SIMBA imefanya tathmini ya ratiba ya Ligi Kuu na Kombe la Shirikisho Afrika kwa mechi za mwishoni mwa mwezi huu na mwanzoni mwa Desemba na baada ya hapo ikapeleka barua bodi ya Ligi Tanzania (TPLB) ikiwa na maombi mawili.
Ombi la kwanza ambalo Simba imeliomba ni TPLB kuurudisha mchezo dhidi ya Pamba ambao awali ulipangwa kuchezwa Novemba 21 na kuahirishwa ili kuipa fursa ya kujiandaa na mchezo wa Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Onze Bravos ya Angola, Novemba 27.
Ukiondoa hilo, Simba imeomba mchezo wake wa ugenini dhidi ya Singida Black Stars huko Singida ambao umepangwa kuchezwa Desemba Mosi uahirishwe kwa vile imebaini kuwa utaathiri maandalizi ya mechi yao ya pili ya hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya CS Constantine ya Algeria, Desemba 8. Uamuzi wa kuomba mechi dhidi ya Pamba ichezwe kwa tarehe ileile iliyopangwa awali umechangiwa kwa kiasi kikubwa na uwepo wa uhakika wa usafiri wa moja kwa moja wa ndege ambao utarahisisha timu kwenda na kurudi Mwanza kutokea Dar es Salaam na hivyo bado itakuwa na siku angalau tano za kujiandaa na mechi dhidi ya Bravos.
Simba inaamini hadi inakabiliana na Pamba, itakuwa na idadi ya kutosha ya wachezaji kwa vile wengi waliopo katika timu za taifa watamaliza majukumu yao, Novemba 19.
Wakati huohuo, Simba imebaini kuwa haitopata fursa nzuri ya maandalizi ya mchezo dhidi ya CS Constantine iwapo itacheza mechi yake ya Ligi Kuu dhidi ya Singida Black Stars.
“Ukitazama ratiba ilivyo, mchezo dhidi ya Singida Black Stars ndio ulipaswa kusogezwa mbele kwa vile hakuna ndege ya moja kwa moja kutoka Singida hadi Dar es Salaam. Maana yake tukicheza Desemba Mosi, kesho yake tutasafiri kwa basi hadi Dodoma, mwendo wa zaidi ya saa 5 kisha hapo tuunganishe kwa ndege hadi Dar es Salaam.
“Baada ya hapo kuna safari ya kuunganisha ambayo tukitoka Dar es Salaam, Desemba 3, tutaingia Algeria Desemba 4 na baada ya hapo tutaanza safari ya kwenda Constantine ambako mechi itachezwa hivyo hata wachezaje watakuwa hawajapata angalau muda kidogo wa mapumziko ndio maana tumeomba mechi dhidi ya Pamba tucheze lakini ile ya Singida isogezwe mbele hivyo tunasubiria majibu ya bodi ya ligi,” alisema kiongozi mmoja wa Simba.
Ofisa habari wa TPLB, Karim Boimanda alikiri bodi imepokea barua hiyo na itatoa majibu baada ya muda mfupi. “Ni kweli barua hiyo ya Simba imetufikia lakini bado hawajajibiwa. Bodi ikifanya hivyo tutajulisha umma,” alisema.
Simba inaongoza msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara ikiwa imekusanya pointi 25 katika michezo 10 na katika Kombe la Shirikisho Afrika imepangwa kundi A na timu za CS Constantine (Algeria), Onze Bravos (Angola) na CS Sfaxien ya Tunisia.