KOCHA wa JKT Queens, Esta Chabruma amesema amekoshwa na viwango vinavyoonyeshwa na wachezaji wachanga akimtaja Christer Basil.
Ikumbukwe JKT yenye viongozi wazawa na inaongozwa na benchi la ufundi wazawa na imesajili wachezaji wote wazawa.
Utaratibu wa JKT wanasajili mabinti wadogo ambao asilimia kubwa wanawatoa kwenye mashindano ya ligi za mkoa na kisha kuwatengeneza na wakipata uzoefu wanapandishwa timu kubwa.
Akizungumza na Mwanaspoti, Chabruma alisema anafurahishwa na viwango vya nyota hao ambao bado hawana uzoefu na ligi akiwatabiria makubwa baadae.
Aliongeza kiungo kama Christer Bazil ambaye amekuwa akitumika kwenye mechi mbalimbali msimu huu, anazidi kupata uzoefu tofauti na hapo awali.
“Tunaendelea kupambana kuhakikisha tunapata ushindi kwenye kila mechi ingawa haitakuwa rahisi, mkoani tulipata tabu kidogo tukiacha pointi mbili,” alisema Chabruma na kuongeza;
“JKT haisajili wachezaji wa nje na kumekuwa na utaratibu wa kuwachukua vijana wadogo na tukiona wameanza kuiva, tunawapa mechi ili kuwapa uzoefu, kuwatoa hofu na kuwajengea kujiamini na tunashukuru tumefanikiwa kwenye timu.”