TS Galaxy ya Afrika Kusini ambayo Julai mwaka huu ilicheza mechi maalumu ya kirafiki na Yanga kufungwa 1-0 inadaiwa ipo katika mazungumzo ya kumng’oa kocha wa KMC, Abdihamid Moallin ili akaifundishe timu hiyo.
Taarifa kutoka ndani ya uongozi wa KMC zimeliambia Mwanaspoti, Moallin ni miongoni mwa makocha wanaotajwa kujiunga nao huku meneja wake akiwa katika mazungumzo hayo na viongozi wa TS Galaxy, ambao wameonyesha nia ya kuihitaji saini yake.
“Ni kweli ni miongoni mwa makocha wanaohitajika kuifundisha timu hiyo na mazungumzo yameshaanza japo bado hayajafikia muafaka, kama kila kitu kitaenda sawa Moallin atajiunga na TS Galaxy ingawa ana mkataba na KMC,” kilisema chanzo hicho.
Akizungumzia hilo, Moallin alisema kwa sasa malengo yake ni kutengeneza kikosi cha KMC kiweze kuleta ushindani msimu huu na kama kuna mengine yatatokea ataweka wazi juu ya hatima yake, japo mashabiki wake watambue bado yupo na anawapenda.
Kwa upande wa Ofisa Mtendaji Mkuu wa KMC, Daniel Mwakasungula alisema taarifa za kocha wao kuhitajika hazina ukweli bali ni tetesi tu zinazozushwa mitandaoni, huku akiweka wazi viongozi wote bado wana imani na malengo naye ya muda mrefu.
“Hizo taarifa sisi kama viongozi hazijatufikia hivyo naweza kusema ni tetesi tu, Moallin ni kocha mzuri na tunamtegemea msimu huu na tayari ametoa mapendekezo yake kuelekea dirisha dogo na tumeshaanza kuyafanyia kazi kwa haraka,” alisema.
Hatua ya Moallin kuhitajika na timu hiyo inajiri baada ya aliyekuwa kocha mkuu wa kikosi hicho Mjerumani, Sead Ramovic kujiuzulu kutokana na matokeo mabaya, huku kwa sasa kocha msaidizi, Adnan Beganovic akipewa jukumu hilo la kukisimamia.
Ramovic amejiuzulu mwenyewe baada ya kuiongoza timu hiyo katika michezo sita ya Ligi ya Afrika Kusini bila ya ushindi ambapo kati yake ametoka sare miwili na kupoteza minne, akiiacha mkiani mwa msimamo ikiwa na pointi mbili tu.