Sababu Serikali kuifumua sera ya sayansi, teknolojia

Dodoma. Wizara wa Elimu, Sayansi na Teknolojia imeanza mchakato wa kufanyia maboresho ya Sera ya Sayansi na Teknolojia, ambapo wadau wenye maoni wametakiwa kuyawasilisha kwa ajili ya uchambuzi.

Akizungumza mwishoni wa wiki iliyopita, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda alisema marekebisho ya sera hiyo yalisimama kupisha mageuzi ya elimu.

Alisema ili kufanikisha maboresho hayo, wameunda kamati maalum ambayo inakusanya maoni na kisha kuyachambua.

Alisema baada ya uchambuzi huo, wataangalia kama sera iliyopo ifanyiwe maboresho ama itungwe sera mpya.

Hata hivyo, alisema lengo ni kutokuwa Sera ya Sayansi na Teknolojia tena, bali sasa kuwa na Sera ya Sayansi, Teknolojia na Ubunifu.

“Karibuni tutaipeleka katika baraza la mawaziri kwa ajili ya kufanyiwa uamuzi lakini maoni yanakusanywa sasa hivi na tungependa kutangaza kuwa kila mwenye maoni apeleke katika kamati,”alisema.

Kuhusu kongamano la tisa la kitaifa la Sayansi, Teknolojia na Ubunifu litakalofanyika kuanzia Desemba 2 hadi 4, 2024 jijini Dar es Salaam, Profesa Mkenda amesema atazindua mfuko wa mikopo kwa ajili ya kusaidia ubidhaishaji na ubiasharishaji wa bunifu na teknolojia zilizobuniwa na vijana wa Kitanzania.

Alisema kongamano hilo litabeba kauli mbiu ya matumizi ya sayansi, teknolojia na ubunifu katika kuhimili changamoto za mabadiliko ya tabianchi na kuchangia kwenye uchumi shindani.

Alisema kongamano hilo ambalo Rais Samia Suluhu Hassan atalizindua, ni muhimu katika kuleta mawazo na mikakati mipya, kuimarisha utafiti na ubunifu unaojibu mahitaji na kutatua changamoto za maendeleo ya kiuchumi na kijamii.

“Pia Rais Samia atakabidhi hundi yenye thamani ya Sh6.3 bilioni kwa watafiti 19 katika masuala ya tabia nchi ikiwemo nishati safi ya kupikia,”alisema.

Naye Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Profesa Carolyne Nombo alisema bado wanakusanya maoni kutoka katika taasisi na makundi mbalimbali na baadaye watakuwa na kongamano kubwa la kuangalia maudhui yanayopaswa kuingia kwenye sera hiyo.

“Kuna kamati imeundwa kwa ajili ya kupitia sera yetu ya sayansi na teknolojia ambayo ilikuwa ni mwaka 1999 na ukiangalia kwa kweli ya muda mrefu na sayansi na teknolojia imebadilika sana, kwa hiyo tuna ulazima wa kuhuisha sera yetu,”alisema.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH), Dk Amos Nungu alisema kupitia mfuko wa Taifa wa kuendeleza sayansi na teknolojia, wamekuwa wamekuwa wakiwapatia wabunifu fedha hadi Sh40 milioni kulingana na bunifu zao.

Alisema wabunifu hao wamekuwa wanakitengeneza sampuli kifani ya bidhaa ambayo wanataka kuipeleka sokoni, lakini haikidhi sifa ya kupata mkopo benki.

“Wanaotaka kwenda kubiasharisha lakini hawajapata vigezo vya kukidhi uwekezaji, wanaweza kuwekeza pale, itakuwa wanakopa na kurudisha,”alisema.

Related Posts