IFIKAPO Januari mwakani, mkataba wa beki na nahodha wa Simba, Mohammed Hussein ‘Zimbwe Jr’ a.k.a Tshabalala utabakiza miezi sita kumalizika na hapo kanuni inamruhusu kufanya mazungumzo na hata kuingia makubaliano ya awali ya kujiunga na timu nyingine na taarifa zinasema zipo ofa tatu zinamsikilizia.
Gazeti hili linafahamu, mpango uliopo mezani kwa Simba ni kumpa mkataba mpya kabla msimu haujamalizika ingawa upande wa mchezaji unaonekana hauna haraka ya kufanya jambo hilo kama inavyoelezwa hali ilivyo kwa kiungo mshambuliaji wa Yanga, Pacome Zouzoua anayejatwa huko Msimbazi.
Taarifa ambazo Mwanaspoti imezinasa ni kwamba Zimbwe ana ofa tatu za maana ambazo zimetua mezani kwa mchezaji huyo ambazo zinaweza kufanya mipango ya klabu yake kumbakisha kuwa migumu, ikiwamo moja ya vigogo vya soka nchini vinavyotajwa vimekuwa vikimpigia hesabu kwa muda mrefu bila kumnasa.
Ukiacha ofa hiyo ya hapa nyumbani, lakini chanzo cha kuaminika kutoka kwa mchezaji huyo ni kwamba kuna ofa mbili za klabu za nje ya nchi moja ikiwa ya Algeria na nyingine ya Afrika Kusini.
Ofa ya Afrika Kusini ni ya Kaizer Chiefs ambayo baada ya kumkosa Zimbwe mwaka 2022, imepanga kutumia fungu la maana kumnasa beki huyo ambaye ilikuwa ikimtamani kwa muda mrefu.
Gazeti hili linafahamu kuwa, Kaizer ilikuwa katika nafasi kubwa ya kumchukua beki huyo mwaka 2022, lakini walishindwana baada ya Simba kutenga fungu kubwa la dau la usajili zaidi ya lile ambalo wao waliliweka, wakati kwa ofa ta Algeria inatajwa klabu ya JS Kabylie.
Kumbuka klabu hiyo inanolewa na kocha wa zamani wa Simba, Abdelhak Benchikha ambaye anafahamu kuwa mkataba wa beki huyo unaelekea ukingoni na tayari ameshawadokeza viongozi wa timu hiyo iliyo tayari kutoa fedha ili kutimiza mpango wake wa kumsaini beki huyo wa kushoto anayeichezea timu ya taifa.
Ofa ya ndani ni ya timu ambayo ina beki wa kigeni na inataka kupunguza gharama za mshahara na nyinginezo inazotumia kwa mchezaji wao kwa kumsajili Zimbwe Jr.
“Mchezaji anawasikilizia Simba, lakini hizo ofa zipo. Kaizer ndio wanaonekana kumhitaji zaidi kwa vile walianza kuvutiwa naye toka zamani na walikuwa na nafasi kubwa ya kumpata,” alisema ndugu wa karibu wa Zimbwe Jr alipozungumza na Mwanaspoti, huku Meneja wa beki huyo, Carlos Sylivester alisema kwa sasa hakuna timu ambayo inaruhusiwa kufanya mazungumzo na beki wake kwa vile ni mchezaji halali wa Simba.
“Mohammed Hussein ni mchezaji wa Simba na kwa sasa hakuna chochote kipya. Mchezaji ana furaha katika timu yake na kama kuna chochote kitatokea, klabu itatolea ufafanuzi,” alisema Sylivester
Mwanaspoti limedokezwa mapema jana kwamba kama Yanga, isipoamka usingizini, ijue kabisa itakula kwao baada ya staa wa timu, Pacome Zouzoua kuwekewa mkakati mzito wa kumvusha upande wa pili akutakiwa na Simba.
Iko hivi. Mkataba wa Pacome na Yanga unafikia tamati mwisho wa msimu huu, huku mazungumzo yakiwa yanaendelea na mabosi wa klabu hiyo, lakini Simba wanataka kufanya kufuru la kumsomba mido huyo, ikiwa kama njia ya kulipa kisasi cha Clatous Chama aliyenyakuliwa na watani wao hao msimu huu.
Simba inataka kasi na ufundi wa Pacome katika kukiboresha zaidi kikosi chao na hesabu zao ni sawa na zile wanavyomtamani Feisal Salum ‘Fei Toto ambaye bado ana mkataba wa miaka miwili na Azam FC.
Simba inaona kuna ugumu wa kumpata Fei Toto kwa sasa kutokana na aina ya mkataba alioingia na Azam, lakini hapohapo wanaona kama wataweka nguvu kuna nafasi ya kumchukua Pacome anayeichezea Yanga kwa msimu wa pili baada ya kumsajili kutoka Asec Mimosas ya Ivory Coast na kufanya mambo makubwa.
Ingawa msimu huu hajaanza kwa kasi kubwa akifunga bao moja na asisti moja, Simba inaona Pacome bado ni kiungo bora ambaye ataongeza kitu kikubwa eneo lao la juu la kiungo mshambuliaji, nafasi ambayo kocha Fadlu Davids ameshawaeleza mabosi wa Msimbazi kuwa, anamtaka mtu sambamba na beki ya kati.
Tayari mabosi wa Simba wameweka kambi kwa meneja wa kiungo huyo, Zambro Traore ambaye pia ndio anayewamiliki mastaa watatu wa Wekundu hao Charles Ahoua, Chamou Karabou na Valentin Nouma.
Japo, Simba inafanya siri lakini Mwanaspoti linafahamu kwamba mpango mzima unasimamiwa na tajiri wa Wekundu hao, Mohammed Dewji ‘MO’ ambaye ndiye aliyempa kazi Traore kumtafutia mastaa hao watatu waliokuja kuirudishia timu hiyo nguvu msimu huu.
“Kila kitu kinafanywa kwa siri sana kati ya MO na Zambro (Traore),unajua kasi ya Pacome na ufundi wake sio kitu cha mchezo kama atakuja pale Simba, acha tusubiri kuona kitu gani kitatokea,” alisema bosi huyo wa juu wa wekundu hao.
Yanga wao wanaendelea na mazungumzo na kiungo huyo wakiamini kwamba watafanikiwa kumshawishi kuongeza mkataba mrefu zaidi kama ilivyotokea kwa Stephane Aziz KI aliyesalia kikosini hapo kwa msimu wa tatu mfululizo.