Dar es Salaam. Uchunguzi uliofanywa na Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) umebaini wanawake ndio wateja wakubwa wa dawa za kulevya aina ya skanka ikidaiwa huitumia kupunguza msongo wa mawazo na kujistarehesha.
Hayo yamebainika wakati wa operesheni iliyofanyika katika kipindi cha Oktoba na Novemba, 2024 iliyowezesha kukamatwa kilo 687.32 za skanka na kilo moja ya hashishi katika eneo la Goba jijini Dar es Salaam zikiwa zimefichwa ndani ya nyumba ya mtuhumiwa.
Skanka ni jina la mtaani linaloitambulisha bangi yenye kiwango kikubwa cha sumu (TetraHydroCannabinol – THC) ikilinganishwa na bangi ya kawaida.
Dawa hii ya kulevya hutokana na kilimo cha bangi mseto, asilimia 75 ni bangi aina ya sativa na asilimia 25 ni bangi aina ya indica.
Kamishna Jenerali wa DCEA, Aretas Lyimo amesema hayo leo Novemba 12 2024 na kuongeza kuwa, uchunguzi uliofanywa na mamlaka hiyo umebaini kuna ongezeko la matumizi ya dawa hizo za kulevya kutokana na udhibiti wa dawa zilizokuwa zikitumika awali.
“Katika uchunguzi wetu ambao tulifanya kwenye vijiwe, saluni na maeneo mbalimbali tulibaini watumiaji wakubwa wa skanka ni wanawake. Kuna ambao tulizungumza nao na hata mimi nimezungumza na baadhi ya wanawake wanakiri wanatumia skanka kujiondolea mawazo.
“Ukisikiliza sababu zao wengi wanashindwa kuhimili misongo ya mawazo inayotonakana na changamoto za uhusiano, hivyo wanakimbilia kwenye ulevi huo kwa kile wanachoamini inasaidia kupunguza mawazo,” amesema Lyimo akizungumza na waandishi wa habari leo Novemba 12, 2024 jijini dar es Salaam.
Hata hivyo, ameeleza tofauti na watumiaji hao wanavyoamini kwamba skanka inawapunguzia mawazo, uhalisia ni kwamba inawaingiza kwenye uraibu na hatari ya kupata changamoto ya afya ya akili.
Akizungumzia hilo, daktari bingwa wa magonjwa ya akili katika Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Tanga, Wallace Karata amesema matumizi ya bangi hubadilisha utendaji kazi wa ubongo na kumfanya mtumiaji awe tofauti.
“Kuna magonjwa ya akili ambayo yamejificha, inawezekana mtoto kwenye familia yake kuna ugonjwa wa akili wa kurithi sasa akitumia bangi anaenda kuyaamsha. Hiyo skanka madhara yake ni makubwa na yanatokea kwa haraka zaidi.”
Katika operesheni iliyofanyika kati ya Oktoba na Novemba, DCEA imesema zilikamatwa pia mililita 447 za dawatiba zenye asili ya kulevya kati ya hizo, mililita 327 zilikutwa nyumbani kwa mtuhumiwa eneo la Tabata Kinyerezi.
Mililita nyingine 120 za dawatiba zenye asili ya kulevya aina ya Codein zilikamatwa katika Uwanaja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) zikiwa zinasafirishwa kwenda nje ya nchi.
“Dawa hizo ziliingizwa nchini kinyume cha taratibu zikiwa zimewekwa chapa bandia ya dawa za kuogeshea mbwa na paka ili kuepuka kubainika. Kukamatwa kwa dawa hizi ni ishara ya uwepo wa tatizo la matumizi holela ya dawatiba zenye asili ya kulevya,” amesema Lyimo wa DCEA.
Katika hatua nyingine mamlaka imewakamata watuhumiwa wawili mkoani Dodoma wakiwa na gramu 393 za dawa za kulevya aina ya heroini.
Watuhumiwa hao ni Kimwaga Lazaro (37) na Suleiman Mbaruku (52) anayefahamika kama Nyanda akitajwa kuwa kinara wa biashara hiyo jijini Dodoma.
“Huyu Nyanda anafahamika kama kinara wa biashara ya dawa za kulevya jijini Dodoma, tumekuwa tukimfuatilia kwa muda mrefu na hatimaye tumemkamata,” amesema Lyimo.
Amesema kwa jumla operesheni hiyo imewezesha kukamatwa kilo 1,066.105 za dawa za kulevya, lita 19,804 za kemikali bashirifu, mililita 447 za dawatiba zenye asili ya kulevya na watuhumiwa 58.