Minziro kufyeka wavivu Pamba Jiji

PAMBA Jiji bado inajitafuta katika msimu wa kwanza wa kurejea katika Ligi Kuu Bara na sasa kocha wa kikosi hicho, Fred Felix ‘Minziro’ ameweka bayana atatembeza panga kufyeka wachezaji wote wasiojituma kupitia dirisha dogo litakalofunguliwa mwezi ujao na kufungwa Januari 15 mwakani.

Pamba imerejea Ligi Kuu baada ya kuisotea kwa miaka 23 tangui iliposhuka mwaka 2001 na hadi sasa imeshinda mechi moja na kushika nafasi ya pili kutoka mkiani ikikusanya pointi nane kupitia mechi 11, jambo lililomzindua kocha Minziro aliyetoa tangazo la onyo kwa mastaa wa kikosi hicho mapema.

Minziro aliyejiunga na Pamba, Oktoba 17 akichukua mikoba ya Goran Kopunovic na kuonja ushindi wa kwanza msimu huu wa kuifumua Fountain Gate kwa mabao 3-1, sambamba na sare moja na kupoteza mbili katika michezo minne aliyoiongoza alisema kikosi hicho kina changamoto ya majeruhi , pia kuna udhaifu kwenye utimamu na mazoezi lakini kwa sasa angalau kuna mabadiliko yaliyofikia asilimia 60 ya anachokitaka.

Hata hivyo, alisema pamoja na kufikia hatua nzuri, bado anaona kuna hata ya kuboresha kikosi kwa kuongeza mashine mpya katika dirisha dogo na kuwatema wale ambao hawana msaada kikosini.

“Tutaboresha timu kwenye idara zote kusudi ndani ya timu kuwepo na ushindani, wale wachezaji majeruhi wanachelewa kupona kwa muda mrefu itabidi watupishe tu hakuna namna kwa sababu kama mchezaji yuko nje muda mrefu huisaidii timu mechi 10 hadi 12 utakuwa na faida gani kubaki,” alisema Minziro na kuongeza;

“Tunataka tulete watu wengine wafanye kazi tunataka kikosi kilicho na ushindani na naamini mtauona dirisha dogo, nawaeleza wachezaji kama hufanyi kazi na hutaki kufanya mazoezi ninavyotaka, kwangu nafasi huna.”

Alisema mapumziko kupisha mechi za timu ya taifa yatamsaidia kufanya maandalizi ya nguvu na muda wa kutosha kuifahamu timu yake ili apate kikosi na kitu kilicho bora, huku akiwaahidi mashabiki kuwa boli litatembea na watu wa Mwanza watapata furaha.

Nahodha wa timu hiyo, Christopher Oruchum alisema; “Ningependa maboresho yafanyike ni kila idara tuongeze wazoefu ambao wataleta ushindani ili kiwango cha kila mtu kiimarike. Wakifanikiwa kufanya hivyo itapendeza kwa sababu itatusaidia kuinua kiwango chetu na timu pia iwe bora zaidi.”

Kwa upande wa Msemaji wa Pamba Jiji, Moses William alisema kama uongozi wameliacha jukumu lote kwa kocha Minziro na wasaidizi wake kujua nani aingie na nani atoke ilimradi timu ifanye vizuri kwani kwa sasa wanapo pabaya.

Related Posts