Mwandishi wetu
CHUO Kikuu cha Umoja wa Afrika Tanzania (UAUT) kimesema kimejipanga kuzalisha wanafunzi waliopikwa vizuri ili waweze kuhitimu wakiwa wamebobea katika nyaja mbalimbali.
Hayo yamebainishwa Jijini Dar es salaam mapema leo Novemba 9,2024 na Mwenyekiti wa Baraza la UAUT ,Profesa Rwekaza Mukandala katika mahafali ya tisa ya Chuo hicho tangu uongozi mpya chini ya umiliki mpya .
Amesema wanafunzi watakaohitimu katika Chuo hicho watakuwa na uwezo wa kukabiliana na chagamoto mbalimbali zilizopo katika jamii.
“Sisi haja yetu ni kuwa na wanafunzi wachache watakaopikwa vizuri na kufundishwa ili waweze kuhitimu wakiwa wamebobea katika nyaja mbalimbali”amesema Profesa Mukandala
Profesa Mukandala amesema kuwa kwa sasa Chuo kinatoa masomo ya biashara na komputa huku kikiwa kimejiimarisha kwa kuwa miundombinu, walimu wenye viwango ili kutoa wanataaluma waliobobea kwa ajili ya kutumikia umma wa watanzania.
Ameongeza kuwa watakuwa wakifanya hivyo kwa uhagalifu na mkakati kwa kutegemeana na nyezo na vifaa vilivyopo.
“Ukubwa wa Chuo kwa maana ya kuwa na wanafunzi wengi na taaluma nyingi inategemea na miundombinu ya Chuo kama inatosheleza”amesema
Kwa upande wake Mkuu wa Chuo UAUT, Dkt Kyung Chul Kam amesema baada ya uongozi mpya kuingia kwa sasa UAUT kimejikita zaidi katika kuangalia zaidi jamii.
“Tunamshukuru Serikali ya Tanzania kwa ushirikiano mkubwa na kuamua kuwekeza katika Chuo cha UAUT”amesema
Naye mmoja wa wahitimu katika Chuo hicho Elinami Bwiru amesema Chuo hicho kimekuwa kikitoa elimu itakayomuwezesha muhitimu kuiona dunia ya tofauti huku kikisiamia zaidi misingi ya maadili ya kikiristo.