PAMOJA na kukubali kupunguzwa kasi kwenye Championship, Geita Gold imesema ni mapema sana kwa timu yoyote kutamba kupanda Ligi Kuu, ikieleza kuwa hesabu zao ni kushinda kila mechi na kusubiri hatma yao.
Geita Gold ilishuka daraja msimu uliopita sambamba na Mtibwa Sugar, lakini timu hizo zimeonekana kuwa bora zikikomaa nafasi mbili za juu na kuwa na matuamini ya kurejea tena Ligi Kuu.
Juzi ikiwa ugenini mkoani Mtwara ilijikuta ikipoteza mechi yake ya kwanza dhidi ya Mbeya Kwanza kwa kichapo cha mabao 2-0 na kushuka nafasi ya pili kwa pointi 17 huku Mtibwa wakipaa kileleni kwa alama 19.
Kocha Mkuu wa timu hiyo, Aman Josiah alisema licha ya matokeo waliyoanza nayo lakini ni mapema kutamba kupanda Ligi Kuu badala yake ni kutafuta ushindi kila mechi ili kufikia malengo.
Alisema kuwa kupoteza mechi ya kwanza haiwezi kuwatoa mchezoni au kuwakatisha tamaa kwa namna yoyote akikiri kuwa ushindani ni mkali na kila timu inayo malengo ya kufanya vizuri.
“Ushindani ni mkali na ni mapema kutamba kurudi Ligi Kuu, kimsingi ni kupambana kila mchezo tupate pointi tatu, hatuwezi kukata tamaa au kubweteka kwa matokeo tuliyonayo,” alisema Josiah.
Kocha huyo wa zamani wa Biashara United na Tunduru Korosho, aliongeza siri ya mafanikio hadi sasa ni ushirikiano wa nje na ndani ya uwanja kwa kila mmoja wao kutimiza wajibu wake, huku akiweka wazi wameanza vizuri jambo ambalo ni jema kwao.