Fei Toto, Aziz KI vita ni kali

Bao moja alilolifunga nyota wa Azam FC, Feisal Salum ‘Fei Toto’ katika mchezo wa jana dhidi ya Mtibwa Sugar limemfanya kufikisha mabao 15 ya Ligi Kuu Bara akiwa sambamba na nyota wa Yanga, Stephane Aziz Ki waliopo kwenye vita ya ufungaji bora.

Feisal alifunga wakati Azam ikiitandika Mtibwa Sugar mabao 2-0, jana na kuendeleza kushikilia nafasi ya pili kwenye msimamo baada ya kufikisha pointi 57 nyuma ya vinara Yanga iliyojikusanyia pointi 65 zikiwa zote zimecheza michezo 25.

Katika mchezo huo mbali na Feisal aliyefunga ila bao lingine lilifungwa na Gibril Sillah dakika ya 65 na kuzidi kuiweka Mtibwa Sugar katika nafasi mbaya ya kushuka daraja kwani kichapo hicho ni cha 16 kwao katika michezo 25 iliyocheza hadi sasa.

Mtibwa inayoburuza mkiani katika michezo hiyo 25 imeshinda minne tu na kutoka sare mitano ikiwa imekusanya pointi zake 17. 

Mchezo wa mzunguko wa kwanza baina ya timu hizi uliopigwa Uwanja wa Azam Complex Chamazi, Azam ilishinda pia kwa mabao 5-0, Novemba 24, mwaka jana.

Mbali na huo ila pia mchezo wa mwisho uliopigwa kwenye Uwanja wa Manungu Complex Morogoro, Mtibwa ilichezea kichapo cha mabao 4-3, Novemba 12, 2022.

Akizungumzia matokeo hayo Kocha wa Mtibwa Sugar, Zubery Katwila alisema walipambana kadri ya uwezo wao ingawa makosa binafsi waliyoyafanya yalisababisha kupoteza japo wanaendelea kupambana kwa ajili ya michezo ijayo ili kujua hatma yao.

Kwa upande wa Kocha wa Azam FC, Youssouph Dabo aliwapongeza wachezaji wa timu hiyo kwa kuonyesha kiwango kizuri licha ya kipindi cha pili kuathiriwa na mvua na kusababisha kasi ya mechi hiyo kupungua.

Katika mchezo mwingine uliopigwa mapema saa 8:00 mchana kwenye Uwanja wa CCM Liti mjini Singida ulishuhudia Ihefu SC ikiibuka na ushindi wa mabao 2-0, dhidi ya Namungo kwa mabao yaliyofungwa na Wakenya, Elvis Rupia na Duke Abuya.

Ushindi huo unakuwa ni wa kwanza kwa Ihefu kwani tangu ilipoanza kukutana na Namungo msimu wa 2020/2021, ilikuwa haijawahi kushinda.

Katika michezo mitano kabla ya huo, Namungo ilikuwa mbabe zaidi kwani ilikuwa imeshinda michezo mitatu huku miwili pekee ikiisha kwa sare jambo ambalo limeufanya mchezo huo kuwa wa kisasi zaidi na wenye ushindani kutokana na rekodi hizo.

Hata hivyo, mechi ya mzunguko wa kwanza timu hizo zilipokutana kwenye Uwanja wa Majaliwa Novemba 23, mwaka jana, Ihefu ilifungwa mabao 2-0, yaliyofungwa na nyota wa kikosi hicho, Pius Buswita dakika ya 36 na Hamad Majimengi dakika ya 78.
Ushindi huo ni wa kwanza kwa Ihefu baada ya kucheza michezo mitano mfululizo ya Ligi Kuu Bara bila ya ushindi tangu mara ya mwisho ilipoifunga KMC bao 1-0 katika mechi iliyopigwa kwenye Uwanja wa CCM Liti mjini Singida Machi 5, mwaka huu. 

Matokeo hayo yanaifanya Ihefu kusogea hadi nafasi ya 11 na pointi 28 baada ya kushinda michezo saba, sare saba na kupoteza 11 huku upande wa Namungo ikishika nafasi ya 12 na pointi 27 kufuatia kushinda sita, sare tisa na kupoteza 10

Related Posts