Mwenyekiti wa Bodi ya Taasisi ya Kimataifa inayoshughulikia masuala ya Elimu Duniani (GPE), Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete akizungumza na Viongozi na Watumishi wa Taasisi hiyo katika Makao Makuu ya GPE yaliyopo Ofisi za Benki ya Dunia, Washington, Marekani. Pembeni yake ni Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya GPE Bi. Christine Hogan na Afisa Mtendaji Mkuu Bi. Laura Frigenti.
MWENYEKITI wa Bodi ya Taasisi ya Kimataifa inayoshughulikia masuala ya Elimu Duniani (GPE), Rais Mstaafu Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete leo amekutana na Viongozi na Watumishi wa Taasisi hiyo katika Makao Makuu ya GPE yaliyopo Ofisi za Benki ya Dunia, Washington, Marekani.
Katika kikao cha Viongozi wa GPE kilichohudhuriwa na Makamu Mwenyekiti wa Bodi, Christine Hogan, Afisa Mtendaji Mkuu wa GPE, Laura Frigenti na Naibu Afisa Mtendaji Mkuu, Charles North, Dkt. Kikwete aliongoza majadiliano ya maandalizi mkakati wa 5 wa GPE wa kupata fedha za kuendesha Taasisi hiyo na miradi yake iliyopo katika nchi zaidi ya 90 duniani. Mkakati wa 4 wa GPE wa kipindi cha 2021 – 2025 wenye bajeti ya Dola za Marekani bilioni 4.2 unamalizika mwakani.
Baada ya kikao hicho, Dkt. Kikwete alipata pia fursa ya kukutana na Mamta Murthi, Makamu wa Rais wa Benki ya Dunia ambapo walijadili masuala mbalimbali ya kukuza ushirikiano kati ya Benki ya Dunia na GPE.
Aidha, Rais huyo Mstaafu alipata fursa ya kukutana na kuzungumza na watumishi wa GPE wanaofanya kazi Makao Makuu ya Ofisi hizo, ikiwa ni mara ya kwanza tangu kumalizia kwa gonjwa la UVIKO 19.