Machinjio ya Vingunguti pasua kichwa

Dar es Salaam. Wingu zito limeendelea kufunika hatua za ukamilishwaji wa mradi wa machinjio ya kisasa ya Vingunguti, ulioanza kutekelezwa Juni, 2019 wakati wa utawala wa awamu ya tano chini ya Rais John Magufuli, ukiahidiwa ungekamilika kwa miezi 18.

Ingawa mkandarasi ameshaukabidhi kwa Halmashauri ya Ilala Dar es Salaam, bado haujaanza kazi kwa ufanisi.

Licha ya kwamba machinjio hayo hayajafunguliwa rasmi kufanya kazi kama kulingana na mkataba, sasa yanatumika kinyume na ilivyotarajiwa.

Awali, ahadi za kuanza kufanya kazi rasmi, ziliambatana na kuahidiwa kwa uzinduzi rasmi uliotarajiwa kuhudhuriwa na mkuu wa nchi.

Taarifa za mwisho lilizopewa Mwananchi juu ya sababu za mkwamo huo, ni kutokamilishwa kwa chumba cha ubaridi kitakachotumika kuhifadhia nyama.

Hata hivyo, imeshapita miaka miwili tangu aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Amos Makalla aagize kufanyika kwa mchakato wa uagizaji wa vifaa vya kutengeneza chumba hicho.

Awali, iliahidiwa iwapo yatakamilika yatakuwa na uwezo wa kuchinja ng’ombe 1,500 kwa siku badala ya 1,000 waliochinjwa kabla.

Kwa upande wa mbuzi na kondoo ilielezwa kwa siku, wangechinjwa 3,000 badala ya 500 waliokuwa wakichinjwa katika machinjio ya zamani.

Kwa mujibu wa chanzo cha kuaminika, kuna vyumba viwili vidogo vilivyofungwa mtambo wa ubaridi na inadaiwa ndivyo vitakavyotumika, lakini hadi sasa havijawashwa.

Hata hivyo, chanzo hicho kinaeleza Mwananchi kuwa, vyumba hivyo viwili si kile kilichoahidiwa awali kwa sababu ni vidogo.

“Hivyo vyumba vilivyofungwa mashine hizo ni stoo na tunaona ni kama zuga endapo kiongozi mkubwa atafanya ziara hapa, havitasaidia,” kinaeleza chanzo hicho.

Kwa mujibu wa chanzo hicho, inashangaza uwekezaji mkubwa wa Serikali katika mradi huo unaishia ulipoishia sasa.

Mwananchi ilimtafuta Msemaji Halmashauri ya Jiji la Ilala, Tabu Shaibu kujua mkwamo ni nini, ambaye amesema hana majibu ya kina kwa sababu jambo hilo linashughulikiwa na taasisi mbalimbali na liko katika ngazi ya kiutendaji.

“Sio kwamba hakuna kinachoendelea, lakini mradi ule una mambo mengi ambayo hayashughulikiwi na sekta moja tu, hivyo siwezi kukwambia kwa sasa kama nina majibu yoyote kuhusu nini kinachoendelea,” amesema Tabu.

Alipotafutwa Naibu Meya wa Halmashauri ya Jiji hilo, Ojambi Masaburi Masaburi licha ya kudai atafutwe mwenye mamlaka ya kusema kwa niaba ya Baraza la Madiwani, alidokeza jambo hilo linatarajiwa kuzungumzwa katika kikao cha baraza cha wiki ijayo.

Mwananchi haikuishia hapo, ilimtafuta Meya wa Jiji, Omar Kumbilamoto aliyetaka aulizwe Ofisa Mifugo wa Halmashauri.

Mwananchi ilipomtafuta Meneja wa Machinjio hayo, Dk James Kawamala ambaye amesema wanatarajia yataanza kazi rasmi mwezi huu.

Amesema ukamilishwaji wa viyoyozi umefikia asilimia 95 huku vyumba vya majokofu, vikifikia asilimia 97.

Dk Kawamala  amesema mashine za machinjio hayo zinachinja na kuchakata nyama na kwa kila ng’ombe mmoja inatumia dakika tano na kwa saa nane, jumla ya ng’ombe 500, mbuzi 1000 huchinjwa.

Meneja huyo amesema mradi huo ulikuwa ukitarajia kutumia Sh12.5 bilioni hadi kukamilika kwake lakini mpaka sasa umetumia Sh19.5 bilioni.

Fedha hizo zimetumika kwenye ujenzi majengo, uwekaji wa mitambo, ujenzi wa mifumo ya majisafi na taka, mitambo ya viyoyozi na majokofu pamoja na kuwalipa wananchi fidia.

Mradi huo umetekekezwa na mkandarasi kutoka Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) kwa gharama ya Sh12.5 bilioni zinazotokana na mapato ya ndani ya halmashauri.

