Tuendelee kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi – DW – 12.11.2024

Zaidi ya viongozi 90 wa dunia wamekusanyika leo katika siku ya pili ya mkutano huo wa COP29 .

Viongozi ambao hawajahudhuria mkutano huo ni pamoja na Rais wa Marekani Joe Biden, ambaye ahadi zake za kitaifa za kushughulikia mzozo wa mabadiliko ya tabianchi zinaweza kukwama chini ya uongozi mpya wa Rais mteule Donald Trump.

Viongozi wanaohudhuria mkutano wa COP29

Naibu waziri mkuu wa China Ding Xuexiang aliwasili na kulakiwa na Rais wa Azerbaijan Ilham Aliyev. Viongozi wengine, akiwemo Rais wa Maldives Mohamed Muizzu, Rais wa Umoja wa Falme za Kiarabu Sheikh Mohammed bin Zayed Al Nahyan pamoja na waziri mkuu wa Hungary Viktor Orban, pia wamewasili kuhudhuria mkutano huo.Viongozi kutoka Uturuki na Uhispania pia wanahudhuria.

Uwakilishi mkubwa unatarajiwa kutoka kwa mataifa ya visiwa vidogo na pia nchi za bara Afrika. Hii itakuwa mara ya kwanza kwa serikali ya Taliban ya Afghanistan kuhudhuria, ingawa itakuwa tu kama mwangalizi.

Waziri mkuu wa Uingereza, Keir Starmer akizungumza wakati wa mkutano na waandishi wa habari , Samoa, mnamo Oktoba 26,2024
Waziri mkuu wa Uingereza, Keir Starmer Picha: Stefan Rousseau/PA Wire/empics/picture alliance

Akihutubia mkutano huo, Guterres amesema mataifa ya dunia lazima yachangie ufadhili wa kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, la sivyo athari zaidi zitakumba ubinadamu. Katibu huyo mkuu pia ameongeza kuwa wako katika kipindi cha lala salama cha kuweka mikakati ya kuzuia kuongezeka kwa kiwango cha joto la dunia kupita nyuzi joto 1.5 na kwamba hakuna muda wa kupoteza.

Akizungumza leo pembezoni mwa mkutano huo wa COP29, waziri mkuu wa Uingereza Keir Starmer aliutaja mgogoro wa hali ya hewa kama fursa kubwa zaidi kwa ajira ya kizazi kijacho. Starmer pia alitangaza agizo la manunuzi ya thamani ya pauni bilioni 1 ya mitambo.

Mkutano wa kilele wa mazingira COP29 waanza Azerbaijan

Katika mkutano na waandishi wa habari leo, maafisa wa COP29 walitafuta kuzingatia tena lengo kuu la mkutano huo la kukubaliana na mkataba wa hadi dola trilioni moja katika ufadhili wa kila mwaka wahali ya hewa kwa nchi zinazoendelea.

Simon Stiell, mkuu wa sera ya mabadiliko ya tabianchi wa Umoja wa Mataifa, amesema kuziwezesha nchi zote kuchukuwa hatua dhidi ya mabadiliko ya tabianchi ni kwa manufaa kamilifu ya mataifa yote kwasababu mzozo wa hali ya hewa unazidi kuathiri uchumi wa ulimwengu.

 

Related Posts