LICHA ya ushindi wa mabao 4-1 iliyopata Simba Queens kwenye mchezo wa Ligi Kuu, kocha wa timu hiyo, Yussif Basigi amesema walikuwa na nafasi ya kufunga mengi zaidi, lakini tatizo ni uwanja.
Tangu ametua nchini akitokea Hasaacas Ladies ya Ghana, Basigi msimu huu hajapoteza mchezo wowote wa ligi akiongoza kwenye msimamo wa ligi na pointi tisa.
Basigi alisema licha ya kuondoka na pointi na mabao hayo, lakini Uwanja wa Samora uliwapa shida kupiga pasi sahihi na haikuwa rahisi kupata ushindi kwenye mechi ya ugenini kutokana na Ceasiaa kuwa bora licha ya kutanguliwa mabao mawili kipindi cha kwanza.
“Nawapongeza wachezaji wangu kwa kupambania pointi tatu nyingine, lakini uwanja leo ulikuwa mgumu na tunashukuru tumepambana na kuendelea kusalia kileleni,” alisema Basigi.
Aliongeza kwa sasa akili yao ipo kwenye mchezo ujao wa dabi dhidi ya watani zao Yanga Princess ambao hautakuwa rahisi.
“Tunaendelea na maandalizi ya mchezo na Yanga, kwetu hautakuwa rahisi kutokana ni dabi na tunahitaji ushindi ili kujiweka vizuri kutetea ubingwa wetu.”
Kocha huyo amekutana na Yanga Princess kwenye mechi ya nusu fainali ya Ngao ya Jamii na kutolewa kwa mikwaju ya penati 4-3 baada ya sare ya 1-1.