Dar es Salaam. Mfanyabiashara na mkazi wa Mji mdogo wa Tunduma, Ombeni Sanga (30) anashikiliwa na Polisi kwa tuhuma za kuendesha gari kwa uzembe na kusababisha kifo cha askari polisi WP.11725 Koplo Leokadia Mwenda.
Taarifa ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Songwe, Augustino Senga aliyoitoa kwa umma leo Jumapili, Novemba 10, 2024 inaeleza Sanga aliendesha gari Toyota Rumio,“kwa uzembe, kisha kuacha njia, kupinduka na kusababisha kifo kwa Askari WP.11725 Koplo Leokadia.“
Amesema ajali imetokea saa 8:15 usiku wa leo Jumapili, eneo la Old Vwawa, tarafa ya Vwawa, Wilaya ya Mbozi, Mkoa wa Songwe katika barabara ya Mbeya – Tunduma.
Gari hilo lililokuwa likitokea Tunduma kuelekea Vwawa liliacha njia, kupinduka na kusababisha kifo cha askari huyo. Pia, katika ajali hiyo, askari mwingine namba WP.11533 Koplo Tabia amejeruhiwa na anaendelea kupatiwa matibabu katika Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Songwe.
“Uchunguzi umebaini kuwa chanzo cha ajali ni uzembe wa dereva kushindwa kulimudu gari kutokana na mwendo kasi,“ amesema Kamanda Senga.