SINGIDA Black Stars imeenda mapumziko ya Ligi Kuu ikiwa imeporomoshwa kileleni hadi nafasi ya tatu ya msimamo, lakini hilo halijamshtua kocha wa timu hiyo, kwani amesema anapiga hesabu kwa umakini ili ligi ikirudi tena wiki mbili zijazo aendelee na moto ule ule wa kujiweka katika mbio za ubingwa kwa msimu huu.
Katika kuonyesha hatanii, kocha huyo amekirudisha kikosi hicho mazoezini kujiandaa na mechi zijazo za ligi hiyo inayosimama kupisha kalenda ya mechi ya kimataifa kwa timu za taifa ili kukabiliana na ratiba ngumu.
Aussems alisema baada ya mchezo wa mwisho wa Ligi Kuu dhidi ya Coastal Union uliooisha kwa suluhu Novemba 2, aliwapa mapumziko ya siku nne kwa wachezaji kuungaa na familia na ndugu zao, kabla ya sasa kurejea kuendelea kujifua kujiweka fiti kwa vle vita ndio kwanza mbichi Bara.
“Nafikiri imekuwa wakati mzuri kwao kukaa na kufurahia na familia zao katika kipindi hiki ambacho Ligi imesimama kupisha michezo ya kimataifa, muda ni mchache hivyo tumerudi kwa haraka kuendelea na wale ambao hawakwenda timu zao za taifa.”
Kocha huyo aliongeza, katika kipindi hiki cha kupisha michezo ya kimataifa ataangalia uwezekano wa kupata angalau mechi za kirafiki ambazo zitakuwa maalumu kwao kuwajenga zaidi kutokana na ratiba ya michezo migumu iliyokuwa mbeleni mwao.
“Tunahitaji umakini kwa sababu muda ni mchache na ukiangalia ratiba sio rafiki kwetu, tuna michezo migumu ambayo sisi benchi la ufundi tunahitaji pia kujipanga ili tusiruhusu kupoteza pointi kama tulivyofanya kwa Yanga na Coastal Union.”
Singida ipo nafasi ya tatu na pointi 23, baada ya michezo 10 ikishinda saba, sare miwili na kupoteza mmoja, inakabiliwa na ratiba ngumu kwani itakuwa na wiki moja ya kucheza mechi tatu na kati ya hizo mbili ni za ugenini.
Ratiba inaonyesha baada ya wiki ya michezo ya kimataifa itakapoisha, Singida itasafiri hadi Ali Hassan Mwinyi Tabora kucheza na Tabora United Novemba 24 kisha kutaifuata Azam siku nne baaadae kabla ya kurudi nyumbani Uwanja wa Liti, Singida kuvana na Simba Desemba Mosi.