Mbolea ya ruzuku iwafikie wakulima wa Katani

Baraza la Madiwani kimefanyika leo tarehe katika ukumbi wa Halmashauri ya Kilolo chini ya mwenyekiti wa halmashauri Mhe. Anna Msola, kwa lengo la kujadili taarifa za utekelezaji za robo ya kwanza (Julai – Septemba) kwa mwaka wa fedha 2024/2025.Akiwasilisha taarifa ya kamati ya Uchumi,Ujenzi na Mazingira, Mwenyekiti wa kamati hiyo Mhe.

 

Rahman Mkakatu, iliibuliwa hoja ya mbolea ya ruzuku kwa wakulima na Mhe. Bruno Kauku kuhusiana na upungufu wa mbolea katika kata yake.“ Mhe. Mwenyekiti wakazi wa kata ya Idete wanalazimika kufuata mbolea ya ruzuku Bomalang’ombe kutokana na wafanyabiashara/mawakala kushindwa kupeleka Idete kutokana na gharama kua juu za usafirishaji, je Serikali ina mpango gani wa kulitatua hilo?” aliuliza Mhe. Kauku.

 

Aidha Mhe.Bruno Kauku ameiomba Serikali kufanya jitihada za kuwahisha kupeleka mbolea kwa wakulima wa kata hiyo kwani wao wanawahi kuanza msimu mpya wa kilimo ukitofautisha na maeneo mengine, hivyo kukosa mbolea hiyo kwa wakati itarudisha nyuma Zaidi.

 

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Halmashauri ya Kilolo Mhe. Anna Msolla amemuagiza Afisa kilimo wa wilaya hiyo kuhakikisha anafuatilia kwa ukaribu ili wakulima wote wenye uhitaji wa mbolea waweze kujiorodhesha ili uhitaji ujulikane na kisha wapelekewe kwa wakati ili kufanikisha kufanikisha uzalishaji wa mazao kwa tija zaidi.

 

Wakati huohuo baadhi ya waheshimiwa madiwani kutoka kata mbalimbali wameunga hoja hiyo kwa kueleza kwamba tatizo la kutopatikana kwa mbolea katika baadhi ya maeneo huwakatisha tamaa wakulima na kushindwa kuendelea kulima kutokana na kushindwa kugharamia gharama za kuzifuata mbolea hizo maeneo ya mjini na kwingineko, hivyo wanapendekeza serikali ione ni jinsi gani mbolea za ruzuku zitawafikia wakulima katika kila kata kwa bei elekezi ya serikali.

 

Kwa upande wake Afisa kilimo mifugo na uvuvi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilolo, Dkt. John Mwingira ameeleza kwamba amelipokea ombi hilo kutoka kwa wakulima kupitia kwa madiwani hivyo kinachotakiwa ni wakulima kujiorodhesha kwa majina kwa wale wanaohitaji mbolea hizo ili serikali iweze kuona ni kwa utaratibu upi mbolea hiyo itawafikia wakulima.

Related Posts