Wanne wajitosa Urais TOC, yumo Mtaka

Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Anthony Mtaka ni miongoni mwa wagombea wanne waliojitosa kuwania urais kwenye uchaguzi wa Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC).

Wengine ni makamu wa rais wa TOC anayemaliza muda wake, Henry Tandau, Nasra Juma Mohammed na Michael Washa.

Mmoja wa viongozi wa Kamisheni ya uchaguzi huo, ameiambia Mwananchi kwamba wagombea hao watatu wanatoka Bara na Nasra anatokea Zanzibar.

Amesema mbali na urais, nafasi nyingine inayowaniwa ni ya makamu wa rais, na wajumbe 10 ambao nusu ni kutoka Zanzibar na nusu kutoka Bara ambao katika idadi hiyo kila upande unapaswa kuwa na wanawake wawili.

“Kwenye ujumbe kwa Bara waliojitokeza ni 13,” amesema kiongozi huyo wa Kamisheni ambaye hakutaka jina lake litajwe.

Hata hivyo, Mwenyekiti wa Kamisheni ya uchaguzi huo, Ibrahim Mkwawa alipoulizwa amesema mchakato wa kuchukua na kurejesha fomu umefikia tamati jana Novemba 11, 2024 saa 12 jioni.

“Zoezi limefungwa, tunaenda kwenye hatua ya kupitia fomu na kutangaza waliojitokeza ili kama kuna wenye pingamizi waziwasilishe, ingawa ndani ya siku mbili hizi ndipo tutawatangaza waliochukua fomu,” amesema ingawa Mwananchi linafahamu Mtaka, Tandau, Washa na Nasra wamejitosa kuwania urais.

Uchaguzi huo utafanyika Desemba 14 mjini Dodoma, wapiga kura TOC wakimchagua rais, makamu wa rais na wajumbe 10, huku nafasi ya Katibu Mkuu ikiondolewa kwenye nafasi zinazopigiwa kura baada ya Katiba ya TOC kufanyiwa mabadiliko na sasa itakuwa ya kuajiriwa sambamba na nafasi ya mweka hazina.

Uchaguzi huo utatanguliwa na ule wa Kamisheni ya wanamichezo, Desemba 8, kisha wa Olimpians Desemba 10 na kufuatiwa na semina ya Makatibu Wakuu wa Vyama vya Michezo vilivyo chini ya TOC, Desemba 12 mkoani Dodoma.

Katibu wa Olimpians anayemaliza muda wake, Mwinga Mwanjala amesema fomu zinaendelea kutolewa kwa wagombea wa nafasi mbalimbali.

“Nafasi ya mwenyekiti, makamu, katibu mkuu na mweka hazina fomu zinatolewa kwa Sh 20,000 na ile ya ujumbe ni Sh 15,000,” amesema.

Nyota wa zamani wa riadha, Gidamis Shahanga na Suleiman Nyambui ndio mwenyekiti na makamu mwenyekiti wa Olimpians wanaomaliza muda wao.

Related Posts