Biashara Utd mambo magumu | Mwanaspoti

UONGOZI wa Biashara United umekiri kukumbwa na ukata wa kifedha wa kuiendesha timu hiyo msimu huu huku viongozi, wadau na wadhamini mbalimbali wa Mkoa wa Mara na kwingineko nchini wakiombwa kujitokeza kwa ajili ya kukinusuru kikosi hicho.

Kaimu mwenyekiti wa timu hiyo, Augustine Mgendi alisema wamekuwa na kipidi kigumu cha kulipa mishahara ya wachezaji na benchi la ufundi hivyo, anawaomba wadau mbalimbali wa soka wenye nia njema na kikosi hicho kujitokeza kuweza kukinusuru.

“Ni kweli tumekuwa na kipindi kigumu kwa sababu tuna zaidi ya miezi miwili wachezaji na hata benchi la ufundi hatujalipa mishahara yao, tunashukuru tumekuwa bega kwa bega na serikali ya mkoa japo jitihada za kuinusuru zinahitajika,” alisema.

Mgendi aliongeza anatoa wito kwa makampuni au taasisi mbalimbali kujitokeza kuisaidia timu hiyo, akiamini itakuwa njia nzuri kwao ya kuwapa morali wachezaji ya kupambana zaidi na kufanikiwa malengo ya kuirejesha Ligi Kuu Bara msimu ujao.

Timu hiyo ambayo hufahamika kama ‘Wanajeshi wa Mpakani’ inapambana kurejea tena Ligi Kuu Bara baada ya kushuka msimu wa 2021-2022, iliposhinda michezo mitano kati ya 30 iliyocheza, ikitoka sare 13 na kupoteza 12 ikiwa nafasi ya 15 na pointi 28.

Related Posts