Wamarekani hawajawa tayari kuongozwa na Rais mwanamke

Wapenzi wa safu hii, niko jijini Washington D.C, mji mkuu wa Marekani, pamoja na mambo mengine nimepata fursa ya kuushuhudia uchaguzi wa Marekani, nchi inayoitwa “The Biggest Democracy” kumaanisha kuwa ni demokrasia kubwa kwa sababu ilipata uhuru wake Julai 4, 1776.

Wagombea wakuu ni Kamala Harris anayewakilisha chama cha Democrats ambaye pia ni Makamu wa Rais wa sasa na Donald Trump wa chama cha Republican, ambaye aliwahi kuwa rais wa Marekani na akafanya vituko vingi.

Matokeo ni, pamoja na vituko vyake vyote, Wamarekani wamemchagua tena Donald Trump na kumtosa Kamala Harris.

Moja ya sababu za Wamarekani kumchagua tena Trump, licha ya vituko vyake, lakini pamoja na mambo mengine, Wamarekani wameamua kumchagua tena Trump, kwa sababu ni mgombea mwanamume, kuliko kumchagua mgombea mwanamke.

Hivyo, pamoja ni jina kubwa la nchi ya Marekani kuitwa demokrasia kubwa, lakini bado inakabiliwa na udhaifu mkubwa wa ubaguzi wa mfumo dume.

Mara ya kwanza kwa Donald Trump kushinda urais, alishindana na mgombea mwanamke, Hilary Clinton, mke wa aliyekuwa Rais wa Marekani, Bill Clinton.

Kwa kuwa hiyo ndiyo ilikuwa mara ya kwanza kwa mwanamke kugombea urais Marekani, Trump alisema maneno fulani ya udhalilishaji kwa jinsia ya kike, hivyo aliposhinda urais, Wamarekani walionyesha bado hawajawa tayari kutawaliwa na Rais mwanamke.

Chama cha Democrats kilipoamua kumsimamisha tena mgombea mwanamke kwenye uchaguzi wa mwaka huu na Donald Trump akaamua kugombea tena, ikitarajiwa safari hii, Wamarekani watamchagua Rais wa kwanza mwanamke kwa sababu vituko vyake wanavijua.

Matokeo yalipotangazwa, Trump alishinda uchaguzi huo na kuushangaza ulimwengu. Kiukweli mimi ni miongoni mwa tuliopigwa butwaa, na kupata bumbuwazi na matokeo haya ya uchaguzi wa Marekani.

Nikajiuliza kuwa inawezekana hawa Wamarekani nimewaona kama ni majitu majinga ya ajabu kwa kumchagua tena Rais mwanamume yuleyule mwenye vituko vya ajabu na vituko vyake wanavijua na bado wakamchagua.

Wamarekani wameamua, kuliko kumchagua rais mwanamke, wakaamua kumtosa mwanamke na kumchagua rais mwanamume kwa sababu tu ya kugubikwa na ubaguzi wa mfumo dume.

Japo ni demokrasia kumchagua mgombea yeyote kwa sababu yoyote au hata bila sababu yoyote, bali ni kumpenda tu, lakini sio demokrasia ya kweli kutokumchagua mgombea fulani mwenye sifa zote, lakini hachaguliwi kutokana na jinsia yake, huo ni ubaguzi.

Matokeo haya ya uchaguzi wa Marekani, yana uhusiano na uchaguzi mkuu wetu wa mwaka 2025, hivyo natoa wito kwa sisi wa Tanzania, tuyapokee matokeo haya na kuyachukulia kama ni fursa kwa Tanzania kuifundisha dunia demokrasia ya kweli.

Kwa vile mwakani, 2025, Tanzania tunafanya uchaguzi mkuu wa rais na wabunge, na tayari kuna chama kimoja kimeisha tangaza nia kwa kauli na matendo ya utaratibu wake wa ndani wa mserereko, kitamsimamisha mgombea mwanamke.

Kwa vile Tanzania imepata Rais mwanamke kwa kudra tu za Mwenyezi Mungu, kufuatia lile tukio la Machi 17, 2021, lakini Watanzania walikuwa bado hawajawa tayari kuchagua Rais mwanamke, hivyo uchaguzi wa mwaka 2025, macho ya dunia yatakuwa Tanzania.

Mnaonaje kama hiyo 2025, tutaionyeshea Marekani na dunia kwa jumla kuwa Tanzania ni wakomavu zaidi wa demokrasia na tunaweza kufanya demokrasia ya kweli bila ya ubaguzi mbaya wa jinsia na kuukataa mfumo dume kwa Watanzania kuonyesha wanaweza kuchagua kiongozi wao bila kugubikwa na mfumo dume na ubaguzi wa jinsia?

Hivyo, Tanzania tuchangamkie fursa ya kuwa mwalimu wa demokrasia ya kweli kwa Wamarekani na dunia kwa kufanya maandalizi kamambe ya kuwaandaa Watanzania kuchagua Rais mwanamke, na sababu za kuchaguliwa Rais mwanamke, sio kuchaguliwa kwa sababu ya jinsia yake ya kike, bali awe amechaguliwa kwa sababu ya uwezo wake wa urais na uongozi.

Siyo vema kumchagua mtu ambaye hana uwezo, lakini tumchague tu kwa kumhurumia kwa sababu ni mwanamke, lakini pia siyo vema, kutokumchagua mtu mwenye sifa zote na uwezo lakini kumbe ni mwanamke.

Tuyatumie matokeo ya uchaguzi wa Marekani kama shamba darasa la demokrasia ya kweli 2025.

Related Posts