Dar es Salaam. Tanzania na Uingereza zimesaini hati za makubaliano ya nyongeza kuchangia Mfuko wa Kusaidia Sekta ya Afya (HBF) ya Pauni milioni 10 (Sh34 bilioni) kuwezesha utoaji huduma bora za afya nchini kuanzia mwaka 2024 hadi 2029.
Fedha hizo zitatumika katika ununuzi ukiwamo wa vifaatiba vya teknolojia ya hali ya juu, dawa, kuboresha huduma kwenye zahanati, hospitali za wilaya na vituo vya afya.
Asilimia 80 ya Watanzania wanatumia vituo hivyo.
Hati za makubaliano zimesainiwa leo Novemba 12, 2024 jijini Dar es Salaam katika ukumbi wa ofisi za Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR). Utiaji saini umehudhuriwa na viongozi wa Serikali na wawakilishi wa wadau.
Akizungumza baada ya kusaini hati hizo, Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Dk Natu Mwamba amesema wanalenga kutoa huduma bora za afya nchini, zikiendana na utekelezaji wa mpango mkakati wa tano wa sekta ya afya kuanzia mwaka 2021 hadi 2026 unaohakikisha hakuna mtu anakosa huduma ya afya.
Amesema Serikali ya Uingereza ni mmoja wa washirika wa maendeleo wanaochangia Mfuko wa Kusaidia Sekta ya Afya kwa mujibu wa makubaliano ya awali kati ya Tanzania na washirika wa maendeleo yaliyosainiwa Julai 2021.
Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Dk John Jingu amesema mfuko tayari umesaidia huduma za afya katika hospitali za wilaya na vijiji tangu kuanzishwa kwake mwaka 1999.
“Hivi sasa tunazungumzia huduma ya bima ya afya kwa wote, tunachotaka ni kujenga uwezo wa watu kwenda kupata huduma ambazo zinahitajika kuwa imara na zenye ubora. Mfuko huu ni muhimu katika kufikia utoaji huduma kila kona,” amesema.
Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tamisemi, Dk Grace Magembe amesema takwimu za afya zinaonyesha asilimia 60 hadi 70 ya wanaotumia huduma za afya nchini ni watoto chini ya miaka mitano, rika balehe na wajawazito, hivyo fedha hizo zinaenda kuwanufaisha.
“Hii itazidi kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi. Kwa sasa tumepunguza vifo kutoka 556 kwa kila vizazi hai 100,000 hadi kufikia vifo 104,” amesema.
Amesema tangu kuanza ushirikiano na wadau kupitia mfuko wa kusaidia sekta ya afya, Serikali imeongeza kwa idadi kubwa vituo vya afya, zahanati, hospitali za wilaya na kurahisisha upatikanaji wa huduma.
Ameeleza Watanzania asilimia 65 hadi 70 wanapata huduma ndani ya kilomita tano kutoka wanapoishi.
Mkurugenzi wa Maendeleo kutoka Ubalozi wa Uingereza nchini, Kemi Williams amesema Serikali ya Taifa hilo inafahamu umuhimu wa kufikia huduma za afya kwa wote na kuna haja ya kuwa na mifumo ya afya imara, inayoweza kuhimili changamoto kwa njia ya kushirikiana.
“Huduma za afya kwa wote maana yake ni kuwa watu wote, popote walipo au wanapoishi, wanapata huduma bora za afya wanapozihitaji na mahali zinapohitajika bila kuangalia hali zao za kifedha,” amesema.
“Tunathamini jitihada za kushughulikia mapungufu katika rasilimaliwatu ili kusaidia kufikia malengo haya na washirika wataendelea kutoa msaada wa kiufundi ili kuboresha ubora wa huduma za afya ya msingi,” amesema.
Mratibu wa mfuko wa afya wa pamoja na mwakilishi wa ubalozi wa Uswisi, Franziska Freiburghaus amesema ushirikiano huo unaenda kuboresha zaidi utoaji huduma ya afya ambao ni jambo muhimu kwa Watanzania.