MAMBO ni magumu kwa Tanzania katika ligi ya dunia kwa Kriketi ya mizunguko 50 baada ya kipigo kikubwa cha mikimbio 209 kutoka kwa wenyeji Uganda, katika Uwanja wa Lugogo, jijini Kampala mwishoni mwa juma.
Tanzania iliyoanza kwa kufungwa na Italia kwa wiketi tisa katika mchezo wa ufunguzi Alhamisi, ilipokea kipigo kizito kutoka kwa wenyeji katika mchezo wake wa pili na Watanzania walishindwa hata kutengeneza nusu ya mikimbio 289, baada ya wapigaji wote 10 kutolewa wakiwa wametengeneza mikimbio 80 tu baada ya kutumia mizunguko 27 kati ya 50 iliyoweka.
Tatizo kubwa kwa Watanzania ni upigaji (batting) na walijikuta wakipoteza wiketi (wapigaji) saba hadi mwisho wa mizunguko 18 huku wakiwa wametengeneza mikimbio 58 tu.
Hadi kufikia mzunguko wa 22 Tanzania ilikuwa imeshapoteza wiketi tisa huku wakitakiwa kutengeneza mikimbio 225 ili wapate ushindi.
Katika mchezo huo, Uganda ndio walioanza kubeti na kutengeneza mikimbio 289 kutokana na mipira 300.
Mbio za kuifukuzia 289 zilianza vibaya hasa baada ya Tanzania kupoteza wapigaji sita katika kipindi kifupi. Ivan Selemani aliyetengeneza mikimbio 18 kutokana na mipira 18, Sanjay Kumar Thakor aliyetengeneza pia mikimbio 18 kutokana na mipira 48, na Ali Kimote aliyepiga mikimbio tisa kutokana na mipira 17, walipigana kiume kwa ajili ya Tanzania licha ya kupoteza mchezo.
Mwiba mkubwa kwa Watanzania katika mchezo huo alikuwa Mganda Razat Shah aliyetengeneza mikimbio 104 kutokana na mipira 97, akisaidiwa na Aipesh Ramjan aliyetengeneza mikimbio 75 kutokana na mipira 48.
Kabla ya kufungwa na Uganda, Tanzania pia ilipata kipigo cha wiketi tisa kutoka kwa Italia katika uwanja huo huo wa Lugogo.
Tanzania ndiyo walianza kubeti na kutengeneza mikimbio 173 baada ya wapigaji wote 10 kutolewa wakiwa wametumia mizunguko 43. Italia waifikia mikimbio hiyo wakiwa wamepoteza wiketi moja tu baada kutumia mizuguko 27.
Kwa upande wa Tanzania, Mukesh Maker aliyetengeneza mikimbio 50 kutokana na mipira 67, Omary Kitunda aliyetengeneza mikimbio 36 kutokana na mipira 59 na Ally Kimote aliyepiga mikimbio 27 kutokana na mipira 35 ndio waliofanya vizuri licha ya kuukosa ushindi.
Kwa Italia, aliyesaidia sana kuwapa ushindi alikuwa ni Emillio Gay alyetengeneza mikimbio 96 kutokana na mipira 87.
Tanzania imebakiza mechi mbili dhidi ya Bahrain na Hongkong ambazo zitafanyika juma hili.