BILIONEA wa klabu ya Simba, Mohammed ‘Mo’ Dewji atalazimika kuvunja benki ili kuinasa saini ya kiungo mshambuliaji Abdelhay Forsy aliyependekezwa na kocha Fadlu Davids, kutokana na ukweli ndiyo kwanza mchezaji huyo ameanza kuutumikia mkataba wa miaka miwili alioingia na klabu ya Renaissance Club Athletic Zemamra ya Morocco.
Kiungo huyo aliyewahi kufanya kazi na Fadlu wakati wote wakiwa Raja Casablanca inadaiwa anahitajiwa na Simba kwa nia na kuongeza nguvu eneo la mbele na kumpa mtu sahihi nyota wa sasa wa klabu hiyo, Jean Ahoua katika eneo hilo na mazungumzo yanaendelea vizuri ikisubiriwa mambo yatiki atue dirisha dogo.
Hata hivyo, ili Simba imnase kiungo huyo anayesifiwa kwa chenga za maudhi, pasi, penalti na kufunga mbali na uwezo wa kutumika pia kama winga akitumia miguu yote miwili, ni lazima MO Dewji avunje au kuununua mkataba wa mchezaji huyo aliyetua RCA Zemamra, Julai mwaka huu kutoka Raja Casablanca.
Raja ni klabu aliyokuwa akiitumia Fadlu kama kocha msaidia na msimu uliopita walibeba ubingwa wa Morocco kabla ya Simba kumnyakua kuchukua nafasi ya Mualgeria, Abdelhak Benchikha aliyerudi kwao Algeria na sasa akiinoa JS Kabyile. Mara baada ya kudokezwa juu ya dili hilo linalotokana na pendekezo la kocha Fadlu, Mwanaspoti liliamua kuchimba juu ya kiungo huyo na kubaini hana muda mrefu tangu atue RCA Zemamra aliyowahi kuitumikia kwa mkopo mara kadhaa akitokea Raja kabla ya Julai kumbeba jumla.
Thamani ya mchezaji huyo kwa sasa kwenye mtandao wa Transfermarkt ni Euro 275,000 zaidi ya Sh 790 milioni, hapo ni bila kutajwa thamani aliyosainishwa wakati anajiunga na timu hiyo inayoshiriki Ligi Kuu ya Morocco.
Kutokana na kiwango cha thamani cha mchezaji huyo, mwenye umri wa miaka 26 na aliyewahi kukipiga pia KAMC Marrakech iliyopo mji aliozaliwa, CA Khenifra na Raja inaweza kuwa ni mtihani kwa MO Dewji kuvunja benki ili kuinasa saini ya kiungo huyo ambaye Fadlu anamtaka leo kesho atue Msimbazi.
Mbali na Raja, Forsy amewahi pia kuzichezea kwa vipindi tofauti OC Safi na RCA Zamamra aliyoitumikia mara mbili kabla ya kuuzwa jumla Julai mwaka huu, huku ikielezwa kwa MO Dewji kuvunja benki sio ishu sana kwani hata katika sajili zilizopita za nyota waliotumia Simba ikiwamo za msimu huu ameshafanya hivyo.
Inaelezwa kama Mo atafanikiwa kumvuta kiungo huyo ili aungane na Ahoua aliyegeuka lulu ndani ya Msimbazi kwa sasa kwa kuhusika na mabao tisa katika mechi 10 za Simba katika ligi ikiwamo kufunga matano na kuasisti mawili, basi kuna mashine mbili sasa kikosini zitapewa mkono wa kwaheri.
Mmoja ya wanaotajwa huenda akaondoka kwa kuuzwa ni kipa Ayoub Lakred na beki wa kati Chamou Karaboue ambaye hadi sasa hajaonyeha maajabu, kitu kilichomlazimu Fadlu kufikiria kuleta beki mwingine wa kati wa kusimama imara na Fondoh Che Malone na Abdulrazak Hamza mbali na Hussein Kazi.
“Ishu kwa sasa kwa Simba inayozungumza na menejimenti ya mchezaji huyo ni namna ya kuununua au kuvunja mkataba alionao kwa sasa Renaissane,” kilisema chanzo kutoka Simba.
Chanzo hicho pia kimesema wanasimba wana hamu kubwa ya kuona kiungo huyo akitua Msimbazi dirisha dogo kutokana na ukweli hadi sasa bado timu hiyo inayoongoza msimamo wa ligi na idadi kubwa ya mabao ikifunga 21, haina mlishaji mipira kwa washambuliaji Leonel Ateba na Steven Mukwala, tofauti na Simba ya kina Luis Miquissone, Clatous Chama na Saido Ntibazonkiza.
Hata hivyo, inadaiwa kama Renaissane itakomaa, itaulazimu uongozi wa Simba kusaka huduma ya kiungo mwingine anayetajwa pia anapatikana Morocco japo hadi sasa jina lake imekuwa siri kwa vile akili zipo kwa Forsy.
Dirisha dogo la misimu miwili mfululizo iliyopita, Simba pia ilisajili viungo, ila hawa walikuwa wakabaji Msenegal, Babacar Sarr kutoka US Monastir ya Tunisia na Ismael Sawadogo aliyekuwa Difaa El Jadida ya Morocco ambao hata hivyo walichemsha na kutemwa.
Pia ilitumia dirisha dogo kumrejesha Clatous Chama kutoka RS Berkane ya Morocco baada ya kukosa mtu wa kuziba pengo lake baada ya kumuuza 2021 na alichukua muda kukaa sawa na kuibeba Simba kabla ya msimu huu kuhamia Yanga baada ya kumaliza mkataba aliokuwa nao.
Rekodi tamu ya Simba kusajili mchezaji katika dirisha dogo na kuwabeba ilikuwa ni kwa Jean Baleke misimu miwili iliyopita ilipomnyakua kwa mkopo kutoka TP Mazembe ya DR Congo ambaye aliwasha moto kabla ya kumtema dirisia dogo kumrudisha Mazembe iliyompeleka Sl Ittihad ya Libya na dirisha kubwa la msimu huu akarejea tena nchini na kujiunga na Yanga.