Kibaha. Wakurugenzi wa mamlaka za serikali za mitaa nchini kote leo Mei 6, 2024, wameanza mafunzo ya siku tatu yenye lengo la kuwaongezea mbinu za kuboresha utekelezaji wa majukumu yao mahala pa kazi.
Mada zitakazotolewa wakati wa mafunzo hayo yanayofanyika Kibaha mkoani Pwani ni pamoja na masuala ya rushwa na ubadhirifu katika mamlaka za Serikali za mitaa, mambo muhimu katika maandalizi ya uchaguzi wa Serikali za mitaa na mwelekeo wa utoaji wa mikopo kwa vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu.
Hayo yamebainishwa na Naibu Katibu Mkuu Tamisemi, Sospiter Mtwale alipokuwa anazungumza kabla ya kumkaribisha Katibu Mkuu wa Tamisemi, Adolf Ndunguru kwa ajili ya ufunguzi wa mafunzo hayo.
“Mada zingine ni utunzaji wa siri za Serikali, hoja za ukaguzi na upungufu zinazobainika katika ukaguzi. Wakurugenzi watapata wasaa wa kuwasilisha changamoto zinazowatatiza mahala pa kazi ili tuangalie namna ya kuzitafitia ufumbuzi,” amesema.
Mtwale ameongeza kuwa imani ya Serikali ni kwamba baada ya mafunzo hayo wakurugenzi wataongeza ufanisi katika utendaji wao wa kazi, hali itakayoleta msukumo wa maendeleo nchini.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo, Ndunguru amesema kuwa lengo la Serikali ni kuona wakurugenzi wa halmashauri wanasimamia ukusanyaji wa mapato kwa ufanisi kwenye maeneo yao ya kazi pamoja na kuhakikisha pesa za miradi zinatumika kama inavyotakiwa.
“Hakikisheni pesa zinazotengwa kwa ajili ya miradi ya maendeleo mnazipeleka mapema na kusimamia ili zifanye kazi kulingana na matakwa ya Serikali ili kuwaondolea wananchi changamoto,” amesema.
Baadhi ya washiriki wa mafunzo hayo wamesema kuwa yamekuja kwa muda mwafaka kwani yatawaongezea ufanisi wa utendaji wa kazi kwa maslahi ya umma.
“Mada zote zinaonekana zitakuwa na msaada mkubwa kwetu katika kuimarisha utendaji wa kazi, hivyo mafunzo haya yataleta tija kwetu,” amesema Ramadhani Posi, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Chalinze.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Itigi, Justuce Kijazi amesema kuwa mafunzo hayo yatawaongezea tija ya utendaji wa kazi na faida nyingine watakayopata ni kubadilishana uzoefu wa kufanya kazi hasa kupitia changamoto watakazowalisha kwenye kikao kazi hicho.