BAADA ya kupoteza namba katika kikosi cha kwanza chini ya Miguel Gamondi, beki wa kulia wa Yanga, Kibwana Shomari amedaiwa kuomba kuondoka klabuni hapo katika dirisha dogo la usajili litakalofunguliwa mwezi ujao.
Kibwana aliyeitumikia Yanga kwa misimu miwili kwa mafanikio chini ya Nasreddine Nabi amepoteza namba mbele ya Yao Kouassi, aliye majeruhi kwa sasa nafasi kikosini kwa hivi sasa inachezwa na winga Denis Nkane.
Chanzo cha kuaminika kutoka kwa rafiki wa karibu wa mchezaji huyo kimeliambia Mwanaspoti, Kibwana ameandika barua ya kuomba kutolewa kwa mkopo katika dirisha dogo linalofunguliwa katikati ya Desemba na kufungwa Januari mwakani.
“Ni kweli hana furaha ndani ya kikosi hicho kutokana na kupoteza nafasi ya kucheza, sio kikosi cha kwanza tu, hapati namba kabisa hivyo ameandika barua ili atoke kwa mkopo dirisha lijalo,” alisema mtoa taarifa huyo na kuongeza;
“Timu ambazo zinatajwa kumuhitaji mchezaji huyo ni KMC, Singida Black Stars, japo lolote linaweza kutokea kwenda kati ya hizo timu au timu nyingine ambazo zitaonyesha nia ya kumuhitaji kwasababu mchezaji anataka sehemu ambayo atapata nafasi ya kucheza mara kwa mara ili kuboresha kiwango chake.”
Kibwana chini ya Gamondi hajapata nafasi ya kucheza mechi hata moja ya Ligi Kuu na amekuwa akikaa jukwaani, huku mechi na juzi dhidi ya Tabora United wakati watetezi hao wakilala mabao 3-1 alianzia benchini na hakupata dakika hata moja kucheza.
Wakati ikielezwa kuwa beki huyo wa kulia anapambana kuondoka katika dirisha dogo la usajili, endapo kocha Gamondi anayetajwa mbioni kuondolewa ndani ya Yanga kutokana na mwenendo usioridhisha wa timu, huenda uongozi ukamshawishi mchezaji huyo kubaki.
Beki huyo wa kulia mwanzoni mwa msimu huu aliongeza mkataba wa miaka miwili kuendelea kuitumikia timu hiyo hadi 2026 hivyo hatma ya kuondoka kwake ipo mikononi mwa uongozi wa timu hiyo kuamua kumuachia au kuendelea kusugua benchi. Alitua Jangwani akitokea Mtibwa Sugar.