Uuzaji kemikali kiholela janga mtaani

Dar es Salaam. Katika mitaa ya Jiji la Dar es Salaam, uuzaji wa kemikali unafanyika pasipo kufuata taratibu za usajili, hivyo kuchochea madhara ya kiafya na kimazingira.

Kemikali hizi ni zile zinatumika kutengeneza bidhaa kama vile sabuni, batiki na dawa za kuondoa madoa kwenye nguo.

Mwananchi katika ufuatiliaji kwenye baadhi ya maeneo jijini hapa limezungumza na wafanyabiashara, wajasiriamali na wananchi waliozungumzia namna wanavyonunua kemikali hizo na kuzitumia.

Kurugenzi ya Huduma za Udhibiti ya Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu (GCLA) miongoni mwa majukumu yake ni kuratibu, kusimamia na kudhibiti uingizaji, uzalishaji, usafirishaji, utumiaji, utunzaji na uteketezaji wa kemikali.

Hayo yanafanyika ikiwa ni utekelezaji wa matakwa ya Sheria ya Usimamizi na Udhibiti wa Kemikali Na.3 ya Mwaka 2003, Sheria ya Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali Na.8 ya Mwaka 2016 na kanuni zake za mwaka 2020.

Kwa wauzaji na wanunuzi ni lazima kuwa na vibali kutoka GCLA inayosimamia udhibiti wa kemikali hatarishi kwa kuhakikisha wafanyabiashara wanatii vigezo vya usalama na afya ya umma.

Wafanyabiashara lazima wawe na eneo maalumu lenye vigezo vya usalama kwa ajili ya kuhifadhi kemikali ambazo zinapaswa kufungwa na kuwekwa lebo zinazotambulisha aina ya kemikali, tahadhari za usalama.

Muuzaji anapaswa kuhakikisha wateja wanapata maelezo ya kutosha juu ya matumizi salama ya kemikali kwa kuwapatia maelekezo ya usalama na kuwaelimisha juu ya tahadhari na utunzaji salama.

Wajasiriamali wengi wanaotengeneza bidhaa za sabuni (ya maji na miche hususani sabuni za magadi) na dawa za madoa, pia wanaotengeneza batiki hutumia kemikali.

Caustic soda au Sodium Hydroxide ni miongoni mwa kemikali zinazotumika ikiwa na uwezo wa kuchubua na kuyeyusha vitu.

Hutumiwa na wajasiriamali katika utengenezaji wa sabuni kuwezesha mchakato wa mafuta kugeuzwa kuwa sabuni, hutumika katika mchakato wa kutayarisha ngozi za wanyama kwenye viwanda vya ngozi, pia katika utengenezaji wa kemikali zingine.

Licha ya kuwa na faida, caustic soda inapaswa kutumika kwa tahadhari kwani ni hatari ikigusana na ngozi au macho, inaweza kusababisha kuungua au majeraha ya kudumu.

Kemikali nyingine ni sodium silicate (gundi ya glasi) ambayo haina rangi au yenye rangi hafifu, ina hali ya kimiminika au nzito kulingana na kiwango cha maji ndani yake.

Mbali na matumizi mengine ya viwandani, hutumika katika bidhaa za usafi kama ilivyo caustic soda. Pia hutumika kwenye matengenezo ya magari ili kuziba nyufa kwenye injini na radiator, kutengeneza glasi, karatasi, nguo na usindikaji wa ngozi.

Ikiwa na uwezo wa kuzuia maji, kuhimili joto kali na kuimarisha vifaa, matumizi yake pasipo tahadhari yanaweza kuleta madhara.

Kemikali nyingine ni sodium hypochlorite inayotumiwa na wajasiriamali kutengeneza bidhaa za usafi.

Kwa kawaida huwa ya kimiminika chenye harufu kali na rangi ya kijani hafifu au manjano. Hutumika kuua bakteria na virusi kwenye maeneo ya nyumbani, kuua vijidudu kwenye maji, kusafisha na kuua vimelea kwenye vifaatiba ili kuzuia maambukizi, kusafisha nguo kwa kuondoa madoa. Ikitumiwa vibaya inaweza kuchubua ngozi, macho, na hata kusababisha shida ya kupumua inapovutwa kwa kiwango kikubwa.

“Biashara ya kemikali ni nzuri kwetu kwa sababu inaleta kipato. Lakini ukweli ni kwamba, baadhi zinatumiwa vibaya na kuhifadhiwa vibaya na watumiaji,” amesema Juma Ali, mfanyabiashara wa kemikali katika soko la Kariakoo.

