RAFIKI zetu wa Mwanza Pamba wamerudi Ligi Kuu. Imepita miaka 22 tangu walipoondoka zao. Umri wa mtu mzima. Nyakati zimekwenda wapi? Hatujui. Walikuwa na shangwe kwelikweli katika mitaa yao. Namna walivyopokewa ungeweza kudhani wametoka kutwaa Kombe la Dunia.
Unaikumbuka Pamba halisi? Wakati huo wakiwa na kina Fumo Felician, Khalfan Ngassa baba yake Mrisho Ngassa, Kitwana Suleiman, Beya Simba, Hussein Marsha na wengineo wa kizazi kile. Kabla ya hapo walikuwa na kizazi kingine cha kina Joram Mwakatika ‘Mzee wa Upara’. Walisumbua sana.
Walisumbua wakubwa. Walikuwa wana timu hasa. Katika moja kati ya tukio la kusisimua ni kipa wa Yanga, Steven Nemes alipovua glovu zake mbele ya mwamuzi, Nassor Hamduni kutoka Kigoma akichelewesha muda katika dakika kumi tu za mwanzo za mchezo wa Uwanja wa Taifa.
Ndani ya dakika hizo tayari Pamba walikuwa wamegongesha nguzo zake mara nne. Names akaona isiwe shida. Bila ya kuumia akavua glovu zake na kusingizia ameumia. Mashuti ya kina Fumo yalikuwa yamezidi kipimo chake licha ya kusifika kwa ushujaa mkubwa alipokuwa langoni. Wale ndio walikuwa Pamba tuliowafahamu.
Wangekuja Uwanja wa Taifa kucheza na Simba au Yanga usingeweza kutabiri matokeo yao mapema. Walikuwa hawatabiriki. Walisifika sana kwa kuuweka mpira chini kiasi cha kuitwa TP Lindanda. Wao na rafiki zao Ushirika Moshi wangecheza katika dunia ya leo wangekuwa kama Manchester City ya Pep Guardiola.
Wamerudi tena lakini nawakumbusha rafiki zangu kwamba maisha yamebadilika sana. Maisha ya siku zile na siku hizi ni tofauti. Kuna mambo mengi yamebadilika hapo katikati. Swali la kwanza la kujiuliza ni namna gani waliweza kupata wachezaji wazawa wa kiwango kile? Vizazi na vizazi walikuwa na timu bora kiasi cha kutwaa ubingwa wa Muungano.
Mpaka leo wanashikilia rekodi ya kuifunga timu ya kigeni mabao mengi zaidi. Waliifunga Ansa Belou ya Shelisheli mabao 12-1 pale CCM Kirumba, Mwanza. Pamba waliwapataje wachezaji wa dizaini ile? Leo maisha yamebadilika na sidhani hata kama wachezaji waliowapandisha daraja wanaweza kufikia nusu ya wale.
Walikuwa wazawa watu na baadaye wakageuzwa kuwa shamba la Simba na Yanga kuvuna wachezaji. Nakumbuka akina Azim Dewji na Abbas Gulamali walivamia pale na kuwachukua akina George Masatu, Marsha, David Mwakalebela, Rajab Msoma, Nico Bambaga na wengineo wengi.
Pamba ya leo ifahamu kwamba hata wakubwa wenyewe wameacha kutegemea wachezaji wazawa na badala yake wanategemea wachezaji wa kigeni. Pamba imekuja na pesa hizo? Mida hii wanatarajiwa kupishana na timu kama Mtibwa Sugar ambayo inazama ikiwa na wachezaji wazawa. Hawana wachezaji wa kigeni. Pamba imekuja na pesa hiyo?
Mpira wa leo umetawaliwa na pesa. Wakati ule vipaji vilikuwa vingi na vilitawala kila kukicha na ndio maana ilikuwa rahisi kwa Pamba kupambana na Simba na Yanga. Leo maisha yamekuwa magumu na hawa wakubwa wenzao kila mmoja ana wachezaji 12 wa kigeni ambao kwa kiasi kikubwa wamezipeleka juu timu hizi.
Na wakati Pamba haipo ghafla hapo njiani wakazaliwa Azam FC ambao nao wana uwekezaji mkubwa. Pamba wasirudi na kutegemea maisha waliyoishi zamani wanaweza kuishi sasa. Sio kweli. Tunajua kwamba ni vema timu za kitamaduni zikarudi. Tunataka hata Tukuyu Stars warudi lakini warudi kivingine.
Kuna wakongwe wengine Coastal Union. Wapo katika hii Ligi lakini kuna wakati wanachechemea. Zipo nyakati ambazo walishuka hata daraja. Ukongwe hausadii tena. Mpira umetawaliwa na pesa za ajabu. Wachezaji wa kisasa nao wanajitambua. Wanataka pesa nyingi za usajili pamoja na mishahara. Sidhani kama akina Fumo walikuwa na mahitaji hayo.
Halafu kuna mabadiliko ya vizazi. Haya nayo yanasumbua. Mashabiki wa zamani wa Pamba nao wametoweka. Wengine wamehama Mwanza, wengine wamefariki. Kimekuja kizazi kipya cha mtandao ambacho kinaweza kuujaza uwanja wa CCM Kirumba lakini kwa ajili ya kumshangilia Aziz Ki na sio timu yao. Wanakuja kumshangilia Clatous Chama na sio timu yao.
Zamani kulikuwa na uzalendo wa mikoani lakini kwa sasa umetoweka. Watu wa mikoani wamejikita zaidi katika kushangilia Simba na Yanga kuliko timu zao. Na hii ni kuliko ilivyokuwa zamani. Zamani watu wa Mwanza walikuwa wanaipenda zaidi Pamba yao.
Pamba ya sasa hivi itakutana na Usimba na Uyanga ndani ya uongozi wao. Waulize watu we timu nyingine za mikoani watakwambia hili. Majuzi sijui Prince Dube alikuwa anasema kweli wakati alipotuambia kwamba hata Azam kuna Usimba na Uyanga ndani ya timu yao. Kama kweli hilo lipo bado hatuwezi kushangaa sana.
Pamba wamerudi na pesa? Fikiria namna watakavyokabiliwa na safari ndefu ndefu kutoka kwao Mwanza kwenda Mbeya na kwingineko. Walau Kagera Sugar, Geita Gold na Ken Gold wanaweza kuwapunguzia safari lakini vinginevyo wapo mbali kweli kweli na dunia nyingine. Kama wamerudi na pesa basi sio mbaya mara moja moja wawe wanapanda ndege kuja mjini.
Kuna pesa zipo katika mpira kutoka Azam TV na NBC. Lakini wanahitaji kuwa na wadhamini zaidi ili wasirudi walikotoka. Wanahitaji pia kuwa na tajiri ili wawe na uhai kama ndugu zetu Ihefu. Sio mbaya wakiwekeza pia kwa vipaji maridhawa vya nje kwa sababu siamini kama tunaweza kupata vipaji kama vya akina Fumo kwa urahisi sana.
Tuwakaribishe tena katika Ligi kuu. Ufalme wa akina Hamis Gaga na Athuman China ulitoweka lakini sasa kuna ufalme wa akina Aziz Ki. Wanapiga mashuti kama wamewehuka. Ni bora wakajiadhari nao mapema. Vinginevyo wanaweza kurudi walikotoka. Wasije mjini kichwa kichwa kama baadhi ya rafiki zetu walivyofanya.