Ushindi wa Trump, joto kwa Prince Harry, Meghan

Dodoma. Kufuatia ushindi wa Donald Trump katika uchaguzi wa urais, Prince Harry na Meghan Markle wanaripotiwa kuwa na wasiwasi kuhusu maisha yao nchini Marekani, hasa kutokana na mabadiliko yanayotarajiwa katika sera za uhamiaji.

Ushindi wa Trump umeibua mjadala kuhusu iwapo Prince Harry na Meghan watakabiliwa na changamoto mpya za kisheria na za kiuhamiaji, hasa kutokana na taarifa za matumizi ya awali ya dawa za kulevya zilizotajwa katika kitabu chake cha Spare.

Kitabu cha Spare kinaelezea kumbukumbu ya Prince Harry, ambacho kilitolewa Januari 10, 2023. Kiliandikwa na J. R. Moehringer na kuchapishwa na Penguin Random House.

Ndani ya kitabu hicho, Harry amekiri kutumia dawa za kulevya kama bangi na kokeini wakati wa ujana wake.

Kwa mujibu wa sheria za uhamiaji za Marekani, watu wenye historia ya matumizi ya dawa za kulevya mara nyingi hukataliwa kuingia nchini humo, jambo linalofanya watu wengi kutilia shaka iwapo Harry alipatiwa upendeleo maalumu kwa kupewa viza.

Taasisi ya Heritage Foundation imekuwa ikifuatilia suala la viza ya Harry, ikidai kuwa utawala wa Rais Joe Biden ulikuwa na msimamo mwepesi kwa Harry tangu mwaka 2020 alipohamia Marekani na mkewe Meghan.

Wakurugenzi wa Heritage Foundation, akiwamo Nile Gardiner, wamesisitiza kuwa Harry anapaswa kutoa maelezo ya kina kuhusu ombi lake la viza, wakidai anapata upendeleo maalumu.

Gardiner ameeleza mwaka huu, Harry na Meghan hawakutoa kauli yoyote hadharani kuhusu uchaguzi wa Marekani, tofauti na uchaguzi wa mwaka 2020 walipoonekana kumuunga mkono Biden kwa kauli zao za kupinga hotuba walizoziita za chuki na habari za kupotosha walizodai zilitolewa na Trump wakati wa kampeni.

Hata hivyo, kwa sasa Gardiner amesema iwapo Harry hana cha kuficha kuhusu viza yake, basi anapaswa kuruhusu maelezo ya ombi lake yawe wazi kwa umma.

Septemba 2024, ombi la Heritage Foundation la kutaka rekodi za uhamiaji za Harry ziwekwe wazi lilikataliwa na mahakama kwa hoja kuwa “Umma hauna masilahi makubwa ya kujua kuhusu rekodi hizo.”

Hata hivyo, ushindi wa Trump umeibua matarajio kwamba suala hili linaweza kufikishwa tena mezani, hasa chini ya utawala mpya ambao unaonekana kuwa na msimamo mkali kwenye masuala ya uhamiaji.

Heritage Foundation imeendelea kusisitiza kuwa Serikali ya Marekani inapaswa kufichua rekodi za uhamiaji za Harry ili kuondoa shaka juu ya suala hilo.

Trump amekuwa na msimamo mkali kwa Prince Harry na Meghan tangu mwanzo wa uhusiano wao, akisema hadharani kuwa hatalinda haki ya Harry kubaki Marekani iwapo kuna msingi wa kisheria wa kumkatalia viza.

Trump pia alikosoa tabia ya Harry kujiweka mbali na familia yake ya kifalme na kumlaumu kwa ‘kumvunja moyo’ Malkia Elizabeth II (sasa marehemu).

Akizungumza katika mkutano wa kisiasa Februari 2024, Trump alidai utawala wa Rais Biden ulikuwa ‘neema sana’ kwa Harry tangu 2020 alipohamia California na Meghan.

“Sitamlinda. Alimsaliti Malkia. Hilo halisameheki. Angekuwa peke yake ikiwa ingekuwa chini yangu,” alisema.

Eric Trump, mwanaye Trump pia alitoa maoni yake, akidai sababu pekee ya Harry kuwa na viza ni: “Watu wengi hawajali kuhusu suala hilo.”

Eric alieleza baba yake alimpenda Malkia Elizabeth II na alihuzunishwa na jinsi Harry alivyosababisha mgawanyiko kwenye familia ya kifalme baada ya yeye na Meghan kujiweka pembeni na majukumu ya kifalme.

Katika mahojiano na vyombo vya habari, Trump alitoa kauli kali kwa Meghan akimwita ‘mgawanyiko’ na kudai alimharibu Harry.

Awali, Trump alisema Meghan alikuwa ‘chukizo kwa wanawake’ na kwamba alikuwa na ushawishi hasi kwa Harry.

Trump alisema anahisi Harry alitekwa kihisia na kwamba Meghan huenda atamuacha wakati atakapopata mtu mwingine anayempenda zaidi.

Pamoja na sintofahamu hii, wachambuzi wa kisiasa wanaona Trump anaweza kutumia ushindi wake kama fursa ya kurekebisha sera za uhamiaji kwa msimamo mkali zaidi, hali inayoweza kuleta changamoto kwa Harry na Meghan.

Iwapo utawala mpya utafuata sheria kali kuhusu uhamiaji, Harry anaweza kukabiliwa na vizuizi zaidi vya kisheria katika jitihada zake za kubaki Marekani.

Related Posts