Haruni Moshi, anayeuza kemikali eneo la Mbagala anasema: “Changamoto katika kila biashara hazikosekani, najitahidi kwenda sawa na kibali cha biashara, nimekuwa nikitoa darasa namna sahihi ya kutumia na kuhifadhi.”

Asha Said, mjasiriamali anayetengeneza sabuni eneo la Mbagala anasema baadhi ya wauzaji hutoa kemikali hizo bila kujua iwapo mtu ana elimu ya matumizi yake.

“Mara ya kwanza nilikuwa nachukua katika kiwanda kimoja kilichopo Keko baadaye nikahamia katika duka moja la Kariakoo na kwa sasa nachukulia Mbagala Rangi Tatu, huku hatuulizwi juu ya vibali vya kutumia kemikali ukifika unasema unachokita unapewa na kuondoka,” anasema.

Anasema kemikali wanazotumia kutengenezea sabuni zina athari, hivyo kama si mtaalamu katika matumizi unapata madhara.

Asha anasema amewahi kupata muwasho wa ngozi na macho alipotumia kemikali hizo.

Kwa mujibu wa Asha, wengi wanaotumia kemikali hizo kutengeneza sabuni hawana maeneo maalumu, hivyo hufanya kazi nje au ndani wanapolala, wakihusisha watoto jambo ambalo ni hatari.

Baadhi ya wauzaji wa kemikali hizo huzifungasha kwenye chupa za maji zilizotumika.

Kutokana na baadhi ya kemikali kutokuwa na rangi na kuwa katika mfumo wa kimiminika, zinapofungashwa kwenye chupa hizo au zingine zikiwamo za soda na kutotunzwa vyema, husababisha madhara.

“Hakuna utaratibu rasmi wa kutoa vifungashio salama kwa wateja wa kawaida, kwa hiyo wengi hutumia chupa za zamani za vinywaji kwa kuwauzia Sh1,000 au Sh2,000,” anasema Rashid Juma, mfanyabiashara wa kemikali katika soko la Kariakoo.

Kemikali zikichanganywa kwenye ndoo kwa lengo la kutengeneza sabuni ya maji.

Hamis Abdallah, mkazi wa Temeke, anasema alikunywa kemikali iliyohifadhiwa kwenye chupa ya soda, akidhani ni kinywaji.

“Nilihisi kiu, nikaona chupa imewekwa mezani nikaamua kunywa, nilihisi maumivu makali kinywani na tumboni. Baada ya muda mfupi, nikaishiwa nguvu na kupelekwa hospitali,” anasema Hamis ambaye anaendelea na matibabu kwa majeraha ya ndani aliyopata.

Hussein Bakari, kijana wa miaka 20 anasema alikunywa kinywaji alichodhani ni juisi aliyoikuta jikoni bila kujua ni kemikali.

“Nilipokunywa nilihisi ladha kali na uchungu, ghafla nilianza kutapika na kuumwa tumbo hadi sasa ninapata maumivu nikila chakula,” amesema Hussein,

Aisha Juma, mama wa mtoto mwenye umri wa miaka minne, anakumbuka jinsi mwanawe alivyokunywa kemikali iliyohifadhiwa kwenye chupa ya maji.

“Mtoto aliokota chupa sebuleni na kuanza kunywa ndani ya sekunde chache alianza kukohoa na kulia kwani alikunywa kwa pupa, tulimpa maziwa kama huduma ya kwanza tukampeleka hospitali kwa matibabu zaidi,” amesema.

Kemikali za caustic soda, sodium silicate na sodium hypochlorite zinahitaji vifungashio maalumu kwa sababu ni kali na zinaweza kuathiri mazingira au kusababisha majeraha ikiwa itamwagika au kutofungwa vizuri.

Zinaweza kuhifadhiwa kwenye plastiki nzito, vifungashio vya glasi kwa Sodium Silicate, ambayo si kali sana ikilinganishwa na Caustic Soda au Sodium Hypochlorite, vifungashio vya glasi vinaweza kutumika lakini ni muhimu kuzuia mwanga mkali kwa baadhi ya kemikali kama Sodium Hypochlorite ambayo hupoteza ufanisi inapokabiliwa na mwanga.

Sabuni zikiwa tayari zimewekwa kwenye vidumu.

