Fedha ni njia tunayotumia kupima thamani ya bidhaa na huduma tunazonunua au kuuza. Kwa kawaida, kila nchi inatumia sarafu yake kama kipimo cha thamani. Kwa mfano, Tanzania inatumia shilingi, wakati nchi nyingine kama Marekani hutumia dola.
Lakini, kuna wakati fedha za kigeni zinahusishwa katika biashara, hasa kwa sababu ya biashara za kimataifa. Hata hivyo, hivi karibuni, Benki Kuu ya Tanzania imepiga marufuku matumizi ya fedha za kigeni, kama dola, kwa upangaji wa bei na malipo ndani ya nchi.
Hatua hii inalenga kulinda na kuimarisha thamani ya Shilingi. Unapopanga bei ya bidhaa kwa kutumia fedha za kigeni, kama dola, kuna hatari kwamba thamani ya Shilingi itashuka. Hii ni kwa sababu watu wengi watahitaji kubadilisha Shilingi kuwa dola, na hivyo kufanya Shilingi ipoteze thamani yake sokoni. Matokeo yake, gharama za maisha zinaweza kupanda kwa sababu bidhaa nyingi zinapangwa kwa bei ya juu, kulingana na mabadiliko ya fedha za kigeni.
Kwa kuwa marufuku hii inalenga kulinda Shilingi, inaweza kuwa na faida kwa wananchi wa kawaida, kama vile wakulima na wafanyakazi. Kwa mfano, ikiwa unalipwa kwa Shilingi lakini bidhaa zinapangwa kwa dola, utalazimika kutumia pesa zaidi kulingana na kiwango cha ubadilishaji wa fedha. Lakini, kama bei zitapangwa kwa Shilingi, inakuwa rahisi kwako kupanga bajeti na kutumia kipato chako kwa ufanisi. Pia, hii inasaidia kuhakikisha kwamba wafanyabiashara hawapandishi bei kiholela kwa kuzingatia fedha za kigeni, jambo ambalo linaweza kupunguza shinikizo la bei kwenye bidhaa na huduma.
Hatua hii pia inalenga kuzuia mianya ya ukwepaji wa kodi na utoroshwaji wa fedha za kigeni. Wakati malipo yanafanyika kwa fedha za kigeni, kuna uwezekano kwamba baadhi ya shughuli za kiuchumi hazitaonekana kwenye mfumo rasmi wa uchumi. Hii inamaanisha kwamba Serikali inakosa mapato ya kodi ambayo ingetumika kugharamia huduma za jamii kama elimu, afya na miundombinu.
Hivyo kuhakikisha kwamba malipo yanafanywa kwa Shilingi ya Tanzania kunarahisisha ufuatiliaji wa kodi na kuimarisha mapato ya Serikali. Pia kutakuwa na uthibiti wa utoroshwaji wa fedha za kigeni ambao unaweza kufanyika kiholela na hivyo kutoa mwanya kwa benki kuu kuwa chombo pekee kama chanzo cha fedha za kigeni kwa ajili ya kulipia bidhaa zinatotoka nje ya nchi.
Nchi nyingi duniani zimechukua hatua kama hii kwa kutoruhusu fedha za kigeni kutumika katika malipo ya ndani. Hii inasaidia kudumisha thamani ya sarafu zao na kulinda uchumi wa ndani. Kwa Tanzania, hatua hii inaweza kuchangia sana katika kuboresha uchumi, kwa sababu sarafu thabiti inatoa uhakika kwa wawekezaji na wafanyabiashara wa ndani. Iwapo shughuli nyingi za kiuchumi zitatumia shilingi, hii itasaidia pia kujenga heshima na utambulisho wa shilingi ya Tanzania kimataifa.
Kwa kumalizia, marufuku ya matumizi ya fedha za kigeni katika malipo ya ndani inalenga kuimarisha uchumi wa Tanzania. Hii inalinda thamani ya shilingi, inasaidia kupunguza gharama za maisha, na inaweka mazingira bora kwa biashara na wawekezaji wa ndani na wa kimataifa. Hivyo, hatua hii ni muhimu kwa maendeleo ya muda mrefu ya uchumi wa taifa.