KIUNGO mshambuliaji wa Hua Hin City, Mtanzania John Mgong’os amesema sababu ya kupoteza mchezo dhidi ya Raj Pracha 2-1 ni uchovu kutokana na umbali mrefu kutoka walipo hadi uwanjani.
Nyota huyo anayeichezea timu hiyo ya Ligi daraja la pili Thailand maarufu ‘TL3’ akiwa Mtanzania pekee nchini humo, aliliambia Mwanaspoti umbali mrefu waliotumia uliwasababishia na kuwafanya wasicheze kwa kiwango chao.
Mgong’os alisema licha ya kupoteza mmoja kwenye mechi tisa ilizocheza timu hiyo lakini bado kwenye hatua nzuri ya kuendelea kupambana kurudi Ligi Kuu.
“Tuna nafasi nzuri kama tutakuwa na muendelezo mzuri wa matokeo na naamini msimu huu tunaweza kucheza ligi kuu Thailand licha ya ugumu wa timu tunazokutana nazo,” alisema Mgong’os.
“Mechi ya nane ilikuwa mbaya sana kijumla hatukuwa na kiwango bora nilipata nafasi ya kuingia dakika 56 kulikuwa na uchovu kwa wachezaji naamini zijazo tutafanya vizuri.”