Kwa mujibu wa meneja wa mradi, Mburuga Matamwe, uchinjaji utafanywa kwa mitambo itakayosimikwa katika machinjio.

Mitambo hiyo inahusisha ile ya kuchinjia, mikasi ya umeme ya kukatia kwato na pembe, mashine za kuchuna ngozi na mikanda ya kusafirishia nyama na bidhaa za nyama kutoka sehemu moja hadi nyingine.

Pia, jengo hilo litakuwa na sehemu ya kuchinjia, kuvujishia damu, matanki ya kuhifadhia damu, maji taka na sehemu ya kuhifadhi kwato na pembe.

Kutakuwa na vyumba nane vya kuhifadhia nyama vyenye uwezo wa kuhifadhi ng’ombe 580, mbuzi na kondoo 160 wakichinjwa kwa wakati mmoja.

Pia, kutakuwa na maduka maalumu ya kuuzia nyama, vyakula na jenereta la ziada kwa ajili ya kufua umeme endapo umeme wa gridi ya Taifa utakatika.

Alipotafutwa kuzungumzia mkwamo huo, Meneja wa Mawasiliano kwa Umma wa NHC, Muungano Saguya amesema walishakabidhi kazi mwaka mmoja uliopita baada ya kukamilisha kwa mujibu wa masharti ya mkataba.

Pia, amesema hadi sasa, kipindi cha matazamio ya mradi kimeishia Januari mwaka huu, hivyo hakuna wanachodaiwa.

Alipoulizwa kwa nini mradi haufanyi kazi amesema, “nadhani kwa nini majengo hayatumiki hadi sasa mnapaswa kuwauliza wenye mradi wenyewe labda wanaweza kuwa na majibu.

“Ila tu niseme, sisi kazi yetu tulishaimaliza na kuukabidhi mradi kwa wenyewe, mnaweza kuwauliza wanaweza wakawa na sababu zao labda.”

Mradi huu ulianza kupamba moto baada ya Septemba 16, 2019, Rais wa wakati huo, John Magufuli, alipoutembelea na kushuhudia hali ya uchafu iliyokuwepo hapo.

Kutokana na hilo alipunguza muda wa ujenzi uliokuwa umepangwa kuchukua miezi 18 na kutaka ukamilishwe ndani ya miezi mitatu. Kwa maana ulipaswa ukamilike Desemba 31, 2019.

Hata hivyo, haukufanikiwa na hadi anafikwa na mauti Machi 17, 2021 haukuwa umekamilika kuanza kazi. Akaingia Rais Samia Suluhu Hassan, Machi 19, 2021 na mpaka sasa haujaanza kazi.

Tangu wakati huo, viongozi mbalimbali wakaanza kupigana vikumbo kuutembelea akiwamo Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa aliyefika hapo Desemba 3, 2019 na Mei 17, 2021.

Majaliwa katika ziara yake ya Mei 17, 2021 aliagiza uongozi wa Jiji kuhakikisha hadi Juni 30, 2021 uwe umekamilika, baada ya aliyekuwa Mkurugenzi wake, Jumanne Shauri kueleza ulishindwa kukamilika kama ilivyoagizwa na Rais, awali baada ya kuwepo kwa mvua kubwa iliyosababisha ujenzi kusimama.

Hata hivyo, wakati Majaliwa anakwenda hapo, mradi huo ulikuwa umekamilika kwa asilimia 95 na aliagiza kazi za kuchinja zianze ili wafanyabiashara waanze kuzoea.

Siku hiyo alimuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kuhakikisha marekebisho madogo madogo yaliyosalia yanakamilika ili mradi uanze kutumika rasmi.

Pia, aliyekuwa Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Joseph Nyamhanga, alitembelea hapo na kuelekeza uongozi wa Jiji la Dar es Salaam kuhakikisha machinjio hayo yanaanza kutoa huduma.

Wakati Nyamhanga akitembelea machinjio hayo, alielezwa tayari ujenzi wake umekamilika kwa asilimia 98.

“Kwa kuwa ujenzi wa machinjio hii umeshakamilika kwa kiwango cha kuanza kutoa huduma sasa inatakiwa kazi zianze hata kwa kuchinja ng’ombe, mbuzi na kondoo wachache mpaka hapo mtakapokamilisha ujenzi kwa asilimia 100,” alisema.

Alisema machinjio hayo yakianza kutoa huduma Halmashauri itakua inakusanya Sh2 bilioni hadi Sh5 bilioni za mapato na hivyo kupunguza utegemezi wa Serikali.

Ma-RC wanne wagonga mwamba

Hadi sasa ni wakuu wa mikoa wanne wamepita Dar es Salaam bila mradi huo kuanza kazi rasmi.

