Kama ulishtuka kusikia bosi wa Yanga,Hersi Said yupo jijini Lubumbashi nchini DR Congo akifuata mashine mpya, basi sikia na hii namna ambavyo vigogo wa klabu hiyo walivyogawana anga wakishambulia ndani na nje ya nchi kusaka mashine mpya.
Matamanio yaliyopo nyuma ya vigogo hao ni kuhakikisha Yanga inacheza fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu ujao na siyo robo fainali kama ilivyokuwa msimu huu.
Hersi ambaye mashabiki wanamwaminia kwenye dili za usajili, Mwanaspoti limejiridhisha yupo DR Congo akimalizana na klabu mbili juu ya kuchukua mastaa wawili wa taifa hilo ambalo wachezaji wake wamekuwa na kismati cha kutamba kila wanapokanyaga Jangwani. Wa kwanza anayewindwa na Hersi huko ni winga Agee Basiala wa Klabu ya Union Maniema, lakini pia beki wa kushoto wa FC Lupopo, Chadrack Boka. Klabu hizo zote mbili ndani ya miaka ya hivi karibuni zimewapa Yanga mastaa na wakang’ara na zina uhusiano mzuri wa nje ya uwanja.
Huku ndani ya nchi nako Yanga wanafanya jambo. Arafat Haji ambaye ni makamu wa rais kapanda ndege kwenda kumaliza dili la yule kiungo mkabaji ambaye Mwanaspoti lilikuambia wiki iliyopita anayekiwasha Singida Fountain Gate, Yusuf Kagoma. Za ndaani zinasema Kagoma aliyewahi kuwika na Geita Gold hataki kuendelea na Singida FG akiwa na madai mengi dhidi ya klabu hiyo lakini muafaka ambao unataka kumaliza mzozo huo ni kwa klabu hiyo kuamua kumuuza Yanga.
Wakati Arafat anakwenda kuhakikisha Yanga inaondoka na pointi tatu dhidi ya Mashujaa juzi baada ya mchezo huo akacheza akili kubwa tena kwa siri kubwa na Kagoma na kumaliza kila kitu na sasa imebaki hatua ya timu hizo mbili kumalizana.
“Kilichosalia sasa ni klabu zenyewe kumalizana lakini mchezaji na Yanga tayari kila kitu kimeshakamilika na bahati nzuri klabu hizi mbili haziwezi kupishana watalimaliza tu hili kutokana uhusiano wa viongozi,” alisema mmoja wa marafiki wa karibu wa kiungo huyo.
Juzi kabla ya mchezo wa Mashujaa Arafat akizungumza na televisheni ya timu hiyo alisema hesabu zao za usajili kila kitu kipo sawa na wanayafanyia kazi maeneo ambayo wanataka kuyaboresha.
“Tunaelekea kumaliza msimu tayari tuliona wakati wa dirisha dogo tulishajua mapungufu yetu yako wapi tukaboresha kidogo pale na kuelekea dirisha kubwa nako kuna maeneo tunataka tuyaimarishe, mipango ilishaanza na hivi tunavyozungumza kutokea Kigoma kuna mambo yataendelea ndani ya huu mkoa haya yote ni kuendeleza furaha ya wanachi,” alisema Arafat akizungumzia mipango ya usajiliwa timu yao.
Msimu wa Ligi Kuu Bara uko ukingoni ambapo Yanga inapewa nafasi kubwa kitakwimu kutetea ubingwa wake huku Simba na Azam wakiipambania nafasi ya pili kushiriki Ligi ya Mabingwa Afrika. Yanga imepania kumaliza usajili kabla ya msimu huu kumalizika ili Kocha atapoenda mapumziko mafupi awe ameshakamilisha hesabu zake za msimu ujao.
Simba nayo iko kwenye mikakati ya chinichini kujipanga kwa kuanzia na benchi la ufundi mpaka uwanjani. Jana ilikuwa inacheza na Tabora United lakini mabosi wa timu hiyo wameshatuma mtu kwa beki wa kati wa ASEC Mimosas, Anthony Tra Bi Tra. Mimosas ndiyo timu iliyowauzia Yanga mastaa Pacome Zouazoua, Azizi Ki na Yao Kouasi Attohoula ambao kwa sasa wanatamba na takwimu zao zinawabeba uwanjani.
Hesabu za vigogo hao wa Simba zinakuja baada ya kutokuwa na uhakika wa kubakia msimu ujao kwa beki wa kikosi hicho, Henock Inonga ambaye taarifa zinaeleza mwishoni mwa msimu huu anaweza kuondoka ili kutafuta changamoto mpya huku FAR Rabat ya Morocco ikimuhitaji. Tra Bi Tra ameiongoza ASEC Mimosas kufika hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika huku akionyesha nia ya dhati ya kutaka kuondoka kutafuta changamoto mpya baada ya kuitumikia timu hiyo tangu mwaka 2021 akitokea FC Foix.
Tayari mabosi hao wameanza kujipanga mapema baada ya kuona ubingwa wa Ligi Kuu Bara msimu huu ni ngumu kuuchukua kwani watani zao Yanga wako kwenye nafasi nzuri ya kuuchukua kwa mara ya tatu mfululizo jambo ambalo hawataki litokea msimu ujao.
Simba mpaka sasa ina asilimia kubwa ya kumpata beki mzawa wa Coastal Union, Lameck Lawi mwenye uwezo wa kucheza nafasi tatu tofauti kuanzia beki wa kati, beki wa kushoto na kiungo wa kati jambo linalowafanya kuhamishia nguvu kwa nyota wa kigeni.
Tra Bi Tra raia wa Ivory Coast mwenye umri wa miaka 25 ameonyesha nia ya kujiunga na Simba msimu ujao jambo linaloweza kurahisisha dili hilo kutiki licha ya vyanzo kutoka kwa beki huyo vikieleza klabu mbalimbali za Ufaransa zinamuhitaji.
Chanzo cha kuaminika kutoka ndani ya Simba kililiambia Mwanaspoti ni kweli nyota huyo wako kwenye mazungumzo naye ingawa bado hawajafikia makubaliano ya mwisho japo jambo linalowapa matumaini ya kumpata ni kutokana na yeye kuonyesha utayari.
Vigogo wa Simba wameonekana kufanya mambo yao kwa usiri mkubwa ingaa Meneja wa Habari na Mawasiliano, Ahmed Ally alidai kwamba suala la usajili kwa sasa ni mapema kulizungumzia ingawa wao wanatambua wana jukumu kubwa la kuboresha timu hiyo kwa ajili ya kuleta ushindani msimu ujao kwenye mashindano tofauti.
Hata hivyo Mwanaspoti linatambua wakati mchakato huo ukiendelea huko Simba kwa sasa mambo yamekuwa ni mengi kwa viongozi kwani sambamba na usajili wanasaka kocha mpya wa kikosi hicho kwa ajili ya msimu ujao. Simba inataka kuhakikisha kwanza inapata kocha mkubwa na mzoefu wa soka la Afrika baada ya Mualgeria, Abdelhak Benchikha kuondoka Aprili 28, mwaka huu kufuatia kuipa ubingwa wa Michuano ya Kombe la Muungano lililofanyika Zanzibar.
Tayari baadhi ya wachezaji wa timu hiyo ambao mikataba yao inayofikia mwishoni mwa msimu huu wameanza kuongezewa ikiwemo beki, Israel Mwenda na kiungo, Mzamiru Yassin huku kazi kubwa ikibaki kwa Inonga na Kibu Denis ambao bado hakijaeleweka.