Na Mwandishi Wetu
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Geophrey Pinda amemkabidhi Anna Kitundu Mwandishi Mwendesha Ofisi ambaye ni mlemavu wa miguu pesa taslimu Shilingi Millioni moja kwa ajili ya kununua baiskeli na itakayomsaidia kuongeza ufanisi wake kazini ikiwemo kufika kituo cha kazi kwa wakati.
Mhe. Pinda amekabidhi Pesa hizo muda baada ya kikao cha na watumishi wa Ardhi katika ofisi ya Kamishna Msaidizi wa Ardhi Mkoa wa Singida mapema wiki hii.
Kwa Upande wake Kamshina Msaidizi wa Ardhi Mkoa wa Singida Bi. Shamim Hoza amemshukuru Naibu Waziri Mhe. Pinda kwa upendo wake kwa watumishi wa Ardhi na Watanzania akimuombea heri katika kuwatumikia wananchi wa Tanzania.
“Tunakushukuru sana Mheshiwa Naibu Waziri kwa kuguswa na hili kwani ni alama bora ya upendo ya kudumu na mfano wa kuigwa katika jamii” amesema Bi Shamim.
Naye Anna Kitundu amemshukuru Naibu Waziri Mhe. Pinda kwa Kumpatia fedha ya kununua baiskeli kwani itamsaidia kufika kazini kwa urahisi zaidi na kumuepusha na changamoto za barabarani.
“Napenda kukushukuru Naibu Waziri Mhe. Geophrey Pinda kwa kuninunulia baiskeli ya kunisaidia kutoka nyumbani mpaka eneo la kazi kwani amenipunguzia changamoto nilizokuwa nakumbana nazo barabarani ikiwemo bajaji kukataa kunibeba wakiamini mimi sina nauli ya kulipa” amesema Anna.
Anna Kitundu ni mtumishi Ofisi ya Ardhi Mkoa wa Singida, hufika kazini kwake kila siku kwa kutumia usafiri wa umma maarufu kama bajaji hapa nchini, hivyo fedha hizo atazotumia kununua baiskeli ambayo itaongeza ufanisi wake kazini.