Bocco namba hazidanganyi hadi JKT Tanzania

JOHN Bocco, mshambuliaji ambaye ameandika historia ya kipekee kwenye soka la Tanzania, anaendelea kuthibitisha uwezo wake akiwa na JKT Tanzania.

Katika mechi dhidi ya Tabora United, alifunga mabao mawili na kuisaidia JKT kushinda mabao 4-2. Mabao hayo yamemfanya kufikisha 156 katika Ligi Kuu Bara na ndiye mfungaji bora wa muda wote.

Kwa zaidi ya muongo mmoja, Bocco amekuwa jina kubwa kwenye soka la Tanzania akifanya makubwa kwa klabu na timu ya Taifa aliyotundika daruga miezi michache iliyopita.

Mabao mawili aliyofunga dhidi ya Tabora United yanathibitisha bado ana makali licha ya umri kusonga mbele.

Kufikia 156 ni mafanikio makubwa na inamfanya kuwa mshambuliaji mwenye rekodi ya kufunga zaidi katika historia ya Ligi Kuu Bara na bado anaendelea kutesa.

Kuweka rekodi kama hiyo siyo jambo la kawaida na ni ushahidi wa muda mrefu wa juhudi zake za kuwa mshambuliaji wa hali ya juu.

Kwa takwimu za miaka ya hivi karibuni, amekuwa akifunga wastani wa mabao 12 hadi 15 kwa msimu, jambo linaloonyesha uthabiti katika soka.

Hata wakati alipokuwa akikumbwa na majeraha, alirudi kwa kasi na kuendelea kuwa tishio mbele ya lango la wapinzani.

Akiwa na uwezo wa kucheza kwa nguvu na akili kwenye eneo sahihi kwa wakati sahihi, amekuwa mshambuliaji wa aina yake.

Bocco amedumu kwenye kiwango cha juu cha soka kwa miaka mingi kutokana na nidhamu yake na kujituma  mazoezini. Kulinda mwili wake dhidi ya majeraha na kujiandaa kwa kila mechi, kumemfanya kuwa mchezaji wa kipekee.

Mara nyingi Bocco ameongelea jinsi anavyoweka mkazo katika mazoezi ya ziada, lishe bora, na maandalizi ya kisaikolojia ili kuhakikisha anadumu kwenye ubora wake.

“Soka ni zaidi ya kipaji; ni nidhamu na kujiandaa kila siku,” aliwahi kusema Bocco katika moja ya mahojiano.

Ameonyesha mfano mzuri kwa wachezaji wachanga kuhusu jinsi ya kujitunza ili kudumu kwa muda mrefu kwenye kiwango cha juu.

Pia, Bocco ana uwezo wa kujifunza na kubadilika kulingana na mazingira ya soka, jambo ambalo limemsaidia kufanikiwa kwenye timu mbalimbali.

Uhamisho wa Bocco kwenda JKT Tanzania haukukuwa tu faida kwa klabu hiyo, bali pia kwa mchezaji mwenyewe. Ameleta uzoefu mkubwa ndani ya kikosi cha JKT, hasa kwa wachezaji wachanga wanaojifunza kutoka kwake. Uwezo wake wa kufunga mabao na kuongoza safu ya ushambuliaji umeifanya JKT kuwa na timu yenye nguvu zaidi.

Mchango wake katika timu haumalizii tu kwenye ufungaji wa mabao, bali pia kwenye uongozi wa timu. Bocco ni kiongozi wa asili, mwenye uwezo wa kuhamasisha wenzake na kuweka nidhamu uwanjani. Hii ni faida kubwa kwa JKT Tanzania wanaoendelea kupambana kwenye ligi.

Bocco ataendelea kukumbukwa kama mshambuliaji mwenye uwezo mkubwa wa kufunga mabao, nidhamu ya hali ya juu na kiongozi bora uwanjani.

Mabao yake 156 yanaweka alama kubwa kwenye historia ya Ligi Kuu Tanzania Bara, na ni vigumu kuona mshambuliaji mwingine akifikia rekodi hiyo kwa haraka.

