Dodoma. Kilio cha gharama za usafirishaji wa mizigo, mfumuko wa bei na uharibifu wa barabara nchini, Serikali imevipatia ufumbuzi kwa kufungamanisha reli zote tatu za MGR (ya zamani), Tazara na reli ya kisasa (SGR) kupitia Kidatu mkoani Mogororo.
Mpango huo ni moja ya kazi zitakazotekelezwa na Wizara ya Uchukuzi kwa mwaka wa fedha 2024/25.
Tangu ubinafsishaji wa Shirika la Reli Tanzania (TRC) na shughuli za uendeshaji wa huduma za usafiri wa reli kuchukuliwa na kampuni ya RITES ya India kwa kipindi cha miaka 25, kampuni hiyo haikuweza kufanya vizuri na Serikali iliamua kusitisha mkataba wa ukodishwaji mwaka 2010 na kuanzia Julai 22, 2011 kampuni ilirudi mikononi mwa Serikali kwa umiliki wa asilimia 100.
Lakini hali usafiri haikuwa nzuri na mizigo mingi ilisafiri kwa malori huku abiria wakitumia mabasi.
Wizara ya Uchukuzi leo Jumatatu, Mei 6, 2024 imeliomba Bunge kuidhinisha Sh2.7 trilioni kwa ajili ya matumizi ya kawaida na uekelezaji wa miradi ya maendeleo. Kati ya fedha hizo Sh114.7 bilioni ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida na Sh2.6 trilioni ni kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Wazi wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa ameliambia Bunge katika mwaka wa fedha 2023/24, wizara hiyo ilitengewa Sh1.9 trilioni kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo na hadi kufikia Machi, 2024 Sh1.7 trilioni sawa na asilimia 89.12 ya bajeti ya Maendeleo iliyoidhinishwa zilitolewa.
Amesema katika mwaka ujao wa fedha Serikali itaanza kutekeleza mkakati wa kuhakikisha SGR inaanza kufanya kazi na kujiendesha kibiashara.
“Lengo la Serikali ni kutoendelea kutumia ruzuku kuendesha reli ya SGR mara baada ya kukamilika,” amesema.
Profesa Mbarawa amesema ili kufikia azma hiyo, miongoni mwa hatua zitakaochukuliwa na Serikali ni kufungamanisha reli zote tatu za MGR, Tazara na SGR kupitia kituo cha usafirshaji cha Kidadu (Kidatu Transhipment).
“Reli zote hizo zitawasiliana kwa kuweka ‘Gantry Crane Storage Facilities’ pamoja na kuimarisha reli ya Morogoro, Kilosa hadi Kidatu kilometa 108. Uunganishaji huu utawezesha usafirishaji wa mizigo kutoka kusini mwa Afrika mpaka mikoa yote ya Tanzania pamoja na nchi jirani.
“Kufungamanisha Bandari Kavu za Kwala, Isaka, Bandari za Mwanza na Kigoma na hatimaye Bandari za Dar es Salaam na Tanga kwa kuunganishwa na MGR na SGR,” amesema Profesa Mbarawa.
“Njia hii pamoja na manufaa mengine itaongeza wigo wa matumizi ya reli kwa mizigo ya ndani pamoja na inayotoka na kuingia nchini,” amesema Profesa Mbarawa.
Amesema tofauti na ilivyozoeleka Tanzania imekuwa ikitegemea mizigo inayoletwa kutoka nje ya nchi, hivyo ili kuhakikisha kuwa kunakuwa na upatikanaji wa mizigo ndani ya nchi, Serikali kupitia Wizara itatekeleza mkakati wa kuchochea upatikanaji wa mizigo kwa kuhamasisha shoroba za kiuchumi.
Profesa Mbarawa amesema kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wakiwemo Taasisi ya Ushoroba wa Kati (Central Corridor Transit Transport Facilitation Agency – CCTTFA), Mfuko wa Chakula Duniani (WFP), na Watumiaji wakubwa wa Bandari za Tanzania wa ndani na nje wamebaini Shoroba kubwa tatu ambazo zitaweza kuchochea upatikanaji wa mizigo ndani ya nchi.
“Shoroba zilizobainishwa kuwezesha upatikanaji ni Ushoroba wa Baridi ambao utahamasisha mizigo ya nyama, samaki, matunda, mboga na maua; Ushoroba wa Njano kwa ajili ya mizigo ya madini; na Ushoroba wa Kichele ambao utahusisha mizigo mingine, hususan mizigo mikubwa pamoja na mizigo ya viwandani na kilimo ikiwemo pembejeo.
Amesema utekelezaji wa mkakati huu utawezesha kupatikana kwa mizigo mingi ndani ya nchi na kuwezesha TRC kuingia makubaliano na kampuni kubwa na wateja wa muda mrefu.
