Mbeya. Mkazi wa kijiji cha Mwaya wilayani Kyela Mkoa wa Mbeya, Michael Mwaisaka (42) amehukumiwa kifungo cha miaka 20 jela, baada ya kupatikana na hatia ya shambulio la aibu la kumwingilia kingono mtoto wa miaka minne.
Imeelezwa mahakamani hapo kuwa shambulio hilo lilifanywa kwa mtoto ambaye ni mwanafunzi wa darasa la awali katika shule ya msingi Mwaya iliyopo Wilaya ya Kyela mkoani hapa.
Mwendesha Mashtaka, Mkaguzi Msaidizi wa Jeshi la Polisi, Bihemo Mayangela ameiambia Mahakama kuwa mshtakiwa alitenda kosa hilo Agosti 19, 2024.
Ilielezwa kuwa siku ya tukio, mshtakiwa huyo aliyekuwa amejenga mazoea na bibi wa mwathirika huyo (jina limehifadhiwa), alifika kumchukua na kumpeleka kwenye kichaka na kisha kumvua nguo na kumfanyia vitendo vya kingono.
Mayangela amesema kitendo hicho ni udhalilishaji na kuomba Mahakama kutoa hukumu kwa mshtakiwa kwa mujibu wa kifungu cha 130(i) na (ii)(e) na kifungu cha 131 Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai.
Kufuatia maelezo yaliyotolewa mahakamani hapo, Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Wilaya ya Kyela, Paul Barnabas amemhukumu mshtakiwa kutumikia kifungo cha miaka 20 jela ili iwe fundisho kwa wengine.
Hata hivyo, mshtakiwa alipopewa nafasi ya kujitetea, aliiomba Mahakama impunguzie adhabu, ombi lililokataliwa.
Wakati huohuo, mwanafunzi wa kidato cha nne katika Shule ya Sekondari Ikimba (jina limehifadhiwa) amehukumiwa kifungo cha nje cha miezi 12 na kulipa fidia ya Sh200,000 kwa makosa mawili ya kumbaka na kumpa ujauzito binti wa miaka 17, mwanafunzi kidato cha tatu.
Hukumu hiyo imetolewa Oktoba 24, 2024 na Hakimu Barnabas, baada ya kuridhishwa na ushahidi uliotolewa mahakamani hapo.
Imeelezwa mshtakiwa alitenda kosa hilo Julai 15, 2024 kwa kumlaghai kuwa atamuoa baada ya kuhitimu masomo yake, jambo ambalo sio kweli.
Upande wa Mahakama umeeleza kuwa hukumu na adhabu zimetolewa kwa mujibu wa kanuni na sheria ili iwe fundisho kwa watu wengine.