LICHA ya uwepo wa kocha Juma Mgunda na msaidizi wake Seleman Matola, beki Mkongomani wa Simba, Henock Inonga ambaye alikuwa kati ya wachezaji wa akiba amegeuka kocha katika mchezo wa Ligi Kuu Bara ambao timu hiyo imeibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Tabora United.
Bao la Sadio Kanoute katika dakika ya 19 likiwa la tatu kwake msimu huu na Edwin Balua katika dakika 77 kwenye Uwanja wa Azam Complex, yalitosha kwa Wekundu wa Msimbazi kufikisha pointi saba wakiwa chini ya Mgunda aliyekaimishwa nafasi ya Abdelhak Benchikha aliyeachana na timu hiyo baada ya kuipa ubingwa wa Muungano.
Katika kipindi cha kwanza mara kadhaa Inonga ambaye anahusishwa na FAR Rabat ya Morocco mwishoni mwa msimu, alikuwa akifanya mawasiliano na mabeki wenzake Che Malone Fondoh pamoja na Kennedy Juma ambao walikuwa wakiunda ukuta wa timu hiyo kuhakikisha kwamba lango lao linakuwa salama.
Inonga ambaye wakati huo alikuwa ameketi alionekana kuwakumbusha majukumu yao mabeki hao baada ya kufanya kosa kubwa katika dakika ya 24 ambapo Kennedy alishindwa kuokoa mpira ambao pia ulimpita Che Malone.
Hata hivyo, nyota wa Tabora United, Kalumba Banza alishindwa kutumia nafasi hiyo kwa mpira wake kuchezwa na kipa Ayoub Lakred ambaye ameendelea kuonyesha kiwango bora akiwa na timu hiyo.
Hali ilionekana kuwa tofauti kwa Inonga katika kipindi cha pili, Mkongomani huyo alisimama kwa dakika zote huku safari hiyo akihamia upande wa washambuliaji ambao walikuwa wakicheza karibu naye.
Inonga alikuwa akionekana kutupa mikono huku na kule kama vile ambavyo makocha wamekuwa wakifanya na muda mwingine kwa ishara na hata pale ambapo mwamuzi wa kati hakuonekana kufanya sawasawa alionyesha wazi kutokubaliana naye.
Tukio la namna hiyo limekuwa likifanywa na wachezaji kadhaa wenye wito wa ukocha na muda mwingine wenye shauku ya kutaka kuona timu zao zinapata matokeo ya ushindi.
Katika uwanja huuhuu wa Azam Complex, eneo hilohilo ambalo alisimama Inonga ndipo Stephane Aziz KI naye alikuwa akihasisha wenzake baada ya kutolewa ili kufanya kweli Machi 14 katika mchezo wa ligi dhidi ya Geita Gold.
Ushindi ambao Simba imeupata umeifanya timu hiyo kufikisha pointi 54, ikiendelea kusalia nafasi ya tatu nyuma ya Azam wenye pointi 57 huku ikiwa nyuma kwa mchezo mmoja. mapema leo Azam imeibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Mtibwa.
VIKOSI
SIMBA: Ayoub Lakred, Israel Mwenda, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, Che Malone, Kennedy Juma, Fabrice Ngoma, Edwin Balua, Sadio Kanoute, Freddy Michael, Mzamiru Yassin na Ladack Chasambi.
TABORA UNITED: Noble John, Shafih Maulid, Abdallah Salum, Andy Bikoko, Pemba Kingu, Daud Rashid, Daniel Lukandamila, Najim Mussa, Eric Okutu, Kalumba Banza na Impiri Mbombo.