika hatua ya robo fainali ya mashindano tofauti ya klabu Afrika mara nne mfululizo.

Related Posts