Mkutano wa kilele wa nchi zaidi ya 50 za Kiarabu na Kiislamu ulikamilika jana katika mji mkuu wa Saudia Riyadh na ulitoa nafasi kwa viongozi hao kuzungumza kwa kauli moja kuhusu machafuko yanayolikumba eneo la Mashariki ya Kati, ikiwa ni zaidi ya mwaka mmoja tangu kuanza kwa vita vya Israel na Hamas katika Ukanda wa Gaza.
Taarifa rasmi iliyotolewa mwishoni mwa mkutano huo ilieleza kuwa amani ya haki na ya kina katika eneo, haiwezi kupatikana bila kukomesha ukaliaji wa kimabavu wa Israel wa maeneo yote ya Waarabu na kuzingatiwa mipaka ya tarehe 4 Juni 1967, ikimaanisha maeneo ya Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu, Jerusalem mashariki, Gaza na eneo la milima ya Golan.
Taarifa hiyo imeyataja pia maazimio ya Umoja wa Mataifa yaliyoitaka Israel kujiondoa katika maeneo hayo, pamoja na Mpango wa Amani wa nchi za Kiarabu wa mwaka 2002, ambao mataifa ya Kiarabu yaliahidi kuwa na mahusiano ya kawaida na Israel ikiwa ingeliafiki makubaliano hayo. Taarifa hiyo imesisitiza kuwa jumuiya ya kimataifa inapaswa kuanzisha mpango madhubuti na kuchukua hatua maalum ili kuwezesha uwepo wa taifa huru la Palestina.
Soma pia: Mataifa ya Kiarabu na Kiislamu yatoa wito wa kusitisha vita Gaza na Lebanon
Viongozi hao wa mataifa karibu 57 ya Kiarabu na Kiislamu wametoa pia wito wa usitishwaji mapigano huko Gaza na nchini Lebanon huku wakilaani pia “uhalifu mbaya na wa kutisha” unaofanywa na jeshi la Israel, wakisema umefanyika “katika muktadha wa uhalifu wa mauaji ya halaiki”.
Viongozi hao wahimiza Israel isitishwe katika Umoja wa Mataifa
Tamko la mwisho la mkutano huo wa kilele limehimiza uhamasishwaji wa kimataifa ili kusitisha uanachama na ushiriki wa Israel katika Umoja Mataifa na kukomesha uvamizi wa Israel katika eneo hilo, huku wakizitaka nchi zote zipige marufuku usafirishaji au uhamisho wa silaha na risasi kwa Israel. Waziri wa Mambo ya Nje wa Saudia Mwanamfalme Faisal bin Farhan ameelezea nia ya mataifa hayo ya kumaliza vita.
” Kwa kuzingatia kuendelea hujuma za Israel katika ardhi za Palestina na kutanua operesheni hizo za kijeshi katika Jamhuri ya Lebanon, mkutano huu wa kilele unakuja kama uthibitisho wa nia ya dhati ya nchi zetu za Kiarabu na Kiislamu kukamilisha juhudi zetu zinazolenga kutuliza mivutano katika eneo hili ili kukomesha uhalifu unaofanywa na vikosi vya uvamizi na kuondoa vikwazo vinavyozuia kuingia kwa misaada ya kibinadamu, panoja na kuunga mkono suluhisho la mataifa mawili kama njia pekee ya kufikia suluhisho la haki na la kudumu ambalo litadumisha amani katika eneo hilo, ” alisema Farhan.
Soma pia: Viongozi wa Kiarabu na Kiislamu wakutana Saudia kujadili mzozo wa Mashariki ya Kati
Kundi la Hamas limeyahimiza mataifa ya Kiarabu na Kiislamu kutekeleza ahadi hizo kwa vitendo na kusisitiza kuwa kuanzishwa kwa taifa huru la Palestina na Jerusalem kama mji mkuu wake kutahitaji juhudi za haraka ili kuilazimisha Israel kukomesha kile ilichokiita “uchokozi na mauaji ya kimbari” dhidi ya watu wa Palestina.
Hata hivyo, serikali ya Israel yenye misimamo mikali ya mrengo wa kulia inayoongozwa na Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu bado inapinga vikali uwepo wa taifa huru la Palestina na waziri mpya wa mambo ya nje wa Israel, Gideon Saar, amepuuzilia mbali matarajio hayo akisema kwa sasa “hayatekelezeki”. Waziri wa Fedha wa Israel Bezalel Smotrich alienda mbali zaidi na kusema atashinikiza kunyakuliwa rasmi kwa baadhi ya maeneo ya Ukingo wa Magharibi ifikapo mwaka 2025.
(Vyanzo: AP, DPAE, AFP)