Kwa wachezaji wachanga, Bocco ni mfano wa kuigwa, si tu kwa uwezo wake wa kufunga, bali pia kwa nidhamu na juhudi alizoweka katika taaluma yake.

Mashabiki wa soka nchini wana kila sababu ya kumshukuru kwa mchango wake kwenye soka na jina lake litabaki katika kumbukumbu za historia ya soka la Tanzania kwa muda mrefu.

Kila anapokanyaga uwanjani, Bocco anaendelea kuthibitisha ni mshambuliaji wa aina yake, mwenye uwezo wa kubadili matokeo ya mechi. Kadri anavyoendelea kucheza, ni dhahiri atazidi kuongeza mabao na kujijengea urithi wa kuwa mmoja wa wachezaji bora kabisa waliowahi kucheza Ligi Kuu ya Tanzania Bara.

Bocco alianza safari yake ya soka akiwa na  Azam FC na aliibuka kuwa mmoja wa wachezaji muhimu. Uwezo wake wa kufunga mabao na kuongoza safu ya ushambuliaji ulimfanya kuwa kipenzi cha mashabiki.

Wakati akiwa Azam, Bocco aliisaidia timu hiyo kushinda taji la Ligi Kuu Bara mwaka 2014, pia alishinda mataji ya Kombe la Mapinduzi na Kombe la Shirikisho (FA Cup).

Baadaye alihamia Simba SC mwaka 2017 na aliongeza zaidi kiwango chake na kuchangia kwa kiasi kikubwa mafanikio ya timu hiyo. Akiwa Simba, alishinda mataji ya Ligi Kuu Bara mara nne mfululizo (2017-2021), pamoja na kushinda Ngao ya Jamii mara kadhaa.

Alikuwa mfungaji wa kuaminika na wakati mwingine aliongoza timu kama nahodha. Kati ya mwaka 2018 hadi 2022, Bocco alikuwa na msimu bora zaidi akiwa Simba na alifunga mabao muhimu kwenye mechi kubwa kama dabi ya Kariakoo dhidi ya Yanga na mashindano ya kimataifa kama Ligi ya Mabingwa Afrika.

Kocha Mohammed Badru, ambaye amewahi kumkabili Bocco akiwa kocha wa timu kadhaa kwenye Ligi Kuu Bara, alimsifu mshambuliaji huyo kwa nidhamu yake uwanjani.

“Bocco ni mfano bora wa mchezaji mwenye nidhamu na uongozi mzuri. Ameweza kudumu kwa muda mrefu kwenye kiwango cha juu kwa sababu anajua ni nini inahitajika kuwa mchezaji bora,” anasema Badru.

Kwa mujibu wa Badru, Bocco sio tu mchezaji mwenye kipaji cha kufunga mabao, pia ni kiongozi anayeweza kuwahamasisha wachezaji wenzake uwanjani.

Aliongeza kuwa Bocco ana uwezo mkubwa wa kufunga kutokana na akili yake ya mpira na uwezo wa kutumia nafasi.

Kwa upande wake, kipa wa Namungo, Beno Kakolanya, ambaye amekutana na Bocco mara kadhaa uwanjani, anamwelezea mshambuliaji huyo kuwa mmoja wa wachezaji wagumu zaidi kuwazuia uwanjani.

“Kama kipa, unapokutana na Bocco unajua kuwa unahitaji kuwa makini kila wakati. Ana uwezo wa kusoma mchezo vizuri na anajua jinsi ya kujipanga dhidi ya safu ya ulinzi,” anasema Kakolanya.

Kakolanya anaongeza Bocco ana uwezo wa kutengeneza nafasi zake mwenyewe hata kama anakuwa amezingirwa na mabeki.

“Hana haraka ya kufanya maamuzi mabaya. Anapopokea mpira, ana utulivu na anajua wapi na lini pa kupiga shuti. Hiyo ni sifa ambayo kila mshambuliaji bora anapaswa kuwa nayo.”

Related Posts