Dar es Salaam. Katika jitihada za kuongeza matumizi ya nishati safi katika shughuli mbalimbali, wadau mazingira wamekuja na njia tofauti za kuhakikisha watu wanahama katika utegemezi wa nishati walizozizoea.
Miongoni mwa hatua za hivi karibuni ni kuwa na matumizi ya gesi asilia (CNG) na umeme katika vyombo vya moto ambavyo awali vilikuwa vikitumia nishati ya mafuta, hata hivyo kikwazo kikubwa kinachotajwa ni gharama kubwa za mifumo hiyo.
Kutokana na changamoto hiyo, baadhi kampeni ya kuhamasisha matumizi ya CNG kwenye bajaji imezinduliwa ikilenga zaidi kufadhili ununuzi wa bajaji zinazotumia nishati hiyo ili kupunguza zile zinazotumia mafuta (ambazo ndizo zinazotumika kwa wingi sasa).
Kampeni hiyo ya utunzaji wa mazingira chini ya kampuni ya Watu Credit (Tanzania) Limited imeanza kufanya kufadhili ununuzi wa bajaji za CNG na lengo ni kuwezesha ununuzi wa bajaji 1,000 hadi mwisho wa mwaka huu.
Katika uzinduzi huo Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo, anasisitiza juu ya umuhimu wa ushirikiano kati ya serikali na sekta binafsi ili kutimiza lengo la maendeleo endelevu la saba (7) linalohakikisha upatikanaji wa kupata nishati endelevu, safi na nafuu ifikapo mwaka 2030 kwa kila mtu.
”Tuko hapa leo kudumisha dhamira yetu ya wazi ya kukuza matumizi ya magari ya miguu mitatu yanayoendeshwa kwa gesi asilia (CNG) na hata yale yanayotumia umeme, na hivyo kupunguza utegemezi wa mafuta yanasababisha ongezeko la hewa ukaa iletayo ongezeko la joto duniani huku sekta ya usafirishaji ikichangia kwa kiasi kikubwa uchafuzi wa mazingira’.
Mkurugenzi Mkazi wa Watu Credit (Tanzania) Limited, Rumisho Shikonyi, amesema kuhamia kwenye nishati safi ni muhimu kwani inasaidia kulinda mazingira, kwa sababu mustakabali wa sayari yote unategemea hatua tunazochukua leo.
“Watu wamekuwa wakifanya kazi kuelekea lengo hili, wakifadhili bajaji zaidi ya 200 zinazoendeshwa kwa gesi asilia zenye thamani ya Sh2.2 bilioni katika miezi miwili iliyopita pekee,” amesema Sikonyi.