Vyombo vya chuma vilivyopakwa mipako maalumu vinaweza kutumika kwa baadhi ya kemikali kama sodium silicate, lakini hakifai kwa kemikali kama caustic soda, ambayo inaweza kushambulia chuma na kusababisha kutu. Pia zinapaswa kufungwa vizuri ili kutopitisha hewa na kutoweka eneo la joto.

Dk Lucy Mwakiposa, mtaalamu wa magonjwa ya mfumo wa mmeng’enyo wa chakula anasema kemikali zinapoingia mwilini huweza kusababisha kuchomwa kwa utando wa koo, tumbo na hata figo.

“Madhara yake ni makubwa na yanaweza kuhitaji matibabu ya muda mrefu. Wapo wagonjwa wanaopoteza uwezo wa kula kwa kawaida na hata kupata matatizo ya kudumu ya figo,” anasema.

Mtaalamu wa magonjwa ya ngozi, Dk Sophia Juma anasema wananchi wanapoumia kwa kutumia kemikali hizo, madhara yake huwa ya muda mrefu.

“Tunashuhudia watu wakiwa na matatizo ya ngozi, macho, na wakati mwingine hata mfumo wa kupumua kwa sababu ya kemikali zinazotumika katika mazingira yasiyokuwa na usalama,” anasema.

Anasema kwa wanaoweka kemikali kwenye chupa za maji wanatakiwa kupewa elimu kwa ajili ya kuwalinda watu wengine ambao wanafika na kunywa bila kujua.

Esther Kiungi, mfanyabiashara wa batiki eneo la Karume anasema huvaa glovu na barakoa kila anapotengeneza bidhaa zake.

“Ni muhimu kujikinga, lakini wateja na watumiaji wengi wa bidhaa hizi hawajali madhara ya kemikali hivyo tunahitaji elimu zaidi,” anasema.

Subira Omari, anayetengeza bidhaa hizo anasema huweka alama kwenye chupa zinazotumika kuhifadhi kemikali ili kuepusha madhara.

“Ninaandika kwenye chupa kuwa ni sumu na kuiweka mbali na watoto, lakini bado kuna hatari kwa wageni au wanafamilia wasiofahamu,” anasema.

“Kuna umuhimu wa kuelimisha jamii juu ya madhara ya kemikali hizi na kutoa maagizo kwa wafanyabiashara kuhakikisha kemikali zote zinafungashwa kwenye vyombo sahihi na vilivyo na alama za tahadhari kama ‘sumu’ au ‘hatari’ ili kuepusha ajali hizi,” amesema Dk Lucy.

Kwa upande wake, Dk Sophia anashauri Serikali kutoa mafunzo ya mara kwa mara kwa wafanyabiashara wa kemikali na wananchi wanaozitumia.

“Tunashauriwa kuwa na kampeni za uhamasishaji kwenye maeneo ya masoko, ambako wafanyabiashara na wateja wataelezwa kuhusu matumizi salama ya kemikali. Hii itasaidia kupunguza athari zinazoweza kuepukika,” amesema.

Mkemia Mkuu wa Serikali, Dk Fidelice Mafumiko amesema huwa wanatoa elimu kwa wadau wanaotumia kemikali, wakiwamo wajasiriamali kwa kushirikiana na Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (Sido).

“Tunasisitiza kama mtu anatumia kemikali ajitahidi kupata elimu maana kemikali hizi hatusemi ni mbaya kwa sababu zina manufaa kiuchumi na zikitumika vibaya si salama kabisa,” amesema.

Amesema kemikali zina manufaa mkubwa kwenye ukuaji wa uchumi na kwa wanaojishughulisha nazo kwani zipo za aina tofauti; zisizo na madhara makubwa na ambazo tabia zake zinaweza kuwa na madhara makubwa kama hazitatumika kwa usahihi na usalama. Hivyo, amesema watu wasitumie kemikali bila kujua tabia na madhara yake.

Dk Mafumiko amesema kila anayetumia kemikali ahakikishe ana kibali cha kuingiza au kununua kutoka kwenye mamlaka yao na zikiwa za hospitali kibali kiombwe kwa Mamlaka ya Dawa na Vifaatiba (TMDA).

Amesema usimamizi wa sheria upo na kwa yeyote anayetaka kujua matumizi sahihi ya kemikali aende kwenye ofisi za kanda za Mkemia Mkuu wa Serikali.

Kuhusu chupa za maji na soda kutumika kama vifungashio vya kemikali amesema watalifanyia kazi katika ufuatiliaji kwa kushirikiana na kanda, ikiwemo ya Dar es Salaam.

Related Posts