Swali: Anti habari, pole na majukumu. Mke wangu nimemuoa huu mwaka wa saba, kwa bahati mbaya hatujabahatika kupata mtoto, mwenzangu ana mtoto aliyezaa kabla ya uhusiano wetu.
Changamoto ndiyo imeanzia hapo, ananilaumu kwa kila kitu, sifanyi jambo jema bila kunishinikiza nimpe mimba. Kwa kifupi kukesha nikidaiwa mimba ni jambo la kawaida maishani mwangu kwa sasa, ninarudi nyumbani nikapumzike baada ya kazi za kutwa nzima, lakini sina uhakika wa kulala, ni makelele mpaka nakosa amani.
Nishauri nifanyeje kwa sababu hata sijui nianzie wapi.
Jibu: Duh! Pole sana. Mkeo atakuwa amepata tatizo la kisaikolojia linalotokana na tamaduni za Kitanzania kama siyo za Kiafrika kuamini mwanamke akiolewa ili ndoa ikamilike azae.
Katika jamii nyingi, suala la uzazi na mimba ni jambo nyeti lenye uzito wa kihisia. Kibaya zaidi inawezekana kutokana na kuihitaji sana mimba kunamfanya aikose kabisa, kwani anajipa msongo wa mawazo ambao unaweza kuvuruga homoni zake.
Kwenye jamii nyingi watoto wanatafsiriwa kama baraka na kuna mashinikizo kutoka kwa wanafamilia, jambo linalomkosesha raha mkeo. Pengine anavyokulalamikia ni mbinu ya kujiepusha na lawama ya kutozaa kwa sababu tayari ana mtoto.
Kwa jumla kwenye familia mahusiano huwa magumu pale ambapo kuna tofauti ya mawazo kuhusu uzazi.
Mwanzoni kabisa ulipaswa kuchukua hatua ya kufanya naye mazungumzo ya kukuza uelewa wake kuhusu suala hilo, lakini kwa sasa sidhani kama atakusikiliza. Hivyo watumie watu wake wa karibu kumshawishi aonane na mtaalamu wa saikolojia atakayemjengea uelewa kwanza kabla ya kuchukua hatua nyingine. Kwa sasa ni ngumu kuelewa chochote, yeye anaamini amezaa na hawezi kushindwa kufanya hivyo kwa mara nyingine. Ingawa kitaalamu anaweza kupata changamoto hiyo hata baada ya kuzaa mtoto mmoja, wawili au vinginevyo.
Akishaonana na mtaalamu wa saikolojia atakayemjenga kuhusu uelewa wa kukosa mtoto, siyo kesi ya mmoja kwa wenza, ndiyo uende naye hospitali kwa ajili ya vipimo, kwani kwa sasa itakuwa ngumu hata kupokea majibu endapo ataambiwa yeye ndiyo ana tatizo. Iwapo tatizo ni lako pia atapokea majibu, kwani atakuwa ameshapata utulivu wa akili.
Majibu ya daktari mbobezi kwenye masuala ya uzazi ndiyo yatawapa mwelekeo wa muanzie wapi kupata mtoto.
Iwapo itashindikana kuna njia nyingi siku hizi za kufanya ili kupata watoto, ikiwamo kupandikiza na kuasili. Naamini akiwa na utulivu ni rahisi kufanikiwa, kwani daktari atawashauri namna ya kufanya.
Swali: Nimfungulie biashara gani mke wangu?
Mke wangu hataki kazi ya kuajiriwa, hivyo ninataka nimfungulie biashara. Changamoto sina uzoefu au sijui nimfungulie biashara gani. Naomba ushauri kwa uzoefu wako ni biashara gani itamfaa. Kwa msaada zaidi wa ushauri ninaishi Dar es Salaam na mke wangu hachagui biashara, kwani kwao wapo wafanyabiashara ingawa yeye hakujikita huko muda mwingi alikuwa anasoma.
Jibu: Kumfungulia mke wako biashara ni hatua nzuri na inaweza kusaidia kuongeza kipato cha familia na kumwezesha kuwa na uhuru wa kifedha. Katika mji wa Dar es Salaam, kuna fursa nyingi za kibiashara.
Ila ungemshirikisha mwenyewe pengine angekuwa na wazo zuri zaidi kulingana na anachokitaka. Hata hivyo, kwa kuwa umetaka ushauri nitajitahidi. Anaweza kuanza na duka la vyombo na vifaa vya nyumbani, kwa sababu ni mahitaji ya watu ya kila siku na kwenye jiji kama Dar es Salaam kama nilivyosema awali fursa ya kuuza ni kubwa, kwani watu ni wengi.
Pia unaweza kumfungulia saluni, ukubwa, ubora wa huduma na vifaa inategemea na mtaji ulionao. Ila ungejitahidi kumfungulia inayotofautiana na zilizopo eneo husika ili kuvutia wateja wengi zaidi.
Muhimu azingatie ubora wa huduma. Hii biashara uzuri wake ni kipenzi cha wanawake, kwa kifupi biashara inayohusisha urembo ina wateja wengi.
Biashara nyingine ni duka la kuoka mikate ambalo pia atalitumia kukoka keki. Siku hizi matumizi ya keki yanazidi kuongezeka, hivyo akichanganya bidhaa hizo mbili na akaoka kwa ustadi, biashara hii nayo ni nzuri, kwani inahusisha matumizi ya watu ya kila siku. Ila uangalie eneo zuri kwa ajili ya biashara hiyo, likiwa na mzunguko wa watu itapendeza zaidi.
Biashara ya chakula kama mgahawa au duka la vyakula vitupu kwa jumla na rejareja. Hili akilifungua karibu na makazi ya watu itakuwa nzuri zaidi.
Muhimu kabla ya kumfungulia biashara, hakikisha unamshirikisha mke wako katika maamuzi ili ajisikie mwenyewe kwenye biashara hiyo. Pia, fanya tafiti za soko ili kujua mahitaji katika eneo unalofikiri kuanzisha biashara. Hii itaiwezesha biashara unayomfungulia kuwa na nafasi nzuri ya kufanikiwa.