NYOTA wa Tabora United, Offen Chikola aliyemtungua mara mbili Diarra Djigui amevunja ukimya, mabao mawili aliyoifungia timu yake wakati Yanga ikifa 3-1 Novemba 7 katika mchezo wa Ligi Kuu Bara, kwenye Uwanja wa Azam Complex yamempa ufalme mpya akipokea pongezi nyingi tofauti na awali.
Chikola alikuwa mwiba mkali kwa Yanga na alikifanya kikosi hicho cha Kocha Miguel Gamondi kupoteza mchezo wa pili wa Ligi Kuu Bara mfululizo baada ya Novemba 2, kwenye uwanja huo wa Azam Complex kuchapwa bao 1-0 dhidi ya Azam FC.
Akizungumza na Mwanaspoti, Chikola alisema baada ya mchezo huo alipokea ujumbe mwingi kutoka kwa mashabiki mbalimbali wakimpa pongezi kutokana na kiwango bora alichokionyesha, huku akiahidi ataendelea kupambana kwa manufaa ya timu hiyo.
“Nilijisikia faraja sana kuona watu wananifuatilia na kupenda kile ninachokifanya, kwangu imeniongezea motisha zaidi ya kujituma, nichukue nafasi hii kuwashukuru na kuwaomba hata pale nitakapokosea pia wasisite kuniambia ili nijirekebishe.”
Nyota huyo aliyejiunga na Tabora msimu huu baada ya kuachana na Geita Gold, mbali na kufunga mabao mawili huku lingine likifungwa na Mkongomani, Nelson Munganga ila alichaguliwa mchezaji bora wa mchezo.
Kwa sasa nyota huyo amefikisha mabao matatu ya Ligi Kuu Bara na uwezo aliouonyesha umekifanya kikosi hicho cha Tabora kushinda michezo mitatu mfululizo ikiwa ni rekodi pia kwani kabla ya hapo ilikuwa haijawahi kufanya hivyo.
Pia, ushindi huo ni wa pili mfululizo kwa kocha mpya wa timu hiyo Mkongomani Anicet Kiazayidi aliyetambulishwa Novemba 2, mwaka huu akichukua nafasi ya Mkenya, Francis Kimanzi aliyetimuliwa Oktoba 21, kutokana na mwenendo mbaya wa kikosi hicho.
Anicet aliyewahi kuzifundisha timu mbalimbali zikiwemo za AS Vita Club, FC Simba Kolwezi, FC Les Aigles du Congo na Maniema Union, alianza kwa ushindi wa bao 1-0, dhidi ya Mashujaa nyumbani Novemba 4, kisha kuifunga Yanga 3-1, ugenini.