Wakuu hao wa mikoa ni Paul Makonda (sasa Mkuu wa Mkoa wa Arusha), Aboubakar Kunenge (sasa Mkuu wa Mkoa wa Pwani), Amos Makalla (sasa Katibu mwenezi CCM) na wa sasa Albert Chalamila.

Makonda alikuwa akifanya ziara hadi za usiku kuhakikisha agizo la Rais la kukamilika kwa machinjio hayo ndani ya miezi mitatu linakamilika na moja ya ziara aliifanya Oktoba 14, 2019.

Kunenge naye Desemba 2 2020, alitembelea hapo akiwa na kamati yake ya Ulinzi na Usalama.

Akiwa hapo, Kunenge alisema hatua iliyofikiwa ya majaribio ya uchinjaji wa mifugo ni ya kutia moyo ingawa bado kuna kazi kubwa inatakiwa kufanywa ili kukamilisha machinjio hayo mapya kwa wakati.

Aidha, alisema nyama itakayochinjwa katika machinjio hayo itakuwa ni ya kisasa inayowezwa kusafirishwa kwenda nje ya nchi kwa ajili ya kitoweo kwa kuwa imezingatia vigezo vyote muhimu vya afya.

Mwaka 2022, Makalla kwa wakati wake alitembelea eneo hilo na kuonyesha kutoridhishwa baada ya kuambiwa sababu kubwa ya kutoanza kazi kwa machinjio hayo ni kutokamilika kwa chumba cha kuhifadhi baridi.

Kutokana na hilo, Makalla aliagiza halmashauri kuanza mchakato wa kumpata mkandarasi wa  kutengeneza chumba hicho cha ubaridi.

Desemba 22, 2023 Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam wa sasa, Albert Chalamila naye alitembelea na kumtaka mkandarasi anayesimamia mradi huo kuukamilisha kwa wakati uliopangwa.

Pia, katika ziara hiyo alimuagiza mkuu wa wilaya kuunda kamati maalumu itakayochunguza mwenendo wa utendaji kazi katika machinjio hiyo ili kubaini changamoto zilizopo na kutoa mapendekezo ya mambo ya kufanya ili kuboresha shughuli zinazoendelea machinjioni hapo.

Licha ya kununuliwa mashine mpya kwenye machinjio ya kisasa ya Vingunguti, wafanyabiashara wamelalamikia hazifanyi kazi kama walivyokuwa wanatarajia.

Kutokana hatua hiyo, wafanyabiashara hao wamerudi kwenye mfumo wa zamani wa kutumia wachinjaji katika kuhakikisha wanapata nyama kwa ajili ya wateja wao.

Mmoja wa wafanyabiashara, Ahmad Issa amesema mashine zilizopo katika machinjio hayo hazifanyi kazi kama ilivyotarajiwa, wamekuwa wakiendelea kuchinja ng’ombe kama zamani.

Issa amesema kati ya ng’ombe 400 wanaochinjwa sasa ni 10 hadi 15 pekee ndizo wanapelekwa kwenye mitambo kwa ajili ya kupasuliwa ili kuondoa vitu vya ndani.

“Kwa upande wa uchunaji tunaona watu ndiyo wanachuna kwenye upasuaji, zinatumika mashine zinazotumia umeme yaani mambo mengi bado tuliahidiwa kufunguliwa lakini hadi leo hii ni mwaka wa tatu na tozo wanatutoza za machinjio mpya wakati haijaanza kazi na wanatuambia ikikamilika wanapandisha tena tozo,” amesema Issa.

Hata hivyo, Issa amelalamikia kufanya kazi taratibu kwa mitambo hiyo, tofauti na ilivyoahidiwa awali kwamba kila kitu kingekwenda haraka.

Sakina Samwel ni mfanyabiashara, amesema kazi inayofanywa na mashine hizo ni kutoa vitu vya ndani.

Amesema chumba cha kuchinjia ni kidogo kutokana na wingi wa ng’ombe wanaoingizwa na hakimpi mfanyabiashara fursa ya kwenda kuhakiki, anaishia kusubiri nyama ambayo hana uhakika kama ni ya kwake au la.

Eneo la kuhifadhi kinyesi cha ng’ombe ni changamoto nyingine katika machinjio hayo, kama inavyoelezwa na mfanyabiashara, Abraham Rajabu.

Amesema malalamiko mengine kwa upande wa zizi lililojengwa kwenye machinjio hayo ni dogo linahifadhi ngombe 350 wakati ngombe wanaopelekwa ni zaidi ya 400.

Rajabu  ameitaja changamoto nyingine ni sehemu ya kuhifadhia nyama kwa kuwa bado chumba cha ubaridi hakijakamilika.