“Hatua hii itawezesha TRC pia kuendelea kuratibu usafirishaji kwa kutumia wabia wa sekta binafsi kupitia utaratibu wa Open Access,”alisema.
Profesa Mbarawa aliliambia Bunge vipaumbele vya wizara kwa mwaka wa fedha 2024/2025, vinajumuisha kuendeleza ujenzi na uendeshaji wa SGR na kuboresha miundombinu ya reli ya MGR na CGR, pamoja na ununuzi wa vifaa.
Amesema pia Wizara itaboresha uendeshaji wa ATCL, kuimairisha miundombinu ya viwanja vya ndege na kujenga viwanja vipya, kuimarisha usafiri, usalama na mawasiliano katika maziwa makuu nchini.
Kuhusu usafiri wa ardhini, alisema Serikali itaendelea kuimarisha usalama, udhibiti na utoaji wa huduma za usafiri na usafirishaji wa abiria na mizigo, kuboresha miundombinu na uendeshaji wa bandari nchini ikiwa ni pamoja na uendelezaji wa bandari kavu.
Profesa Mbarawa alizungumzia changamoto katika utekelezaji wa majukumu yao kwa mwaka 2023/24, Wizara ya Uchukuzi inakabiliwa na changamoto mbalimbali.
“Baadhi ya changamoto hizo na mikakati ya kuzitatua ni mahitaji makubwa ya fedha za utekelezaji wa miradi mingi ya uchukuzi kuhitaji fedha nyingi (capital intensive) katika utekelezaji wake.
“Mathalan, mradi wa SGR utagharimu takriban Sh23 trilioni hadi kukamilika kwake,” alisema.
Alisema mkakati wa kulitekeleza hilo ni kuendelea kuhamasisha sekta binafsi kutekeleza baadhi ya miradi inayohitaji uwekezaji mkubwa na hivyo kupunguza gharama kwa Serikali.
Wakichangia mjadala wa bajeti hiyo, Mbunge wa Segerea (CCM) jijini Dar es Salaam, Bonnah Kamoli alisema mradi wa SGR umefunga barabara kwa zaidi ya miaka miwili na nusu na kusababisha shida kwa wananchi, wakiwamo wafanyabishara.
Pia, amesema mradi huo umesababisha maji kujaa kwenye makazi ya watu na amemuomba Waziri Mbarawa kulishughulikia tatizo hilo.
Kamoli pia amesema malipo ya fidia kwa wakazi wa Kipunguni waliopisha ujenzi wa uwanja wa ndege hayajalipwa na Serikali kwa takriban miaka 27 sasa huku, wakazi wake wakiishi kama wakimbizi ndani ya nchi yao.
Mbunge wa Nkasi (Chadema), Aidan Kenan amelalamikia kukosekana usafiri kwenye Ziwa Tanganyika akisema ni miaka minane sasa Wizara hiyo imekuwa ikiwataja kwenye vitabu lakini hakuna utekelezaji.
Kenan amesema kukosekana kwa meli ya mizigo kunaikosesha Serikali mapato kwa kuwa asilimia 60 ya mizigo kutoka Tanzania inakwenda Jamhuri ya Kidemokrasi ya Cong (DRC).
Naye mbunge wa Kilombero (CCM), Abubakar Asenga aliomba Wizara hiyo kulipa madeni ya wakandarasi kwa kuwa miradi mingi imekwama.
Amesema wameshuhudia kuwepo madeni ya wakandarasi maeneo mengi ya nchi na wanalalamika hawajalipwa na ameiomba Serikali ipunguze madeni yao ili sekta iweze kwenda vizuri.
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge Miundombinu, Moshi Kakoso akisoma maoni ya kamati alibainisha uchache wa fedha katika baadhi ya miradi ulivoyosababisha kusuasua kwa miradi hiyo.
Ameutaja mradi wa ujenzi wa Kituo cha Kikanda cha Kuratibu Utafutaji na Uokoaji Majini (MRCC) kwamba unatakiwa kukamilika ifikapo Novemba, 2024, lakini hadi kufikia Machi, 2024 fedha iliyolipwa kutekeleza mradi ilikuwa Sh953.9 bilioni sawa na asilimia 20 tu.
“Mapokezi yasiyoridhisha ya fedha za mradi, kwa sehemu kubwa yameathiri utekelezaji wa mradi ambapo hadi Kamati inafika uwandani kwa ajili ya ukaguzi, ujenzi wa mradi ulikuwa ni asilimia 10.
Kakoso aliutaja ujenzi wa mradi wa SGR kipande cha tano (Isaka- Mwanza) kwamba hadi kamati inatembelea Machi, 2024, Serikali ilikuwa imeshafanya malipo kwa Mkandarasi ya Sh1.3 trilioni sawa na asilimia 40.53 ya gharama za mradi huku maendeleo ya mradi yakiwa yamefikia asilimia 54.01.