Serikali kuweka sheria maalumu kwa wataalamu wa usafirishaji

Dar es Salaam. Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa amesema wizara hiyo, inaendelea na mchakato wa kuweka sheria  mahususi ya usimamizi wa watalaamu wa usafirishaji nchini.

Amesema lengo ni kuhakikisha sekta ya uchukuzi inaongozwa kitaalamu kwa kutumia sheria, kanuni, taratibu na weledi wa kitaalamu na sio kusimamiwa na kuendeshwa kiholela.

Taarifa iliyotolewa leo Jumamosi Novemba 9, 2024 kwa vyombo imeeleza kuwa, Profesa Mbarawa ameyasema hayo katika mkutano wa Chama cha Watalaamu wa Lojistiki na Usafirishaji (TALTA)

Waziri Mbarawa amesema Taifa linatakiwa kuweka msingi ya namna bora ya kusimamia wataalamu wa sekta hiyo ili nchini na inufaike kwa kuwa na huduma stahiki za lojistiki na usafirishaji zinazowezesha sekta zingine kufikia malengo.

“Ili tufikie huko Taifa linatakiwa kuhakikisha wataalamu wa lojistiki na usafirishaji wanadhibitiwa kama ilivyo kwa sekta nyingine za kitaalamu nchini, kupitia bodi itakayoanzishwa kisheria ya kusimamia wataalamu wa sekta hii.

 “Napenda kuwafahamisha wizara inaendelea na hatua za kuwezesha kutungwa kwa sheria mahsusi ya Usimamizi wa Wataalamu wa Usafirishaji Tanzania,” amesema Profesa Mbarawa.

Kwa mujibu wa Mbarawa, kupitia sheria hiyo kutaanzishwa bodi ya usimamizi wa Wataalamu wa Usafirishaji itakayokuwa na jukumu kubwa la kudhibiti maadili na utendaji kazi wa wataalamu husika.

Rais wa Chama TALTA, Alphonce Mingira amesema  taasisi hiyo ina lengo la kusaidia watalaamu na wafanyabiashara wa usafiri na usafirishaji katika maendeleo ili  kuona  fursa zilizopo na  kuweka mazingira mazuri ya utendaji kazi kati ya sekta binafsi na Serikali.

Mkurugenzi wa Idara ya Udhibiti Kiuchumi wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA), Daniel Malanga amesema taasisi hiyo inaendelea kutoa elimu kuhusu usafiri na usafirishaji kwa manufaa  ya  Watanzania wote.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, mkutano huo umehudhuriwa na taasisi zilizopo chini ya sekta ya uchukuzi ambapo washiriki kutoka wizara ya ujenzi, Tamisemi na vyuo vya elimu ya juu.

Related Posts