George Saimon Kifuko ambaye ni Mwenyekiti wa kamati ya malisho na utatuzi wa migogoro ya wafugaji na watumiaji wengine wa ardhi, amesema kutoanza kazi kwa machinjio hayo hadi sasa ni jambo la kusikitisha.

Saimon aliyewahi kuwa Mwenyekiti wa Wafugaji Tanzania, amesema wakati kuna miradi inaendelea ya kunenepesha mifugo, machinjio hayo yangekuwa mkombozi wa kuwapatia soko la nje la uhakika na kuuza mifugo yao katika hali ya ubora wa juu.

“Badala yake pamoja na unenepeshaji mifugo hiyo, tumekuwa tukiuziwa mifugo kiholela, na wakati mwingine wafanyabiashara kutoka nje wanakwenda moja kwa moja kwa wafugaji kununua kwa bei za kulangua.

“Ifike mahali Serikali iwekeze nguvu kwenye miradi inayoleta faida moja kwa moja kwa wananchi kama haya machinjio ambayo yangesaidia kubadilisha maisha ya wananchi kwa kiasi kikubwa,” amesema mwenyekiti huyo.

Wasomi, wananchi washauri

Mtaalamu wa Uchumi kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) Profesa Abel Kinyondo, amesema tatizo la nchi hii watu wana kiu ya kujenga miradi mikubwa bila kufanya utafiti wa kutosha.

Profesa Kinyondo amesema ukizunguka nchi nzima kuna masoko mengi makubwa yamejengwa lakini hayatumiki na kueleza hata pale Karume jijini Dar es Salaam licha ya kuwepo Jengo la Wamachinga, bado watu wanakaa barabarani kuuza bidhaa.

“Tutaendelea kufanya hayo, kwa sababu hakuna mtu anayewajibika, miradi inayojengwa halafu haitumiki kwani katika nchi nyingine hayo hayafanyiki hasa pale wanapoomba fedha kwa ajili ya mradi fulani, huwa mtu anaulizwa kwanza mradi uliopita umefanya nini na kutuletea faida gani hadi sasa.

“Pia, usikute huyo aliyeandika rasimu ya machinjio hayo ya Vingunguti, yupo ameshaandika rasimu ya machinjio mengine ya kuku na hakuna wa kumuhoji,” amesema mwanataaluma huyo.

Hata hivyo, amesema haya yanafanyika kwa kuwa, maeneo ambayo watu wanapiga fedha ni haya ya ujenzi wa miradi na ndio maana kila siku mambo yanajirudia.

Profesa Kinyondo amesema Dar es Salaam bado watu wanakula nyama, licha ya kuwa machinjio hayafanyi kazi na hakuna aliyewahi kulalamika kuhusu ubora, ina maana hakukuwa na haja.

Mchambuzi na mshauri wa masuala ya kiuchumi na Kijamii, Oscar Mkude amesema athari za kutoanza kutumika kwa mradi huo wa machinjio ni kubwa kwa sababu baadhi ya vifaa huenda visifae kutumike tena hivyo Serikali ikalazimika kuingia gharama za ziada.

“Yale malengo ya kujengwa kwa mradi huo yanaweza yasitimie ikiwamo kuchinja nyama kisasa na kusafirisha nje ya nchi,” amesema Mkude.

Athari nyingine amesema ni kwa mlaji kula nyama inayochinjwa katika mazingira mabaya, lakini wanaochinja wanafanya kazi katika mazingira magumu na kubwa ni fedha iliyowekwa pale haizalishi zaidi ya kuteketea.

Amedai hali inavyoonekana hueda mradi huo ulikuwa wa viongozi fulani na haukuwa kwenye bajeti.

“Nakumbuka kipindi cha Makonda akiwa mkuu wa mkoa alisema ni moja ya mradi mkubwa sana, sasa sijui kimetokea nini hapa haupewi kipaumbele,”amesema Mkude.

“Ukweli kwamba bado kwenye sekta ya uchinjaji hatupo vizuri kuanzia uchakataji wake, ubebaji hadi kufika kwa mteja wa mwisho, hivyo machinjio hayo kwa namna tulivyoelezwa ingekuwa muhimu.”

Baadhi ya wananchi akiwamo Shalom Kilaga, mkazi wa Vingunguti, amesema inaleta hasira miradi mikubwa kutumia fedha za walipa kodi mwisho inatelekezwa.

“Kulikuwa na haja gani ya kuteketeza zaidi ya Sh4 bilioni hapa kama hawakuwa tayari kuutumia huu mradi, hizo fedha si bora wangeenda kununulia dawa hospitali, kuokoa maisha ya Watanzania wengi,” amesema.

Mathias John, mkazi wa Gongolamboto, amesema inaonyesha viongozi waliopo hawajavutiwa na mradi huo wala kuona umuhimu wake, ndiyo maana hawaumizwi na wanachokiona.

Related Posts